Baraza la Usalama laidhinisha AUSSOM kuchukua jukumu la ATMIS Somalia
Baraza la Usalama laidhinisha AUSSOM kuchukua jukumu la ATMIS Somalia
- AUSSOM kuchukua nafasi ya ATMIS kuanzia Januari 1 hadi Desemba 31 2025
- Inafuatia ombi la Muungano wa Afrika kusongesha ulinzi na usalama Somalia
- Ufadhili wake unatoka Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika
- Marekani haikupiga kura yoyote na imeelezea msimamo wake
Harakati za kukabiliana na ugaidi nchini Somalia zimepatiwa shime mpya hii leo baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio linaloidhinisha pendekezo la Muungano wa Afrika, AU la kuanzisha Ujumbe wa Muungano wa Afrika wa Usaidizi na kuweka Utulivu nchini Somalia, AUSSOM.
Wajumbe 14 walipiga kura za ndio, ilhali hakuna aliyepinga, ambapo Marekani kwa upande wake ilijizuia kuonesha msimamo wowote.
AUSSOM inachukua nafasi ya Ujumbe wa Mpito wa Muungano wa Afrika nchini Somalia, ATMIS ambao mara ya mwisho muda wake uliongezwa tarehe 15 Agosti hadi tarehe 31 mwezi huu wa Desemba.
Azimio hilo namba 2767 (2024), lenye kurasa 13 linapatia mamlaka nchi wanachama wa Muungano wa Afrika kuchukua hatua zote za kipindi cha miezi 12 kuanzia Januari 1, 2025 kuhamishia majukumu ya ATMIS kwenda AUSSOM.
Halikadhalika nchi wanachama kupatia AUSSOM askari 12626 wakiwemo polisi 1,040 na vle vile uoanishaji wa askari wa AU kutoka ATMIS kwenda AUSSOM uwe umekamilika umekamilika ifikapo tarehe 30 mwezi Juni 2025.
Uingereza: Usuli wa Azimio 2767 (2024)
Akizungumza kabla ya kupitishwa kwa azimio hilo namba 2767 (2024) Uingereza ambayo ndio iliandaa rasimu ya azimio hilo ilizungumza kupitia Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa taifa hilo kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi James Kariuki.
Amesema “azimio hili linaimarisha msaada wa Baraza kwa Somalia. Linapatia mamlaka AUSSOM kusaidia Somalia kwenye vita dhidi ya Al-Shabaab, linaimarisha juhudi za Somalia za kuweka utulivu, na pia kuwezesha kufikisha kwa misaada ya kibinadamu.”
Balozi Kariuki ameongeza pia azimio linaweka msingi wa Baraza kuidhinisha mabadiliko ya kimuundo katika ufadhili wa AUSSOM mwezi mei mwaka 2025, ambapo kwa mara ya kwanza utatumika mfumo wa ufadhili uliopitishw ana azimio namba 2719 la mwaka 2023.
Sababu ya Marekani kujizuia kupigia kura azimio
Balozi Dorothy Shea ambaye ni Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa akihutubia Baraza kuelezea sababu ya kura yao ya kutoonesha msimamo wowote wa ndio au hapana ,amesema "tuliunga mkono azimio namba 2719 sio tu kama chanzo cha ufadhili, lakini kama njia ya kuimarisha ubia kati ya Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa. Marekani kuunga mkono azimio 2719 kulifanyika kwa sababu tulisikiliza, tukachukua hatua ya msimamo wa muda mrefu wa wadau wetu wa Afrika."
Azimio namba 2719 lilieleza kwamba operesheni za ulinzi wa amani zinazoongozwa na Muungano wa Afrika, AU na kuidhinishwa na Baraza la Usalama zitapafa fedha kutoka Umoja wa Mataifa na kiwango hicho hakitazidi asilimia 75 ya bajeti yao mwaka, na kiwango kingine kitatolewa na AU.
Balozi Shea amesema kupitia azimio la leo, mchango wa Umoja wa Mataifa utafikia asilimia 90.
Hivyo amesema kwa mtazamo wao, masharti bado hayajakidhi kwa ajili ya mpito wa haraka kuanza kutumia azimio namba 2719 nchini Somalia.
Kauli ya nchi za Afrika ndani ya Baraza la Usalama
Algeria imezungumza kwa niaba ya kundi la nchi 3 + au A3 Plus linalojumuisha nchi tatu za Afrika wajumbe wa Baraza la Usalama la UN, pamoja na nchi moja kutoka Amerika ya Kusini na Karibea. Nchi hizo ni Algeria, Msumbiji, Sierra Leone na Guyana.
Mwakilishi wa Kudumu wa Algeria kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Amar Bendjama amesema “AUSSOM inawakilisha jaribio la kwanza la kwa Jumuiya ya Kimataifa na utayarai wake kusaidia Muungano wa AFrika katika kutatua changamoto zake za kiusalama. Hivyo tumeonesha mfano dhahiri wa kulegeza misimamo wakati wa mashauriano, ili kila upande uweze kufikia matokeo yanayokubalika na sahihi kwa pande zote.”
Balozi Bendjama amesema kuunga mkono azimio hilo linatokana na kuamini kwamba njia zote lazima zitumike kusaidia Somalia kukabiliana na ugaidi kwa kuzingatia nia na matamanio ya Somalia.
Somalia yasema mchango wa asilimia 75 ni jambo jema
Kwa Somalia, kupitishwa kwa Azimio hilo ni kiashiria cha kuanza kutekelezwa kwa azimio namba 2719 la kufanikisha operesheni za ulinzi wa amani Afrika zinazoongozwa na Afrika yenyewe lakini kwa ufadhili wa AU na Umoja wa Mataifa.
Akihutubia Baraza baada ya kupitishwa kwa azimio, Naibu Mwakilishi wa Somalia kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Mohamed Rabi Yusuf, amesema “Kwa kupata ufadhili wa fedha kutoka Umoja wa Mataifa kwa hadi asilimia 75 ni hakikisho la AUSSOM kupata fedha kwa uhakika na kwa uendelevu. Na hii itasaidia uwezo wa kukabili changamoto za usalama zinazoletwa na Al-Shabaab”
Ethiopia yataja mambo ya msingi ili AUSSOM iweze kufanikiwa
Mwakilishi wa Kudumu wa Ethiopia kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Tesfaye Yilma Sabo alialikwa kwenye kikao hicho ambapo amesema, “nasi tuna matarajio makubwa kwa AUSSOM katika kuchangia utulivu wa muda mrefu na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana hadi sasa.”
Hata hivyo amesema “kipindi cha mpito kutoka ATMIS kwenda AUSSOM kitakuwa na mafanikio iwapo tu vikosi vya ulinzi vya Somalia vitawezeshwa kubeba wajibu wao kikamilifu. Makubaliano ya kitaifa ndani ya Somalia na eneo la kikanda lenye msimamo mmoja dhidi ya ugaidi ni mazingira yanayohitajika. Bila mazingira hayo na utayari wa kisiasa na kioperesheni, kuendeleza mafanikio ya kiusalama itakuwa vigumu.”