TANBAT 7 warejea Tanzania wakiwa na barua ya pongezi ya kazi nzuri kutoka UN
TANBAT 7 warejea Tanzania wakiwa na barua ya pongezi ya kazi nzuri kutoka UN
Kikosi cha 7 cha Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania, TANBAT 7 kilichokuwa kinahudumu katika Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kuleta Utulivu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR (MINUSCA kimefanikiwa kurejea nchini Tanzania kikiwa salama na kikijivunia kuwa kikosi cha kwanza cha nchi hiyo kupata barua ya pongezi ya Umoja wa Mataifa.
Brigedia Jenerali George Mwita Itang’are ambaye ni Mkuu wa Kituo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani cha Tanzania, akiwapokea askari jijini Dar es Salaam katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Mapinga akiambatana na ujumbe kutoka Makao Makuu ya Jeshi kwa niaba ya Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Luteni Jeneral Haji Othman amesema kikosi hiki kimepata barua ya pongezi kutoka Umoja wa Mataifa kutokana na kutimiza majukumu yao vizuri na kwa nidhamu na sasa jeshi la Tanzania, JWTZ lina imani kwamba askari hawa wanaporejea katika majukumu yao ya kitaifa watayatekeleza vizuri kutokana na uzoefu walioupata.
Akitoa Salamu kwa niaba ya Mnadhimu Mkuu wa JWTZ Brigedia Jeneral George Itang'are amesema "Karibuni nyumbani na asanteni kwa kutuwakilisha vyema kama Jeshi na nchi kwa ujumla pamoja, mliweza kutekeleza jukumu hili vyema ninatambua ushiriki wenu katika jukumu hili mmeweza kupata uzoefu na hili linatokana na mambo matatu ambayo ni nguzo za mwanajeshi utiifu uaminifu na uhodari na kuishi katika viapo vyetu . Ni matumaini yangu mtaendelea kutekeleza majukumu ya kijeshi hapa nchini."
Aidha Kamanda Kikosi hicho kilichomaliza jukumu lake, Luteni Kanali Joseph Mushilu amekabidhi cheti ambacho Kikosi kilitunukiwa na Umoja wa Mataifa kutambua mchango wa Kikosi hicho katika kuwalinda Raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.