Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu wa UN akaribisha makubaliano ya kusitisha uhasama na kuachiliwa kwa mateka Gaza

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kushoto) akihutubia wanahabari kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa baada ya kutangazwa kusitishwa kwa mapigano huko Gaza.
UN Photo/Manuel Elías
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kushoto) akihutubia wanahabari kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa baada ya kutangazwa kusitishwa kwa mapigano huko Gaza.

Katibu Mkuu wa UN akaribisha makubaliano ya kusitisha uhasama na kuachiliwa kwa mateka Gaza

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amekaribisha tangazo la makubaliano ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka Gaza, akiyataja makubaliano hayo kuwa ni hatua muhimu kuelekea kupunguza janga la kibinadamu katika eneo hilo.

Katika taarifa aliyoitoa leo mjini New York Marekani Guterres amezipongeza nchi za Misri, Qatar, na Marekani kwa jukumu lao muhimu kama wapatanishi katika kufanikisha makubaliano hayo.
Amesema “Juhudi zao za dhati za kutafuta suluhu ya kidiplomasia zimekuwa muhimu katika kufanikisha mafanikio haya.
Raia wa Gaza walioko Khan Younis wakipokea msaada wa mchele kutoka WFP
© WFP/Jonathan Dumont
Raia wa Gaza walioko Khan Younis wakipokea msaada wa mchele kutoka WFP
Napongeza tangazo la makubaliano ya sitisho la mapigano na kuachilia mateka Gaza. Nasihi pande zote na wadau husika watumie fursa hii kuanzisha mwelekeo sahihi wa kisiasa kwa maslahi ya wapalestina, waisraeli na ukanda mzima. -  António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
 
Katibu Mkuu amesisitiza wito wake wa muda mrefu wa kusitisha mapigano mara moja na kuachiliwa kwa mateka bila masharti yoyote, huku akisisitiza umuhimu wa kutekelezwa kikamilifu kwa makubaliano hayo.
 
Ameongeza kuwa “Kipaumbele chetu ni kupunguza mateso makubwa yanayosababishwa na mgogoro huu,”.
 
Ameahidi kwamba Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia utekelezaji wa makubaliano hayo na kuongeza juhudi za kibinadamu ili kukabiliana na mahitaji makubwa ya watu walioathirika.

Janga la kibinadamu Gaza limefikia pabaya hatua za haraka zahitajika

Hali ya kibinadamu Gaza imefikia viwango vya janga, huku vikwazo vikubwa vya kiusalama na kisiasa vikizuia juhudi za kufikisha misaada.
Katibu Mkuu Guterres alisisitiza umuhimu wa kuondoa vikwazo hivi ili kuwezesha ongezeko kubwa la msaada wa kuokoa maisha kuingia Gaza.
 
“Ninatoa wito kwa pande zote kuwezesha misaada ya kibinadamu kwa haraka, bila vizuizi, na kwa usalama kwa raia wote wanaohitaji,” ameongeza.
 
Ingawa kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka kunachukuliwa kama hatua muhimu ya awali, Guterres amesisitiza umuhimu wa kushughulikia malengo makubwa zaidi ya kisiasa. Amebainisha hitaji la umoja wa Wapalestina na harakati za kufanikisha suluhu ya mataifa mawili kupitia mazungumzo, suluhu ambayo itahakikisha amani na usalama kwa Waisraeli na Wapalestina.
 
Guterres amesema “Kumaliza uvamizi na kufanikisha suluhisho lenye uhai la mataifa mawili, kwa mujibu wa sheria za kimataifa, maazimio husika ya Umoja wa Mataifa, na makubaliano ya awali, bado ni kipaumbele cha dharura,”
Wafanyakazi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) na UNOCHA, walitembelea hospitali ya Al-Aqsa huko Gaza na kuripoti kuona idadi kubwa ya watu waliojeruhiwa wakiletwa kwa matibabu ya haraka, kufuatia mlipuko. (Maktaba)
WHO Video
Wafanyakazi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) na UNOCHA, walitembelea hospitali ya Al-Aqsa huko Gaza na kuripoti kuona idadi kubwa ya watu waliojeruhiwa wakiletwa kwa matibabu ya haraka, kufuatia mlipuko. (Maktaba)

Daima tutawaenzi waliopoteza maisha Gaza

Amehitimisha taarifa yake kwa kuwaenzi kwa heshima raia, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, na wahudumu wa kibinadamu waliopoteza maisha yao katika mzozo huo.
Guterres amethibitisha tena ahadi ya Umoja wa Mataifa ya kuendeleza juhudi za kukuza amani, utulivu, na mustakabali mzuri kwa eneo hilo.
 
Tangazo la makubaliano haya ya amani linakuja wakati kukiwa na miito ya kimataifa inayozidi kuongezeka ya kupunguza mzozo na kutoa misaada ya kibinadamu Gaza.
Jumuiya ya kimataifa sasa inatarajia pande zinazohusika kuheshimu ahadi zao na kufanya kazi kuelekea suluhisho la kudumu la mzozo huu wa muda mrefu.

Kauli za mashirika ya UN baada ya tangazo la usitishaji mapigano Gaza

Baada ya tangazo hilo la usitishwaji uhasama kutolewa mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa yametoa kauli.

UNRWA inasambaza unga katikati mwa eneo la Gaza, na kufikia karibu familia 9,000.
© UNRWA
UNRWA inasambaza unga katikati mwa eneo la Gaza, na kufikia karibu familia 9,000.

Hatari kwa UNRWA yazidi kuongezeka

Shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limesema “Tangazo la kusitisha mapigano linakuja wakati sheria mbili za Israeli zinazolenga kusitisha shughuli za UNRWA katika eneo la Palestina linalokaliwa zinatarajiwa kuanza kutekelezwa katika kipindi cha wiki chache zijazo.”

Shirika hilo limesema Gaza ina idadi ya watu zaidi ya milioni mbili, ambapo milioni 1.9 tayari wamepoteza makazi yao, na mamia kwa maelfu wanapata katika shule zetu zilizogeuzwa kuwa makazi ya muda.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amerejelea kusema mara kadhaa kwamba UNRWA ni “Uti wa mgongo wa juhudi za misaada katika eneo hilo. Shirika hilo limekumbwa na hasara kubwa, huku wafanyakazi wake 265 wakiuawa na miundombinu yake kushambuliwa.”

Kamishna Mkuu wa UNRWA Philippe Lazzarini leo wakati wa mkutano mjini Oslo uliolenga suluhy ya mataifa mawili amesema “Kuanguka kwa shirika hili  iwe ni mara moja au polepole kutazidisha tu mateso makubwa katika Ukanda wa Gaza.”

Wafanyakazi wa OCHA wakati wa ziara yao huko Gaza.
© OCHA
Wafanyakazi wa OCHA wakati wa ziara yao huko Gaza.

Sitisho la mapigano Gaza latoa tumaini japo bado kuna changamoto: OCHA

Taarifa kutoka kwa mratibu mkuu wa misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura wa Umoja wa Mataifa Tom Fletcher, inasema Sitisho la mapigano lililokubaliwa leo kati ya Israel na Hamas linatoa tumaini linalohitajika sana kwa mamilioni ya watu ambao maisha yao yameharibiwa na mzozo huu. Ninalipongeza makubaliano haya na kusihi pande zote kuyaheshimu.

Ameongeza kuwa mashirika ya kibinadamu yameanza kuandaa vifaa vya msaada ili kuongeza utoaji wa misaada huko Gaza, ambako Wapalestina wamepitia zaidi ya miezi 15 ya mateso, uharibifu, na kwa zaidi ya watu 46,000 vifo. Pia, makumi ya mateka wa Kiyahudi bado wanashikiliwa.

Tutafanya kila tuwezalo kukabilina na hali kwa juhudi, ubunifu, na haraka inayohitajika katika wakati huu, licha ya changamoto kubwa za kiusalama na kisiasa zinazotukabili. Amesema

Fletcher amesisitiza kuwa “Ili tuokoe maisha, tunasisitiza pande zote kuheshimu kikamilifu sheria za kimataifa za kibinadamu. Hii inamaanisha kulinda raia na miundombinu ya kiraia, kuruhusu wafanyakazi wa misaada kufika salama na bila vizuizi kwa watu wenye mahitaji, popote walipo, na kuondoa vizuizi vyote kwa upatikanaji wa misaada muhimu.”

Pia ni muhimu kuwezesha kuingia kwa bidhaa za kibiashara amesema akiongeza kwamba  Tunatoa wito kwa Baraza la Usalama kutumia sauti na ushawishi wake kuhakikisha sitisho la mapigano linadumishwa, sheria za kimataifa zinaheshimiwa, na vizuizi vya kuokoa maisha vinaondolewa.

Ameendelea kusema “Tunasihi nchi wanachama kuhakikisha kuwa operesheni zetu za kibinadamu zinafadhiliwa ipasavyo ili kukidhi mahitaji makubwa yaliyo mbele yetu.Tunatoa wito pia wa uwajibikaji kwa ukatili uliofanywa. Huu ni wakati wa tumaini na fursa, lakini tusidanganyike na ugumu wa kazi ya kuwafikia manusura. Hali ni tete, na umuhimu wake hauwezi kupuuzwa.”

Familia iliyokimbia makazi yapokea nguo za msimu wa baridi huko Der Al Balah, katikati mwa Gaza.
© UNICEF/Mohammed Nateel
Familia iliyokimbia makazi yapokea nguo za msimu wa baridi huko Der Al Balah, katikati mwa Gaza.

Sitisho la mapigano ni tumaini kwa watoto na familia: UNICEF

Kwa upande wake shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, inakaribisha sitisho la mapigano katika Ukanda wa Gaza, likisema linaleta matumaini kwa watoto na familia ambao wamepitia zaidi ya mwaka mmoja wa maangamizi.

Mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Catheine Russell amesema Mzozo huu umesababisha vifo vya watoto wasiopungua 14,500, majeruhi kwa maelfu, karibu watu milioni moja kukosa makazi, na watoto 17,000 kuachwa bila mzazi au kutenganishwa na wazazi wao.

Ameongeza kuwa huduma muhimu zimeporomoka, huku chini ya nusu ya hospitali za Gaza zikiwa zinafanya kazi kwa kiasi, uzalishaji wa maji ukiwa katika asilimia 25 pekee, na uhaba mkubwa wa chakula ukiathiri karibu watu wote milioni 2.1.

Watoto na familia zao wakichota maji kutoka kwa tanki la maji linalofadhiliwa na UNICEF huko Deir Al-Balah katika Ukanda wa Gaza.
© UNICEF/Eyad El Baba
Watoto na familia zao wakichota maji kutoka kwa tanki la maji linalofadhiliwa na UNICEF huko Deir Al-Balah katika Ukanda wa Gaza.

Amesisitiza kuwa “UNICEF iko tayari kuongeza juhudi zake, ikizingatia umuhimu wa kuhakikisha upatikanaji wa chakula, huduma za afya, maji safi, elimu, na msaada wa kisaikolojia bila vizuizi. Sitisho hili la mapigano linapaswa kuwezesha operesheni za kibinadamu kuwa salama na juhudi za haraka za kurejesha hali ya kawaida, ikijumuisha matibabu ya utapiamlo, chanjo kwa watoto 420,000 walio chini ya miaka mitano, na kuzuia mlipuko wa magonjwa.”

UNICEF imesisitiza umuhimu wa kuheshimu sitisho hilo la mapigano na imetoa wito wa suluhisho la kisiasa la kudumu ili kuhakikisha maisha bora ya baadaye kwa watoto wa Gaza, ambao tayari wameumia sana.