Baraza la Usalama laelezwa changamoto za kiusalama Lebanon na Syria
Baraza la Usalama laelezwa changamoto za kiusalama Lebanon na Syria
Jean-Pierre Lacroix, ambaye ni Mkuu wa Idara ya Umoja wa Mataifa ya Operesheni za Ulinzi wa Amani, amesema kurejesha imani na kuimarisha usalama na utulivu kwenye Mstari wa Buluu ambalo ni eneo tenganishi kati ya Lebanon na Israeli ni jambo muhimu sana kwa jamii zilizo kusini mwa Lebanon na kaskazini mwa Israel.
Akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo New York, Marekani kwa njia ya video, ameelezea kuwa kwa kujengea uwezo wa kiulinzi kusini na dhamira mpya kutoka Jeshi la Lebanon kutekeleza wajibu wao chini ya azimio namba 1701, la Baraza la Usalama, kunatarajiwa kuboreshwa zaidi kwa ushirikiano na Ujumbe wa Mpito wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon (UNIFIL).
Vikosi vya Israeli viondoke Lebanon
Lacroix amebainisha kuwa uwepo wa vikosi vya jeshi la Israeli (IDF) ndani ya ardhi ya Lebanon ni ukiukwaji wa azimio hilo namba 1701. Israeli imekuwa inadai uweko wake ndani ya Lebanon ni kukabiliana na wanamgambo wa Hizbollah.
Ametoa wito kwa IDF kuondoka mara moja bila kuchelewa kwa mujibu wa makubaliano yaliyomo kwenye sitisho la mapigano la hivi karibuni.
Lebanon yataka Israeli iheshimu azimio 1701; Israeli yasisitiza haki ya kujilinda
Roua Zoghbi, Afisa katika Uwakilishi wa Kudumu wa Lebanon katika Umoja wa Mataifa, amesisitiza ahadi ya nchi yake kutekeleza azimio namba 1701 na kutaka Israel kuheshimu mipaka ya kimataifa na mamlaka ya Lebanon.
Kwa upande , Danny Danon, Mwakilishi wa Kudumu wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa amesisitiza haki ya Israel kujilinda dhidi ya vitisho vyovyote vya usalama. Alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za kuzuia uingizaji wa silaha kwa wanamgambo wa Hizbollah.
Kinachoendelea milima ya Golani chakwamisha UNDOF
Majadiliano pia yalijikita katika eneo la milima ya Golan, mpakani mwa Syria na Lebanon, ambapo Meja Jenerali Patrick Gauchat wa shirika la Umoja wa Mataifa la Usimamizi wa Mkataba wa kusitisha mapigano, UNTSO ameeleza kuwa IDF inaendelea kufanya kazi za ujenzi na kuweka vifaa vya mawasiliano katika eneo la tenganishi, jambo ambalo linakiuka Mkataba wa 1974 wa Kutenganisha Vikosi kati ya Israel na Syria.
Meja Gauchat ambaye anakaimu nafasi ya Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa huko milima ya Golani, UNDOF, unaosimamia utekelezaji wa mkataba wa mwaka 1974, amesisitiza kuwa ujumbe huo unakabiliwa na changamoto za kiutendaji kutokana na mvutano kwenye eneo linalotenganisha Syria na Israeli.
Naye Mwakilishi wa Kudumu wa Syria kwenye Umoja wa Mataifa, Koussay Aldahhak, amelaani uwepo wa Israel katika maeneo ya Syria na akataka Baraza la Usalama kulazimisha kuondolewa mara moja kwa vikosi vya Israel katika ardhi ya Syria.