Mwaka 2024 umevunja rekodi ya kuwa wa joto zaidi la takriban 1.55 ° C juu ya kiwango cha kabla ya maendeleo ya viwanda: WMO
Mwaka 2024 umevunja rekodi ya kuwa wa joto zaidi la takriban 1.55 ° C juu ya kiwango cha kabla ya maendeleo ya viwanda: WMO
• Miaka kumi iliyopita 2015-2024 ndiyo miaka kumi yenye joto zaidi katika rekodi
• Huenda tumeona mwaka wa kwanza wa kalenda ukiwa na wastani wa halijoto ya kimataifa ya zaidi ya nyuzijoto 1.5 ° C juu ya wastani wa 1850-1900
• Seti sita za takwimu za kimataifa zimetumika kuunda takwimu za kimataifa za WMO
• 2024 ilishuhudia halijoto ya kipekee ya ardhini na baharini na joto la bahari
• Lengo la muda mrefu la halijoto la Mkataba wa Paris bado halijafa lakini liko katika hatari kubwa
Shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa Duniani WMO, limethibitisha kuwa mwaka wa 2024 ndio mwaka wenye joto zaidi katika rekodi ya dunia, kulingana na seti sita za takwimu za kimataifa.
Katika ripoti yake iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi WMO imesema “Miaka kumi iliyopita yote imekuwa katika Kumi Bora, kwenye mfululizo wa kipekee wa viwango vya joto vilivyovunja rekodi.”
Wastani wa joto la uso wa dunia ulikuwa nyuzi joto 1.55 °C juu ya wastani wa mwaka kati ya 1850-1900, kulingana na uchambuzi wa pamoja wa WMO wa seti sita za takwimu zilizokusanywa.
Ripoti inasema “Hii inamaanisha kuwa kuna uwezekano tumepitia mwaka wa kwanza wa kalenda na wastani wa halijoto ya kimataifa ya zaidi ya nyuzi joto 1.5°C zaidi ya wastani wa 1850-1900.”
Ongezeko la joto duniani si ndoto: Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antóno Guterres katika taarifa yake kuhusu ripoti hii asema “Tathmini ya leo kutoka kwa Shirika la WMO inathibitisha tena kwamba ongezeko la joto duniani ni ukweli usio na baridi na si ndoto bali ni hali halisi."
Ameongeza kuwa "Kuwa na baadhi ya miaka iliyovuka kikomo cha juzi joto 1.5 haimaanishi lengo la muda mrefu limeshindwa. Ina maana tunahitaji kupambana zaidi ili tuwe kwenye mstari unaotakiwa. Hali ya joto kali kwa mwaka 2024 inahitaji hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi za 2025. Bado kuna wakati wa kuzuia janga mbaya zaidi la mabadiliko ya tabianchi. Lakini viongozi lazima wachukue hatua sasa".
WMO hutoa tathmini ya halijoto kwa kuzingatia vyanzo mbalimbali vya takwimu ili kusaidia ufuatiliaji wa hali ya hewa wa kimataifa na kutoa taarifa zenye mamlaka kwa mchakato wa mazungumzo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi.
Seti hizo za takwimu ni kutoka Kituo cha Ulaya cha Utabiri wa Hali ya Hewa wa Kati (ECMWF), Shirika la Hali ya Hewa la Japani, NASA, Shirika la Kitaifa la masuala ya Bahari la Marekani na Utawala wa masuala ya Anga (NOAA), Ofisi ya Utabiri wa Hali ya Hewa ya Uingereza kwa ushirikiano na Kitengo cha Utafiti wa Hali ya Hewa katika Chuo Kikuu cha Anglia Mashariki (HadCRUT) na Berkeley Earth.
Historia ya mabadiliko ya tabianchi iko mbele ya macho yetu: Celeste Saulo
"Historia ya mabadiliko ya tabianchi inashuhudiwa mbele ya macho yetu. Hatujawa tun a mwaka mmoja au miwili ya kuvunja rekodi ya joto sduniani lakini miaka 10 mfululizo. Hii imeambatana na hali mbaya ya hewa na mabadiliko ya tabianchi, kupanda kwa kina cha bahari na barafu kuyeyuka, vyote vinachochewa na viwango vya kuvunja rekodi vya gesi chafu kutokana na shughuli za kibinadamu,” amesema Katibu Mkuu wa WMO Celeste Saulo.
Ameendelea kusem kuwa “Ni muhimu kusisitiza kwamba mwaka mmoja wa zaidi ya nyuzi joto 1.5°C haimaanishi kuwa tumeshindwa kufikia malengo ya kupunguza joto ya muda mrefu ya Makubaliano ya Paris, ambayo hupimwa kwa miongo kadhaa badala ya mwaka mmoja mmoja. Lakini, ni muhimu kutambua kwamba kila sehemu ya kiwango cha joto ni muhimu. Iwe ni katika kiwango cha chini au zaidi ya nyuzi joto 1.5°C cha ongezeko la joto, kila ongezeko la joto duniani huongeza athari kwa maisha yetu, uchumi na sayari yetu.”
Tathimini ya hali ya joto duniani
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya WMO kuna kiwango cha kutokuwa na uhakika katika tathmini zote za joto. Seti zote sita za takwimu zinauweka 2024 kama mwaka wa joto zaidi kwenye rekodi na zote zinaonyesha kiwango cha hivi karibuni cha ongezeko la joto. Lakini si zote zinaonyesha hali ya joto inayozidi nyuzi joto 1.5 °C kutokana na mbinu tofauti.
Muda wa kutolewa kwa hifadhidata sita za halijoto uliratibiwa katika taasisi zote ili kusisitiza hali ya kipekee iliyoshuhudiwa mwaka wa 2024.
Utafiti tofauti uliochapishwa katika Advances in Atmospheric Sciences uligundua kuwa ongezeko la joto la bahari mwaka 2024 lilichukua jukumu muhimu katika rekodi ya joto la juu. Bahari hiyo ndiyo yenye joto zaidi kuwahi kurekodiwa na binadamu, sio tu juu ya uso bali pia kwa mita 2000 za juu, kulingana na utafiti ulioongozwa na Profesa Lijing Cheng pamoja na Taasisi ya Fizikia ya Anga katika Chuo cha Sayansi cha China na ilihusisha timu ya wanasayansi 54 kutoka nchi saba na taasisi 31.
Takriban asilimia 90 ya joto la ziada kutoka kwenye ongezeko la joto duniani huhifadhiwa baharini, na kufanya maudhui ya joto ya bahari kuwa kiashiria muhimu cha mabadiliko ya tabianchi.
Kuanzia mwaka 2023 hadi 2024, ongezeko la joto la juu la bahari la mita 2000 ni zettajoules 16 (1021 Joules), karibu mara 140 ya jumla ya uzalishaji wa umeme ulimwenguni mwaka 2023, kulingana na utafiti huo, ambao unategemea seti za takwimu za Taasisi ya Fizikiaya Anga.
WMO itatoa maelezo kamili ya viashirio muhimu vya mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na gesi chafuzi, joto la uso wa dunia, joto la bahari, kupanda kwa kina cha bahari, kuteremka kwa barafu na kiwango cha barafu baharini, katika ripoti yake ya Hali ya Hewa Duniani 2024 itakayotolewa Machi 2025 WMO pia itatoa maelezo ya matukio yenye athari kubwa.
Mkataba wa Paris
Bwana Guterres ametoa wito kwa serikali kuwasilisha mipango mipya ya kitaifa ya mabadiliko ya tabianchi mwaka huu ili kupunguza ongezeko la joto la muda mrefu duniani hadi kufikia nyuzi joto 1.5°C, na kuunga mkono mpango ulio hatarini zaidi na athari mbaya za hali ya hewa.
Amesema “Mwaka mmoja au zaidi unaozidi nyuzi joto 1.5°C haimaanishi kuwa tumekosa lengo la kushikilia ongezeko la wastani la joto duniani hadi chini ya nyuzi joto 2°C zaidi ya viwango vya kabla ya kuanza kwa viwanda na kuendeleza juhudi za kupunguza ongezeko la joto hadi nyuzi joto 1.5° C juu ya viwango vya kabla ya viwanda, na kwa kutambua kwamba hii ingepunguza kwa kiasi kikubwa hatari na athari za mabadiliko ya tabianchi kama ilivyoelezwa katika Mkataba wa Paris.”
Amesema hii inarejelea kipindi kirefu, kwa kawaida miongo au zaidi, ingawa Mkataba wenyewe hautoi ufafanuzi mahususi.
WMO inasema kuongezeka kwa joto kwa muda mfupi katika ongezeko la joto la muda mrefu kunaweza kusababishwa na matukio ya kawaida kama El Niño, ambayo yaliendelea kuanzia katikati ya 2023 hadi Mei 2024.
Wakati ongezeko la joto duniani likiendelea, kuna haja ya dharura ya ufuatiliaji na mawasiliano makini kuhusiana na mahali ambapo ongezeko la joto linahusiana na lengo la muda mrefu la joto la Mkataba wa Paris, ili kuwasaidia watunga sera katika mijadala yao.
Timu ya kimataifa ya wataalam iliyoanzishwa na WMO imetoa dalili ya awali kwamba ongezeko la muda mrefu la joto duniani kama ilivyotathminiwa mwaka 2024 kwa sasa ni takriban nyuzi joto 1.3°C ikilinganishwa na msingi wa mwaka kati ya 1850-1900.”