WHO yaishika mkono Tanzania kuchukua hatua kufuatia shuku ya mlipuko wa homa ya Marburg
WHO yaishika mkono Tanzania kuchukua hatua kufuatia shuku ya mlipuko wa homa ya Marburg
Kufuatia ripoti za kesi zilizoshukiwa za homa ya virusi vya Marbug nchini Tanzania, Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO limeimarisha utayari wake kuisaidia serikali ya Tanzania katika kuchunguza na kuchukua hatua kwa haraka kukabiliana na hali hiyo.
Mamlaka za kitaifa za afya Tanzania zimepeleka kikosi cha wataalamu katika mkoa wa Kagera, kaskazini-magharibi mwa nchi, ambako kesi hizo zimeripotiwa. WHO pia inakusanya rasilimali za kiufundi na vifaa ili kusaidia juhudi zinazoendelea.
Uchunguzi wa haraka ni muhimu kwa hatua za haraka
Taarifa ya WHO iliyotolewa leo mjini Brazzaville Jamhuri ya Congo imesisitiza umuhimu wa taarifa za haraka kuhusu matokeo ya uchunguzi ili kuwezesha hatua za haraka kudhibiti mlipuko huo.
Dkt. Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa WHO amesema “Tupo tayari kusaidia serikali katika juhudi zake za kuchunguza na kuhakikisha hatua za haraka na madhubuti zinachukuliwa.”
Ameongeza kuwa uzoefu wa dharura za awali unatoa nafasi ya kuimarisha hatua
kwa kutumia uwezo wa kitaifa ulioimarishwa kutokana na uzoefu wa kukabiliana na dharura za afya zilizopita, WHO inaweza kuimarisha juhudi za kulinda jamii. Shirika hilo pia limeahidi kuendeleza jukumu lake la kutetea msaada na mshikamano wa kimataifa katika kukabiliana na changamoto hii.
Historia ya Marburg nchini Tanzania
Kwa mujibu wa shirika la WHO, Tanzania iliripoti mlipuko wa kwanza wa virusi vya Marburg mwezi Machi 2023, pia katika mkoa wa Kagera.
Kupitia hatua madhubuti, mlipuko huo uliweza kudhibitiwa na kutangazwa kumalizika ndani ya miezi miwili.
Marburg ni ugonjwa wa virusi unaosababisha homa kali ya kutokwa damu, ugonjwa ambao una mfanano na virusi vya Ebola.
Ugonjwa huu huanza ghafla, na dalili zake ni Pamoja na homa kali, maumivu makali ya kichwa, na udhaifu Mkubwa na dalili za kutokwa damu mara nyingi huonekana ndani ya siku saba.
Virusi vya Marburg huenezwa kwa binadamu kutoka kwa popo wanaokula matunda na huenea miongoni mwa binadamu kupitia mawasiliano ya moja kwa moja na majimaji ya mwili wa watu walioambukizwa, nyuso, na vifaa.
Matibabu na changamoto za kinga
WHO inasema hivi sasa hakuna chanjo wala tiba iliyothibitishwa kwa ugonjwa wa Marburg, ingawa majaribio ya kimatibabu yanaendelea.
Huduma za kusaidia wagonjwa, kama vile unyweshaji maji kwa njia ya mdomo au mishipa, pamoja na matibabu ya dalili maalum, zinaweza kuboresha uwezekano wa kupona.
Kulingana na takwimu za WHO Kanda ya Afrika imewahi kushuhudia milipuko na kesi za virusi vya Marburg katika nchi kama Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Ghana, Kenya, Equatorial Guinea, Rwanda, Afrika Kusini, na Uganda.
WHO haipendekezi vikwazo vyovyote vya usafiri na biashara dhidi ya Tanzania kwa wakati huu.