Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama: Zaidi ya watu milioni 11 ni wakimbizi wa ndani sudan na milioni 8 nje ya nchi na hali inaendelea kuwa tete

Beth Bechdol (kwenye skrini), Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO, akitoa taarifa katika mkutano wa dharura ya Baraza la usalama kuhusu hali nchini Sudan.
UN Photo/Manuel Elías
Beth Bechdol (kwenye skrini), Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO, akitoa taarifa katika mkutano wa dharura ya Baraza la usalama kuhusu hali nchini Sudan.

Baraza la Usalama: Zaidi ya watu milioni 11 ni wakimbizi wa ndani sudan na milioni 8 nje ya nchi na hali inaendelea kuwa tete

Amani na Usalama

Baraza la Usakama la Umoja wa Mataifa leo limesikia kuhusu hali mbaya ya kibinadamu inayoendelea nchini Sudan kuhuku kukiwa na watu milioni 11.5 ambao wamelazimika kuwa wakimbizi wa ndani na milioni 8.5 miongoni mwao wametawanywa tangu Aprili 2023 na watu zaidi ya milioni 3 wamekimbilia nje ya nchi amesema Edem Wosornu mkurugenzi wa kitengo cha utetezi na operesheni katika ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA.

Akitoa taarifa katika Baraza hilo mjini New York Marekani kwa niaba ya Tom Fletcher mkuu wa OCHA ambalo leo linajadili ulinzi wa raia katika mizozo ya silaha likijikita  na suala la uhakika wa chakula Bi. Wosornu amesema “Mwaka huu, mashirika ya kibinadamu yanalenga kusaidia karibu watu milioni 21 ndani ya Sudan, hii ni karibu nusu ya idadi ya watu wa nchi hiyo. Na taarifa hii ya leo inafuatia habari zinazotia wasiwasi kwamba hali ya baa la njaa inaenea.”

Msaada wa chakula unawasilishwa kwa watu waliokimbia makazi yao katika kambi ya Zamzam huko Darfur Kaskazini.
WFP/Mohamed Galal
Msaada wa chakula unawasilishwa kwa watu waliokimbia makazi yao katika kambi ya Zamzam huko Darfur Kaskazini.

Vita Sudan inaendelea kuwa mwiba

Ameongeza kuwa migogoro ya silaha inaendelea kuathiri vibaya raia, wakiwemo wahudumu wa kibinadamu, kote nchini Sudan, licha ya wito wa mara kwa mara wa kusitisha uhasama.

Amesisitiza kuwa “Hali hii ndani na karibu na El Fasher huko Darfur Kaskazini inasalia kuwa janga kubwa.”

Kwa mujibu wa Bi. Worornu mwezi Disemba ulishuhudia kukithiri kwa mapigano hayo, ikiwa ni pamoja na katika kambi ya wakimbizi ya Zamzam, huku raia wakiuawa na kujeruhiwa kwa mizinga na ripoti za wanaotaka kuondoka kambini kuzuiwa kufanya hivyo.

Mapigano pia yameendelea katika maeneo mengine ya nchi, ikiwa ni pamoja na Khartoum, Aj Jazirah, Sennar, Kordofan Kusini na Kordofan Magharibi.

Akitoa mfano wa athari za vita hivyo amesema “tarehe 19 Desemba wakati wa  mkutano wa mwisho wa Baraza wenzetu watatu wa kutoka Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP waliuawa na shambulio la anga kwenye boma lao huko Yabus, katika Jimbo la Blue Nile.”

Ameongeza kuwa changamoto nyingine kubwa ni kufikia maeneo yenye uhitaji mkubwa, ikiwa ni pamoja na maeneo yaliyoathiriwa na njaa.

Edem Wosornu wa OCHA akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu ulinzi wa raia katika migogoro ya silaha nchini Sudan.
UN Photo/Loey Felipe
Edem Wosornu wa OCHA akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu ulinzi wa raia katika migogoro ya silaha nchini Sudan.

Licha ya changamoto kuna matumaini

Bi. Wosornu amesema “Licha ya changamoto zote hizo tumeona baadhi ya hatua chanya katika wiki za hivi karibuni. Tarehe 25 Disemba, msafara wa malori 28 uliwasili Khartoum kutoka Bandari ya Sudan na chakula, vifaa vya lishe na usaidizi mwingine. Huu ulikuwa msafara mkubwa zaidi wa Umoja wa Mataifa kufika mji mkuu tangu mwanzo wa mgogoro, na unafuatia wiki nyingi za mazungumzo. Haya ni maendeleo muhimu, ambayo lazima tuyajenge kwa haraka.”

Pia amesema wiki iliyopita, msafara tofauti wa WFP uliweza kupeleka chakula katika mji wa Abu Jubeiha na maeneo jirani huko Kordofan Kusini. Lakini pia tunashuhudia kubinywa zaidi kwa nafasi ya kufanya kazi katika maeneo muhimu.

Kivuko cha Adre amesema kinasalia kuwa sehemu muhimu ya kuingilia, njia ya kuingia lakini ndani ya Darfur vikwazo vya ziada vinawekwa kwa kazi ya mashirika ya kibinadamu, na taratibu mpya za ukaguzi wa malori yanayokusudiwa kwa maeneo yaliyoathiriwa na migogoro huko Darfur Kaskazini vinaleta vikwazo vipya.

Amesisitiza kuwa “Tunaendelea kushinikiza mamlaka juu ya utekelezaji wa makubaliano yao ya kuanzisha kitovu cha kibinadamu huko Zalingei Darfur ya Kati, kama msingi wa kufanya kazi katika eneo lote.”

Maeneo muhimu katika eneo la Kordofan Kusini yamekatishwa kikamilifu na usaidizi kutoka nje pia Visa kwa wahudumu wa kibinadamu hazitolewi haraka vya kutosha.

Hatari kwa mamilioni kutumbukia katika njaa

Afisa huyo wa OCHA amesema tathimini mpya ya ainisho la awamu jumuishi ya uhakika wa chakula, au IPC imetoa matokeo ya kusikitisha na kushangaza, lakini cha kusikitisha zaidi haishangazi.

Waraka ulioshirikiwa na Baraza Machi mwaka jana uliangazia hatari ya mamilioni ya watu kutumbukia katika janga la uhaba wa chakula.

Huku mapigano yakiongezeka na ufikiaji wa maeneo muhimu yenye njaa ukiwa bado mtihani, kuenea zaidi kwa njaa na baa la njaa kumekuwa kwa kusikitisha na ni hali inayoendelea kusambaa zaidi.

Msaada wa chakula ukikawiwa na WFP Forbaranga Sudan
© WFP
Msaada wa chakula ukikawiwa na WFP Forbaranga Sudan

OCHA inaendelea kuomba mambo matatu kwa Baraza la Usalama

Bi. Wosornu amesema Maswali yetu matatu kwa Baraza la Usalama bado hayajabadilika tangu mwezi uliopita, na tangu waraka uwasilishwe kwa Baraza miezi 10 iliyopita

Mosi, tunahitaji msaada kushinikiza wahusika katika vita kutii sheria za kimataifa za kibinadamu. Hii ni pamoja na wajibu wa kukidhi mahitaji muhimu ya raia, na kulinda bidhaa muhimu, miundombinu na huduma zinazohitajika kwa mifumo ya chakula na uzalishaji wa chakula. Tunatoa wito kwa mara nyingine kusitishwa mara moja kwa uhasama na kwa hatua za kweli na shirikishi kuelekea amani ya kudumu ambayo watu wa Sudan wanaihitaji sana.

Pili ufikiaji ,Tunahitaji ushawishi wa Baraza ili kuhakikisha njia zote kupitia barabara na anga, kwenye mistari ya mbele ya migogoro na mipaka iko wazi kwa vifaa vya misaada na wahudumu wa kibinadamu. Vizuizi vya urasimu lazima viondolewe na vibali na visa kwa wafanyikazi wa kibinadamu wanaoingia vitolewe haraka na kwa ufanisi. Wahudumu wa kibinadamu na mali zao lazima walindwe.

Tatu ufadhili, Kiwango kisicho na kifani cha mahitaji nchini Sudan kinadai uhamasishaji ambao haujawahi kushuhudiwa wa msaada wa kimataifa. Mpango wa Mahitaji na Hatua za Kibinadamu wa Sudan wa 2025 utahitaji dola za Marekani bilioni 4.2 kusaidia karibu watu milioni 21 ambao ni nusu ya wakazi wa Sudan. Dola bilioni 1.8 zaidi zinahitajika kusaidia watu milioni 5 haswa wakimbizi walio katika nchi saba jirani.

FAO: Watu milioni 24.6 hawana uhakika wa chakula

Beth Bechdol, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO, akitoa taarifa katika Baraza hilo ametoa picha ya kusikitisha vile vile akisema "Uchambuzi wa hivi karibuni wa IPC unaonyesha kuwa nusu ya watu waliofanyiwa tathiminiambao ni watu milioni 24.6 wanakabiliwa na viwango vikali vya kutokuwa na uhaba wa chakula. Hii ni watu milioni 3.5 zaidi tangu Juni 2024.”

Raia wengi kote nchini Sudan wanakabiliwa na njaa kali.
Nearly 18 million people across Sudan are facing acute hunger.
Raia wengi kote nchini Sudan wanakabiliwa na njaa kali.

Amebainisha kuwa watu milioni 15.9 wako katika daraja la 3 la IPC la janga la chakula , watu milioni 8.1 katika Daraja la 4 ya hali ya dharura, na zaidi ya watu 637,000 katika Daraja la 5 ambalo ni janga la baa la njaa.

Ameongeza kuwa "Mizozo na watu kufurshwa katika makazi yao vinasalia kuwa vichochezi vya msingi vya janga hili la njaa, ambalo pia linaochochewa na vikwazo vya kibinadamu vya kufikia walio na uhitaji."

Uzalishaji wa kilimo pia umeshuka Bechdol amesema hususan uzalishaji wa mtama, ulezi na ngano ulikabiliwa na punguzo la asilimia 46 kutoka mwaka uliopita.

Kwa msimu ujao wa mavuno, ameonya kuwa njaa na utapiamlo vinazidi kuwa vibaya licha ya kutarajiwa kuwepo kwa chakula.

Sudan ina wasiwasi na tathimini ya IPC

Naye mwakilishi wa kudumu wa Sudan kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Al-Harith Idriss Al-Harith Mohamed ameonyesha wasiwasi wake kuhusu mbinu ya ripoti ya IPC, akisema kuwa uchanganuzi huo uliathiriwa na vikwazo vya ufikiaji wa maeneo yaliyoathiriwa na migogoro.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wa Baraza, balozi huyo amekosoa kutolewa kwa ripoti hiyo akisema imekuwa "haraka na akabainisha kuwa ilitumwa kwa vyombo vya habari kabla ya serikali ya Sudan kupata nafasi ya kujibu matokeo yake.

Alipoulizwa kuhusu utawala unaokuja wa Marekani, amesema, "Rais Trump ni mtengenezaji wa makubaliano. Tutakuwa tayari kufanya naye makubaliano hatutatoka mikono mitupu. Tuna mpango wetu wa kushirikiana na Marekani wakati wote."