Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya watu 5,600 wameuawa na magenge ya uhalifu Haiti 2024: OHCHR

Gari lililochomwa imetumika kama kizuizi kwenye barabara huko Port-au-Prince. Kukiwa na zaidi ya magenge 150 yanayofanya kazi ndani na nje ya nchi, barabara zote zinazoingia na kutoka katika mji mkuu wa Haiti sasa ziko chini ya udhibiti wa magenge.
© UNOCHA/Giles Clarke
Gari lililochomwa imetumika kama kizuizi kwenye barabara huko Port-au-Prince. Kukiwa na zaidi ya magenge 150 yanayofanya kazi ndani na nje ya nchi, barabara zote zinazoingia na kutoka katika mji mkuu wa Haiti sasa ziko chini ya udhibiti wa magenge.

Zaidi ya watu 5,600 wameuawa na magenge ya uhalifu Haiti 2024: OHCHR

Haki za binadamu

Kwa mujibu wa takwimu zilizothibitishwa leo na Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR, takriban watu 5,601 waliuawa nchini Haiti mwaka 2024 kutokana na ghasia za magenge ya uhalifu, likiwa ni ongezeko la zaidi ya mauaji 1,000 ya mwaka 2023.

Twakiwmu zinaonyesha kuwa watu wengine 2,212 walijeruhiwa na 1,494 kutekwa nyara.

"Takwimu hizi pekee haziwezi kudhihirisha kikamilifu hali ya kutisha kabisa inayofanywa Haiti lakini zinaonyesha ghasia zisizo na kikomo ambapo watu wanateswa," amesema Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk.

Mauaji ya kutisha

Katika moja ya matukio mabaya zaidi na ya kushtua mwaka jana, takriban watu 207 waliuawa mapema Desemba kwenye mauaji yaliyoratibiwa na kiongozi wa genge lenye nguvu la Wharf Jérémie katika eneo la Cité Soleil huko Port-au-Prince.

Wengi wa waliouawa walikuwa wazee walioshutumiwa kusababisha kifo cha mtoto wa kiongozi huyo kwa njia ya uchawi.

Ili kufuta ushahidi, washiriki wa magenge hayo walikata na kuchoma miili mingi, huku wengine wakitupwa baharini.

OHCHR pia imerekodi visa 315 vya mauaji ya wanachama wa magenge na watu wanaodaiwa kuhusishwa na magenge hayo ya uhalifu, ambayo wakati fulani yaliripotiwa kuwezeshwa na maafisa wa polisi wa Haiti.

Pia zaidi ya hayo, kesi 281 za madai ya kunyongwa kiholela zilizohusisha vitengo maalum vya polisi zilitokea mwaka wa 2024.

Lori la polisi limeegeshwa ndani ya Hospitali Kuu huko Port-au-Prince, Haiti.
© UNOCHA/Giles Clarke
Lori la polisi limeegeshwa ndani ya Hospitali Kuu huko Port-au-Prince, Haiti.

Ukwepaji sheria umeenea

"Imekuwa wazi kwa muda mrefu kwamba ukwepaji sheria kwa ukiukwaji wa haki za binadamu na ukatili, pamoja na rushwa, bado vimeenea nchini Haiti, ikiwa ni pamoja na baadhi ya vichochezi vya changamoto nyingi ambazo nchi inakabiliana nazo, pamoja na kukosekana kwa usawa wa kiuchumi na kijamii." Ameongeza Bwana. Türk.

Ameendelea kusema kuwa "Juhudi za ziada kutoka kwa mamlaka kwa msaada wa jumuiya ya kimataifa, zinahitajika kushughulikia sababu hizi." Mkuu huyo wa haki za binadamu amesisitiza kwamba kurejesha utawala wa sheria lazima iwe kipaumbele.

Ameongeza kuwa kwa lengo hili, Ujumbe wa Kimataifa wa Msaada wa Usalama wa Kimataifa (MSS) unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa nchini Haiti unahitaji msaada wa vifaa na fedha ili kutekeleza kwa ufanisi mamlaka yake.

Zaidi ya hayo, Polisi wa Kitaifa wa Haiti, kwa msaada wa jumuiya ya kimataifa, wanapaswa pia kuimarisha utaratibu wake wa uangalizi wa kuwawajibisha maafisa wa polisi wanaoripotiwa kuhusika katika ukiukaji wa haki za binadamu.

Kutekeleza vikwazo na vikwazo vya silaha

Bwana Türk amerejelea wito wake wa kutekelezwa kikamilifu kwa sheria ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kuiwekea vikwazo Haiti, ikiwa ni pamoja na vikwazo vya silaha, ambavyo ni muhimu katika kuzuia usambazaji wa silaha na risasi kwa nchi hiyo akisema "Silaha zinazoingia Haiti mara nyingi huishia mikononi mwa magenge ya wahalifu, na matokeo ya kusikitisha ni maelfu ya watu kuuawa, mamia ya maelfu ya wakimbizi, miundombinu muhimu na huduma, kama vile shule na hospitali kuvurugika na kuharibiwa." 

Amebainisha zaidi kwamba kufukuzwa kwa Wahaiti kunaendelea ingawa ukosefu wa usalama na kusababisha mgogoro wa haki za binadamu katika nchi yao hairuhusu kurudi kwa usalama na heshima.

Kamishna Mkuu amesisitiza wito wake kwa Mataifa yote kutomrudisha mtu yeyote Haiti kwa lazima.