Dunia yapata Mkataba wa Kimataifa wa dhidi ya Uhalifu wa Kimtandao
Taswira pana ya ukumbi wa Baraza Kuu la UN lilipokutana leo kujadili na kupitisha Mkataba wa Kimataifa dhidi ya Uhalifu wa Kimtandao
Dunia yapata Mkataba wa Kimataifa wa dhidi ya Uhalifu wa Kimtandao
Sheria na Kuzuia Uhalifu
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha Mkataba wa Kimataifa dhidi ya Uhalifu wa kimtandao, (Cybercrime), ikiwa ni hatua ya kihistoria ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kutokomeza uhalifu huo na wakati huo huo kulinda jamii dhidi ya vitisho vya kidijitali.
Kupitishwa kwa mkataba huo siku ya Jumanne Desemba 24, wenye nguvu kisheria, kumetamatisha juhudi za miaka mitano za nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa za zilizoleta pamoja mashirika ya kiraia, wataalamu wa usalama wa taarifa, wanazuoni na sekta binafsi.
Ushirikiano wa kimataifa umeshinda
Kufuatia hatua hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amekaribisha kupitishwa kwa Mkataba huo uliojadiliwa kwa zaidi ya miaka 20.
“Mkataba huu unaonesha jinsi ushirikiano wa kimataifa unaweza kufanikiwa nyakati ngumu na unaashiria utashi wa pamoja wa Nchi Wanachama wa kusongesha ushirikiano wa kimataifa katika kuzuia na kutokomeza uhalifu wa kimtaifa,”’ amesema Katibu Mkuu kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake.
Taarifa imeongeza kuwa, Mkataba “unaanzisha jukwaa la kipekee la ushirikiano,” katika kubadilishana ushahidi, kulinda waathiriwa, kuzuia na wakati huo huo kulinda haki za binadamu mtandaoni.
Katibu Mkuu amesema anaamini kuwa Mkataba huo mpya utasongesha mtandao salama na ametoa wito kwa nchi zote kutia saini na kuridhia Mkataba na hatimaye kuutekeleza kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Mbinu mpya ya kulinda watu
Philémon Yang, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ameangazia umuhimu wa Mkataba huo mpya.
“Tunaishi katika zama za kidijitali, moja ambayo teknolojia za habari na mawasiliano zina umuhimu mkubwa katika maendeleo ya jamii, lakini vile vile zinaongeza tishio kwenye uhalifu wa mtandao,” amesema.
“Kwa kupitishwa kwa Mkataba huu, Nchi Wanachama zina mbinu na njia za kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kuzuia na kutokomeza uhalifu wa kimtandao, kulinda watu na haki za mtandaoni,” amesema Bwana Yang.
Azimio lililokuwa na Mkataba huo limepitishwa bila kura na wanachama wote 193 wa Baraza Kuu.
Ushindi wa ushirikiano wa kimataifa
Ghada Waly, Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuzuia Dawa za Kulevya na Uhalifu, (UNODC) naye ameelezea pia kupitishwa kwa mkataba huo kuwa ni ushindi mkubwa kwa ushirikiano wa kimataifa.
“Ni hatua muhimu kuelekea katika juhudi zetu za kutatua uhalifu wa kimtandaoni kama vile ukatili wa kingono dhidi ya watoto, utapeli wa hali ya juu mtandaoni, na utakatishaji wa fedha,” amesema Bi. Wally.
Amesisitiza kuwa UNODC imejizatiti kusaidia mataifa yote katika kutia saini, kuridhia na kutekeleza
Mkataba huo, pamoja na kuzipatia mbinu na usaidizi wanaohitaji ili kulinda uchumi na jukwaa la kidjitali dhidi ya uhalifu wa kimtandao.
Mkataba una nini?
Mkataba wa Kimataifa dhidi ya Uhalifu wa Mtandaoni unatambua hatari kubwa zitokanazo na matumizi yasiyo sahihi ya teknolojia za habari na mawasiliano, TEHAMA, ambazo zinawezesha shughuli za kihalifu kwa kiwango, kasi na mawanda makubwa.
Unaangazia madhara ambayo yanaweza kusababishwa na uhalifu huo kwa nchi, mashirika na ustawi wa binadamu na jamii, na unajikita kwenye kuwalinda na vitendo kama vile ugaidi, usafirishaji haramu wa binadamu, usafirishaji wa dawa za kulevya na uhalifu wa kifedha mtandaoni.
Halikadhalika unatambua ongezeko la madhara ya uhalifu wa kimtandao kwa waathiriwa na unapatia kipaumbele haki hasa kwa makundi yaliyo hatarini. Unasisitiza pia umuhimu wa msaada wa kiufundi, kujengea watu uwezo na ushirikiano baina ya nchi na wadau.
Soma kwa kina kwa nini Mkataba dhidi ya Uhalifu wa Kimtandao ni muhimu.
Kifuatacho
Mkataba dhidi ya Uhalifu wa Kimtandao utafunguliwa kwa ajili ya kutiwa saini kwenye hafla maalum itakayofanyika huko Hanoi, Viet Nam, mwaka 2025. Utaanza kutekelezwa siku 90 baada ya kuridhiwa na nchi ya 40.