Sikufahamu ufundi bomba ni nini, sasa ILO imeniwezesha – Msichana Bangladesh
Sikufahamu ufundi bomba ni nini, sasa ILO imeniwezesha – Msichana Bangladesh
Nchini Bangladesh, mradi wa kuimarisha stadi na kufungua fursa za kiuchumi, ISEC miongoni mwa wanawake na vijana, umewezesha wasichana kuvunja mwiko na kuingia kwenye tasnia ambazo zimezoeleka kuwa ni za wanaume, mathalani ufundi bomba. Mradi huo unaolenga wanufaika 24,000 wenye umri kati ya miaka 18 na 35 unatekelezwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Kazi duniani, ILO kwa kushirikiana na serikali ya Bangladesh.
Video ya ILO hapa Cox’s Bazaar inamleta kwako mmoja wa wanufaika hao ambaye hata hivyo jina lake halikutajwa, akiwa ameshikilia vifaa vya ufundi bomba anasema, awali sikufahamu kuhusu hii kozi hadi nilipofahamu kupitia Idara ya Maendeleo ya Vijana. Hii ni mara ya kwanza fursa hii imetufikia katika shule ya sekondari ya juu ya Moheshkhali. Tunajifunza stadi badala ya kupoteza muda nyumbani itanisaidia maisha yangu ya baadaye.
Nikihitimu masomo naungana na kaka kwenye duka lake
Anakiri kuwa kabla ya kushiriki mafunzo haya hakuwa anafahamu kabisa ufundi bomba ni kitu gani. Lakini sasa amejifunza kuhusu vifaa mbalimbali ikiwemo msumeno wa mabomba, spana na kadhalika.
Na ndoto yake ni kwamba nikihitimu masomo nitakwenda kuungana na kaka yangu kwenye duka lake linalounza vifaa vya ujenzi. Nataka niwe mjasiriamali kama yeye, nijitegemee na nisaidie familia yangu. Siku hizi kwenye nyingi zilizoendelea na hata hapa Bangladesh wasichana wanafanya aina zote za kazi.Wanaweza kufanya kazi ngumu kama wanaume, nami nataka kuwa hivyo.
Video ya ILO inamalizika mnufaika huyu amekamilisha kufunga bomba na sasa maji yanatoka, na mkufunzi anatumia maji hayo kunawa mikono.
Malengo namba 4, 5, na 8 ya SDGs yanatekelezwa
Mradi huu ulizinduliwa mwezi Septemba mwaka 2023 ukifadhiliwa na serikali za Canada na Uholanzi kwa lengo la kuendeleza stadi kwa wahusika, kuwa chanzo cha kujipatia kipato na pia kuanzisha biashara na mafunzo kwenye vyuo vya ufundi stadi.
ILO inasema mradi huu unalenga kuchangia kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs, hususan namba 4 la elimu jumuishi na yenye uwiano na kupatia fursa za kujifunza kwa ajili ya kuboresha maisha. Halikadhalika lengo namba 5 la usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake na wasichana.
Lengo lingine ni namba 8 la ukuaji uchumi endelevu, jumuishi kwa kuzingatia ajira fanisi na zenye staha kwa wote.