Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu haina umri wala kuchelewa, wala mwisho: Mkimbizi Philip Long'olea

Mvulana mdogo mkimbizi aliyevaa sare ya shule akizungumza akiwa ameketi nje ya jengo la shule huko Kakuma, Kenya.
UNICEF Philip kijana mkimbizi mwenye umri wa miaka 17 ambaye sasa ndio kwanza yuko darasa la 5 katika shule maalum ya msingi ya Kalobeyei kwenye kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya.

Elimu haina umri wala kuchelewa, wala mwisho: Mkimbizi Philip Long'olea

Utamaduni na Elimu

Migogoro, vita na mabadiliko ya tabianchi mara nyingi vimekuwa vikiwapora watoto fursa ya elimu na hata kusambaratisha mustakbali wao na wengi wanajikuta wakiishia kwenye makambi ya wakimbizi linasema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF. Kwa kulitambua hilo shirika hilo linaendesha miradi mbalimbali ya kuhakikisha watoto waliokosa elimu hata kama wana umri mkubwa wanapewa fursa ya pili kusoma kama ilivyokuwa kwa mkimbizi Philip Lon’golea kutoka Sudan aliyekimbilia Uganda kwanza lakini sasa yuko kwenye kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya.

”Nilikuwa nachunga mbuzi Uganda , na genge la wezi wa mbuzi walinikuta nachunga peke yangu mbuzi wakataa kuiba na mmoja akanikata na shoka katikati ya kichwa, nikazimia na nikalazwa hospitali ya Uganda na asubuhi wakasema hapa hakuna anayeweza kufanya upasuaji wa kichwa chako kisha nikapelekwa Eldoret Kenya nikapigwa x-ray na asubuhi kichwa kikawa kimeshonwa” Amesema Philip, kijana mkimbizi mwenye umri wa miaka 17 ambaye sasa ndio kwanza yuko darasa la 5 katika shule maalum ya msingi ya Kalobeyei kwenye kambi ya wakimbizi ya Kakuma alipowasili baada ya kutoka hospitali kwa msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR. Wakati wote alipokuwa akichunga mbuzi Uganda hakusoma darasa hata moja

“Mwaka 2020 ndio nilijiunga na shule nilifika hapo sikujua hata kuandika na wala sikujua moja ni nini. Niligawiwa sare za shule hapo, nikapewa kalamu, kichongeo na kisha nikapata mawazo ya kusoma kwa bidi hapo. Tulipoingia darasa la pili tulikuwa na mwalimu wetu anaitwa Mwendo alianzisha program nyingine kuhusu kukabili msongo wa mawazo ambayo inasaidia ukiwa na msongo ufanye nini ili uweze kuondokana nao”

Wanafunzi wakimbizi waliovalia sare za bluu nyepesi wakipokea maji kutoka kwenye chombo kikubwa katika makazi ya Kalobeyei nchini Kenya.
UNICEF Philip kijana mkimbizi mwenye umri wa miaka 17 ambaye sasa ndio kwanza yuko darasa la 5 katika shule maalum ya msingi ya Kalobeyei kwenye kambi ya wakimbizi ya Kakuma Kenya.

Program hiyo ni sehemu ya mradi unaoendeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF wa Elimu harakishi au Accelerated Education Programme kwa ufadhili wa serikali ya Uholanzi ukiwalenga watoto wenye umri mkubwa ambao hawajasoma ili waweze kupata elimu. Sara Musengya ni afisa elimu wa UNICEF Kenya anasema “ Lengo la mradi huu ni kuwaweka katika msitari wa elimu watoto na vijana ambao walikosa masomo  kwa muda mrefu kutokana na sababu za mizozo, uhamiaji, na mabadiliko ya tabianchi.”

Wengi wanaonufaika na mradi huu ni wakimbizi kama Philip ambaye ana ndoto kubwa akimaliza masomo

“Nikikua nataka kuwa Daktari kwa sababu vile nilivyozunguka huko wakati nilikuwa mgonjwa, kungekuwa na dakrati ningeweza kusaidiwa haraka.”

Kwa mujibu wa UNICEF watoto 7200 wamefikiwa na mradi huo kambini Kakuma na 432 wamefanikiwa kuhitimu program hiyo na kwenda shule za kawaida.