Ukuaji wa uchumi duniani wadorora na kukwamisha soko la ajira - ILO
Ukuaji wa uchumi duniani wadorora na kukwamisha soko la ajira - ILO
Uchumi wa dunia unadorora na hivyo kuzuia soko la ajira kukwamuka kikamilifu, imesema ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la Kazi duniani, ILO iliyotolewa leo huko Geneva, Uswisi.
Ripoti hiyo Hali ya Ajira na Jamii:Mwelekeo wa 2025 inaweka bayana kuwa mwaka 2024 ajira duniani ziliongezeka sambana na nguvu kazi, na hivyo kufanya kiwango cha ukosefu wa ajira kusalia asilimia 5.
Hata hivyo kiwango cha ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana kilipungua kidogo na kusalia asilimia 12.6, umaskini miongoni mwa waajiriwa ulirejea viwango vya kabla ya janga la coronavirus">COVID-19 huku nchi za kipato cha chini zikikumbwa na mazingira magumu zaidi ya kufungua fursa za ajira zenye staha.
Changamoto za kuongeza ajira
Ripoti inaweka bayana sababu za kudorora kuongeza ajira kuwa ni pamoja na mivutano ya kisiasa na kijiografia, ongezeko la gharama kutokana na mabadiliko ya tabianchi na suala la madeni ambalo linaongeza shinikizo kwenye soko la ajira.
Mathalani kiwango cha ukuaji uchumi mwaka 2024 duniani kilikuwa asilimia 3.2 ikiwa ni pungufu kutoka asilimia 3.3 mwaka 2023 na asilimia 3.6 mwaka 2022.
Ijapokuwa mfumuko wa bei umepungua, bado kiwango ni cha juu na hivyo kupunguza thamani ya mshahara, imesema ripoti hiyo.
Ni katika nchi zilizoendelea peke ambako mshahara halisi umeongezeka, lakini nchi nyingi bado zinajikwamua kutoka katika madhara ya janga la COVID-19 na mfumuko wa bei.
Pengo la ajira limefikia milioni 402
Pengo la ajira duniani ambalo ni makadirio ya idadi ya watu wanaotaka ajira lakini hawana ajira – limefikia milioni 402 mwaka 2024.
Hii inajumuisha watu milioni 186 wasio na ajira, milioni 137 ambao kwa sasa hawako tayari kufanya kazi, na milioni 79 wafanyakazi waliokata tamaa na wameacha kutafuta ajira.
Wakati pengo limekuwa likipungua taratibu tangu COVID-19, linatarajiwa kupungua zaidi katika miaka miwili ijayo.
Fursa mpya katika sekta za uchumi wa kijani na kidijitali
Utafiti uliowezesha kupatikana kwa ripoti hiyo umebainisha ukuaji wa sekta za nishati safi na teknolojia ya kidijitali. Ajira katika sekta ya nishati endelevu zimeongezeka hadi milioni 16.2 duniani kote, zikichochewa na uwekezaji kwenye nishati ya sola na ile ya hewa ya haidrojeni, nusu ya ajira hizo ni Asia Mashariki.
Teknolojia za kidijitali zinatoa pia fursa mpya, lakini nchi nyingi hazina miundombinu na stadi za kunufaika na maendeleo hayo, imesema ripoti hiyo.
Majawabu bunifu
Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Gilbert F. Houngbo, amesisitiza umuhimu wa kuchukua hatua.
“Ajira zenye staha na zenye ufanisi ni muhimu ili kuweko kwa haki ya kijamii na vile vile kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs. Ili kuzuia mvutano wa kijamii ambao tayari uko, kupunguza madhara ya tabianchi na madeni yanayoongezeka kila uchao, ni lazima tuchukue hatua sasa kukabili changamoto za soko la ajira ili kujenga mustakabali wa haki na endelevu,” amenukuliwa Bwana Houngbo.
Mambo yanayopendekezwa na ripoti:
- Kuchochea uzalishaji: Kwa kuwekeza kwenye mafunzo ya stadi, elimu na kujenga miundombinu ya kusaidia ukuaji wa uchumi na kufungua fursa za ajira.
- Kupanua hifadhi ya jamii: Kwa kupatia jamii fursa ya kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii na kuweka mazingira salama ya kazi ili kupunguza ukosefu wa usawa
- Kutumia vizuri fedha binafsi: Nchi za kipato cha chini zinaweza kutumia fedha zinazotumwa na wanafamilia kutoka ughaibuni ili kusaidia maendeleo ya jamii.
Soma ripoti nzima hapa.