Shambulio la Israel laizima kabisa hospitali ya mwisho kaskazini mwa Gaza: WHO
Shambulio la Israel laizima kabisa hospitali ya mwisho kaskazini mwa Gaza: WHO
Afya
Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa WHO leo limesema shambulio la Israel limeicha taabani hospitali ya mwisho iliyokuwa ikifanyakazi Gaza Kaskazini ya Kamal Adwan.
Takriban Wapalestina 75,000 bado wanaishi katika eneo hilo kitengo cha afya kilikuwa mlengwa wa operesheni hiyo ya Israel iliyosababisha uharibifu wa kitengo cha huduma za msingi kwa ajili ya kuendelea kutoa huduma kwa watu wenye uhitaji na WHO inasema inataka kusaidia wagonjwa ambao wameachwa maskini bila msaada wowote.
Hospitali za Gaza kwa mara nyingine tena zimekuwa uwanja wa vita na mfumo wa afya uko chini ya tishio kubwa ameonya Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus.
Tedros amesema hali inazidi kuwa mbaya kaskazini mwa Gaza, baada ya operesheni ya Israeli kwenye hospitali ya Kamal Adwan, ikifuatiwa na mashambulizi, ambayo yamelemaza kabisa huduma.
Uharibifu, kufurushwa na kuwekwa kizuizini
Kwa mujibu wa WHO “Hiki kilikuwa kituo kikubwa cha mwisho cha afya katika eneo hilo, ambacho bado kina Wapalestina 75,000.”
Wagonjwa na wafanyakazi walilazimika kuhama hospitali na mkurugenzi wa kitengo hicho, Hussam Abu Safiya aliwekwa kizuizini.
Mkuu wa WHO ametoa wito wa kuachiliwa kwake mara moja.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa baadhi ya maeneo ya hospitali hiyo yalichomwa moto na kuharibiwa vibaya ikiwemo maabara, kitengo cha upasuaji, idara ya uhandisi na matengenezo na chumba cha upasuaji.
Wakati huu Hospitali ya Kamal Adwan haitumiki, wagonjwa mahututi wamehamishiwa katika Hospitali ya Indonesia, ambayo haiwezi kumtibu mtu yeyote kwa sababu ya uharibifu.
Wagonjwa walio katika mazingira magumu
Leo Jumatatu, WHO imefanya operesheni katika eneo hilo ili kuwasilisha vifaa vya matibabu na usafi, chakula na maji.
Timu ya shirika hilo, pamoja na washirika wengine wamehamisha wagonjwa 10 mahututi hadi Hospitali ya Al-Shifa.
Wagonjwa wanne walizuiliwa wakati wa uhamisho. Shirika hilo limeitaka Israel kuheshimu mahitaji na haki za wagonjwa.
Wagonjwa wengine saba, pamoja na wahudumu 15 na wahudumu wengine wa afya, wamesalia katika Hospitali ya Indonesia iliyoharibiwa vibaya.
Wito wa kukomesha mashambulizi kwenye hospitali
Hospitali ya Al-Ahli na Hospitali ya Urekebishaji ya Al-Wafa katika Jiji la Gaza pia zimeshambuliwa katika siku za hivi karibuni na zote mbili ziliharibiwa.
Dkt. Tedros ametoa wito wa kukomeshwa kwa mashmbulizi dhidi ya hospitali.
WHO inasema Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, eneo karibu na Hospitali ya Kamal Adwan limekumbwa na mashambulizi karibu kila siku.
Katika wiki iliyopita, makombora katika eneo jirani yamesababisha vifo vya watu 50, wakiwemo wahudumu watano wa afya katika kitengo hicho.
Timu ilijaribu mara 140 kufikia kaskazini mwa Gaza bila mafanikio
Wakati wa ziara yao kaskazini mwa Gaza, kaimu mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na misaada ya dharura OCHA katika Maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu, amesema mapigano yanaendelea katika eneo hilo.
Jonathan Whittall ameeleza kuwa timu za Umoja wa Mataifa zimejaribu kufika kaskazini mwa Gaza mara 140 katika kipindi cha miezi miwili iliyopita na maombi yote yamekataliwa.
Amesisitiza kuwa watu hawana chakula, maji wala vyoo na hawajui la kufanya, wapi pa kwenda au jinsi ya kuishi."
Mwakilishi huyo wa OCHA amesema wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu wanahitaji kuwafikia wale wanaohitaji msaada popote walipo na kwamba ukatili lazima ukomeshwe.