Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lakutana kwa mara ya kwanza mwaka huu kujadili Syria

Watoto wakiwa kwenye makazi ya familia zilizotawanywa Raqqa Syria
© UNICEF/Muhannad Aldhaher Watoto wakiwa kwenye makazi ya familia zilizotawanywa Raqqa Syria

Baraza la Usalama lakutana kwa mara ya kwanza mwaka huu kujadili Syria

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limeutana kwa mara ya kwanza mwaka huu wa 2025 kujadili hali nchini Syria wakati kwingineko Mashariki ya Kati kama Gaza vita vinaendelea huku makumi ya raia wakiripotiwa kuuawa na kujeruhiwa nako Lebanon matumaini yakisalia juu ya kuhamisha Madaraka kwa amani baada ya kuangushwa kwa utawala wa Assadna muafaka wa usitishaji uhasama ukishikilia hivi sasa.

 

Mbali ya masuala ya kibinadamu mkutano wa leo pia utaangalia vikwazo dhdi ya taifa hilo la Mashariki ya Kati.
Geir Pedersen Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu kwa ajili ya Syria akihutubia Baraza la Usalama kwa njia ya video kuhusu hali nchini Syria
UN Photo/Loey Felipe Geir Pedersen Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu kwa ajili ya Syria akihutubia Baraza la Usalama kwa njia ya video kuhusu hali nchini Syria

Syria ina fursa kubwa lakini pia hatari: Pedersen

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Syria Geir Pedersen amekuwa wa kwanza kutoa taarifa kupitia njia ya video.
Amewaambia wajumbe 15 wa Baraza hilo pamoja na wawakilishi wa Misri, Iran, Kuwait, Syria na Uturuki, kwamba kuna "fursa kubwa na hatari halisi huku Syria ikiweka historia mpya kufuatia kuanguka kwa utawala wa zamani mwezi mmoja uliopita.”
Amesema wakati sheria na utaratibu "unaonekana kuwa mzuri katika maeneo mengi ya nchi kumekuwa na taarifa nyingi za matukio ya vurugu hasa katika ukanda wa pwani na maeneo ya Homs na Hama.”
Ameongeza kuwa wakati mzozo unaendelea nchini humo kumesalia "tishio la kweli kwa mamlaka ya Syria, umoja na uadilifu wa nchi hiyo," akibainisha kuwa Umoja wa Mataifa "una wasiwasi mkubwa na uwepo wa kijeshi na shughuli za Israeli."
Ameendelea kusema kuwa kundi la kigaidi la ISIL "linasalia kutia hofu na wasiwasi mkubwa."
Wakati huohuo Pedersenamesema wakati "Mahitaji ya watu wa Syria yakibakia kuwa makubwa, kuna kutokuwa na uhakika kuhusu njia kusonga mbele ya mpito wa kisiasa," akiongeza kuwa Umoja wa Mataifa uko tayari kufanya kazi na mamlaka "kuelekea mpito unaoaminika na jumuishi". 
Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA Tom Fletcher akihutubia Baraza la Usalama kuhusu Syria
UN Photo/Loey Felipe Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA Tom Fletcher akihutubia Baraza la Usalama kuhusu Syria

Changamoto tatu kubwa za kibinadamu:  Mkuu wa OCHA

Mratibu Mkuu wa Misaada ya ibinadamu na masuala ya dharura wa Umoja wa Mataifa Tom Fletcher amesema Umoja wa Mataifa "Lazima uchukue fursa ya wakati huu."

Amesema ziara yake ya hivi karibuni nchini Syria imefichua changamoto tatu kubwa kwa timu za Umoja wa Mataifa na wasaidizi wengine wa kibinadamu nchini humo.

Kwanza, hitaji la kuhifadhi na kujenga upya huduma za nchi hiyo zilizosambaratika baada ya miaka 14 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Takriban Wasyria milioni 15 sasa wanahitaji huduma za afya na karibu milioni 13 wanakabiliwa na "uhaba mkubwa wa chakula" amewaambia wajumbe wa Baraza hilo la Usalama.

Pili, zaidi ya Wasyria 620,000 wamesalia kuwa wakimbizi wakati wa msimu wa baridi kali, wakiwa ni mbali ya milioni saba ambao tayari wameyahama makazi yao, hii ikionyesha hitaji la kutanguliza ulinzi wa raia.

Na tatu, ni muhimu kuhakikisha wanawake na wasichana hawabaguliwi na wale wanaowania mamlaka katika Syria mpya.

Bwana. Fletcher alisema kuwa hali ya usalama imetulia "tumeweza kuanza tena shughuli zetu za kibinadamu kwa kiwango kikubwa."

Msaada wa kwanza wa dharura wa WHO 2025 wawasili Syria ukiwa na tani 32.5 za dawana vifaa vya dharura
© WHO Syria Msaada wa kwanza wa dharura wa WHO 2025 wawasili Syria ukiwa na tani 32.5 za dawana vifaa vya dharura

Fletcher ameomba mambo matatu kwa Baraza la Usalama

Akitoa taarifa kwa Baraza hilo, Mratibu huyo wa misaada ya dharura wa Umoja wa Mataifa Tom Fletcher ameliomba baraza hilo:

1. Msaada na ulinzi kwa mujibu wa sheria za kimataifa

2. Ufadhili wa msaada wa muda mrefu unaohitajika Syria

3. Mtiririko mzuri wa misaada kusaidia ndani na kupitia Syria

Mtoto mwenye umri wa mwezi mmoja akipimwa iwapo ana utapiamlo kwenye kliniki inayoendeshwa na UNICEF nchini Syria
© UNICEF/Marissa Sargi Mtoto mwenye umri wa mwezi mmoja akipimwa iwapo ana utapiamlo kwenye kliniki inayoendeshwa na UNICEF nchini Syria

Jinsi UN inavyoisaidia Syria

Zaidi ya watu milioni moja wameyakimbia makazi yao tangu tarehe 27 Novemba, mwaka jana na kuongeza idadi ya wakimbizi wa ndani kufikia milioni 7.2 nchini Syria.
Wakati huu, mashirika ya Umoja wa Mataifa yamefanya kazi chini kwa chini kutoa msaada kwa wale wanaohitaji zaidi.
• Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP, limekuwa likitoa msaada wa chakula cha kuokoa maisha, likitoa chakula cha moto kwa watu wapya 115,500 waliokimbia makazi yao kote nchini Syria.
• Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF, limekuwa likisaidia masomo kwa watoto kupitia utekelezaji wa vituo vya huduma mbalimbali. Vituo hivi pia hutoa msaada wa kisaikolojia na kijamii.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR linatoa msaada wa dharura kama vile blanketi, mikeka ya kulalia, nguo za majira ya baridi na mahema kwa wakimbizi wa ndani. Shirika hilo pia limerejesha uwepo wake mpakani mwa Syria ili kufuatilia mienendo na kutoa msaada kwa Wasyria ambao wamerejea nchini.
• Zaidi ya watu milioni 2.5 kote nchini Syria ikiwa ni pamoja na wale walio katika kambi, vituo vya pamoja na jumuiya za wenyeji walipokea mikate tangu 27 Novemba 2024 kwa msaada wa OCHA.
• Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM pia linafanya kazi mashinani ili kutoa nyenzo muhimu za msaada na huduma kama vile makazi, chakula na maji.