Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi dhidi ya sekta ya afya Haiti yanatia hofu kubwa: OHCHR

Watu wanaendelea kufungasha virago Haiti kutokana na magenge ya uhaliffu
© UNICEF/Ralph Tedy Erol
Watu wanaendelea kufungasha virago Haiti kutokana na magenge ya uhaliffu

Mashambulizi dhidi ya sekta ya afya Haiti yanatia hofu kubwa: OHCHR

Amani na Usalama

Mtaalam wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu kuhusu Haiti William O’Neill, leo amesema anatiwa wasiwasi mkubwa kwamba mashambulizi ya kikatili dhidi ya hospitali, zahanati, na wahudumu wa afya yaliyofanywa na magenge ya uhalifu nchini Haiti mwezi wa Desemba yamedhoofisha zaidi mfumo wa huduma za afya ambao tayari ulikuwa karibu kuporomoka.

Amesema Mashambulizi dhidi ya Hospitali ya Bernard Mevs huko Port-au-Prince tarehe 17 Desemba na mauaji ya waandishi wa habari kadhaa na afisa wa Polisi wa kitaifa wa Haiti, waliokuwepo katika majengo ya Hospitali Kuu Desemba 24 kwa ajili ya kufunguliwa tena rasmi, walikuwa wahanga wa mashambulizi ya hivi karibuni zaidi kwa sekta ya afya nchini humo ambayo imekuwa ikilengwa zaidi katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
"Upatikanaji wa huduma za afya na maisha ya wale wanaoitoa yako hatarini sana nchini Haiti," amesema O'Neill, ambaye aliteuliwa na Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu mwezi Aprili 2023.
Wauguzi wakiwa katika wodi ya watoto katika hispitali ya Justinien  Haiti
© UNICEF
Wauguzi wakiwa katika wodi ya watoto katika hispitali ya Justinien Haiti

Ukatili wa magenge ya uhalifu umefurutu ada

O'Neill  amesema “Magenge ya wahalifu yamewaua na kuwateka nyara madaktari, wauguzi na wahudumu wa afya, wakiwemo wahudumu wa kibinadamu. Magenge hayo yamechoma, kupora, na kuharibu hospitali na zahanati nyingi, na kuwalazimu wengi kufunga au kusimamisha shughuli zao za huduma”.
Ameongeza kuwa "Ni asilimia 37 tu ya vituo vya afya katika mji mkuu, Port-au-Prince, vinavyofanya kazi kikamilifu na ni vigumu kwa watu kuvifikia kutokana na masuala ya usalama. Hali hiyo inachangiwa na idadi kubwa ya wahudumu wa afya wanaotoroka nchini wakihofia maisha yao.”
Vitisho vya mara kwa mara vya washiriki wa magenge ya kushambulia majengo ya afya vinaonyesha kuwa haya ni mashambulizi ya makusudi kwenye mfumo wa huduma za afya, na sio vurugu za kiholela, amesema.
Katika baadhi ya matukio, maafisa wa polisi pia walidaiwa kuhusika katika mashambulizi dhidi ya wagonjwa na vitisho dhidi ya wahudumu wa afya.
Mji w Cité Soleil Port-au-Prince ni moja ya miji hatari zaidi kutokanana na magenge ya uhalifu
© UNOCHA/Giles Clarke
Mji w Cité Soleil Port-au-Prince ni moja ya miji hatari zaidi kutokanana na magenge ya uhalifu

Raia wa Haiti wanalipa gharama kubwa ya magenge ya wahalifu

Kwa mujibu wa mtaalam huyo wa haki za binadamu "Watu wa Haiti ikiwa ni pamoja na mamia ya maelfu ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kwa mara nyingine tena wanalipa gharama kubwa ya ghasia hizi huku haki yao ya afya ikizuiliwa vikali".
Aeongeza kuwa "Kuenea kwa magonjwa, kama vile kipindupindu na kifua kikuu, ni chanzo cha ziada cha hofu kubwa."
Mtaalam huyo amesema mashambulizi ya Desemba 24 pia yanasisitiza ukweli kwamba Haiti inasalia kuwa moja ya nchi hatari zaidi kwa waandishi wa habari, Wengi wameuawa huku wengine wakitoroka nchi kutokana na vitisho vya kuuawa.
O’Neill amesisitiza "Ninaiomba jumuiya ya kimataifa kufanya kila iwezalo kusaidia mamlaka ya Haiti kukabiliana na ukosefu wa usalama na kuhakikisha upatikanaji wa haki ya afya, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa vituo vya afya, bidhaa na huduma bila vikwazo. Serikali lazima pia ichunguze na kuwakamata waliohusika na mashambulizi hayo na kuhakikisha kwamba wanafikishwa mahakamani."