Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yasihi usaidizi kwa ajili ya  watu wanaokimbia ghasia za baada ya uchaguzi nchini Msumbiji

Watu ambao wamekimbia kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi nchini Msumbiji wakiwa wanajiandikisha kwa ajili ya usaidizi katika Wilaya ya Nsanje, Malawi.
© UNHCR/Ahmed Bashir Watu ambao wamekimbia kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi nchini Msumbiji wakiwa wanajiandikisha kwa ajili ya usaidizi katika Wilaya ya Nsanje, Malawi.

UNHCR yasihi usaidizi kwa ajili ya  watu wanaokimbia ghasia za baada ya uchaguzi nchini Msumbiji

Msaada wa Kibinadamu

Vurugu hizo zmekuja baada ya mahakama ya juu nchini Msumbiji kuthibitisha tarehe 23 Desemba kwamba chama tawala cha Frelimo kilishinda uchaguzi wa urais uliokumbwa na utata uliofanyika mwezi Oktoba, na hivyo kuzua maandamano.

Nchi hiyo ya kusini mwa Afrika pia bado inaendelea kupata nafuu kutokana na athari mbaya za Kimbunga Chido, ambacho kilipiga wiki chache zilizopita.
 
Hali ya sasa inatatiza juhudi muhimu za kibinadamu kwa jamii zilizopoteza kila kitu katika dhoruba, huku ikitatiza mwitikio wa kuwasaidia.
 
UNHCR na Serikali ya Malawi wametambua takriban watu 2,000 waliovuka mpaka katika wiki iliyopita, huku wengine 1,000 waliingia Eswatini.
 
Miongoni mwa waliowasili ni wakimbizi na waomba hifadhi wa mataifa mbalimbali ambao wamekuwa wakiishi Msumbiji, na UNHCR inaeleza wasiwasi juu ya ongezeko la watu kuhama makazi na athari zake kwa watu walioathirika.
 
Chansa Kapaya, Mkurugenzi wa UNHCR Kanda ya Kusini mwa Afrika, anasema wakimbizi na raia wote wanakabiliwa na hatari kubwa, kupoteza maisha yao na kutegemea msaada wa kibinadamu.
 
"Wakati tunashukuru kwa ukarimu wa Malawi na Eswatini, msaada wa haraka ni muhimu ili kukabiliana na mzozo unaozidi kuwa mbaya na kuzuia mateso zaidi," amesema.
 

Makazi yaliyojaa watu, uhaba wa chakula

 
Watu waliokimbilia Malawi waliripoti kuwa walitoroka mashambulizi na uporaji katika vijiji vyao. Wengi walitembea umbali mrefu na kuvuka Mto Shire kwa miguu au kwa mashua ndogo. Miongoni mwao ni wanawake wajawazito, wazee na watoto ambao wamekuwa na kiasi kidogo tu cha kula.
 
UNHCR imetoa mahema, blanketi na vifaa vya usafi ili kusaidia walio hatarini zaidi, lakini ilibaini kuwa kuna mapungufu makubwa ya usaidizi wa kibinadamu.
 
Makazi yana msongamano wa watu, vifaa vya kujisafi ni haba, na upatikanaji wa chakula na maji safi hautoshi, UNHCR imeeleza. Zaidi ya hayo, zaidi ya watu 1,000 wanashiriki choo kimoja katika baadhi ya maeneo, na hivyo kuongeza kwa kiasi kikubwa hatari ya magonjwa.
 
Huku ikisisitiza dhamira yake ya kufanya kazi na mamlaka za mataifa husika na wadau, UNHCR inahimiza jumuiya ya kimataifa kutoa msaada kwa nchi mwenyeji na watu walioathirika.
 
Tags: Msumbuji, UNHCR Msumbiji, UNHCR