Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya watu 207 wameuawa Port-au_Prince nchini Haiti - UN

Taswira kutoka angani ya mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince ikionesha pia makazi ya wakimbizi wa ndani.
© IOM/Antoine Lemonnier
Taswira kutoka angani ya mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince ikionesha pia makazi ya wakimbizi wa ndani.

Zaidi ya watu 207 wameuawa Port-au_Prince nchini Haiti - UN

Amani na Usalama
  • Wameuawa na genge la  uhalifu la Wharf Jérémie kati ya tarehe 6 hadi 11 Desemba 2024
  • Wanaume ni 134 na wanawake ni 73
  • Wengi wao ni wazee na wanatuhumiwa 'kumloga' na kumsababishia ugonjwa mtoto wa kiongozi wa genge hilo.

Ikiwa ni chini ya wiki mbili tangu kuongezeka kwa ghasia kwenye kitongoji cha Cité Soleil cha mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince, ripoti ya Umoja wa Mataifa imethibitisha vifo vya zaidi ya watu 207 waliouawa na genge la uhalifu la Wharf Jérémie.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Port-au-Prince na Ofisi ya Umoja Jumuishi ya Umoja wa Mataifa nchini Haiti, (BINUH) na Ofisi ya Kamishna wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, (OHCHR) mauaji hayo yamefanyika kati ya tarehe 6 hadi 11 mwezi huu wa Desemba ambapo waliouawa ni wanaume 134 na wanawake 73.

Idadi kubwa ya waliouawa ni wazee ambao watu wanawatuhumu kuhusika na vitendo vya uchawi na kusababisha kuugua kwa mtoto wa kiongozi wa genge hilo la uhalifu, imesema ripoti hiyo.

Wengine waliuawa wakijaribu kukimbia kutoka kitongoji hicho cha Cité Soleil kwa hofu ya kukumbwa na visasi au kwa kushukiwa kupatia vyombo vya habari tarifa kuhusu uhalifu unaoendelea kwenye eneo lao.

Waliuawa kwa risasi au kwa mapanga

Watu hao waliouawa walifuatiliwa na kwenye makazi yao au nyumba za ibada na kisha kupelekwa kwenye ngome ya genge hilo ambako walishikiliwa mateka, wakahojiwa ndani kile kinachoitwa, “kituo cha mafunzo.”

Kisha walipelekwa eneo jirani la mauaji na kupitwa risasi au kukatwa na mapanga. Genge hilo lilijaribu kufuta ushahidi wote kwa kutia moto miili yao au kuikata vipande vipande na kuitupa karibu na bahari.

Hatuweze kuendelea na shughuli kama vile hakuna kilichotokea,” amesema María Isabel Salvador, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Haiti, na pia mkuu wa BINUH.

“Natoa wito kwa mfumo wa haki Haiti kufanya uchunguz iwa kina wa uhalifu huu wa kikatili na kuadhibu wahusika, na wale wanaowaunga mkono.”

Bi. Salvador ametoa wito pia kwa mamlaka Haiti kuunda mara moja kitengo mahsusi cha mahakama kushughulikia uhalifu wa aina hiyo.

Kituo cha shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM cha mgao wa misaada mjini Port-au-Prince
© IOM/Antoine Lemonnier
Kituo cha shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM cha mgao wa misaada mjini Port-au-Prince

Kiwango cha juu cha ukatili

Tangu mwaka 2022, genge la uhalifu la Wharf Jérémie nchini Haiti limekuwa likikabiliana na magenge pinzani katika kudhibi barabara zinazoelekea bandari kuu ya Port-au-Prince na kituo cha kuhifadhi kontena.

Mwaka huu pekee, BINUH ba OHCHR wamesajili mauaji ya zaidi ya watu 5,350 na zaidi ya 2,155 wamejeruhiwa kutokana ghasia hizo.

Halikadhalika, kiongozi wa genge la uhalifu la Wharf Jérémie  ameweka “kodi” kwa kampuni inayoendesha bandari hiyo, hasa kwa kontena zinazoruhusiwa, pamoja na kampuni za malori zinazosafirisha bidhaa kutoka bandari hiyo.

Halidhalika amejiweka yeye kama dalali wa watendaji wa kitaifa na kimataifa wanaosaka kufikia wananchi wanaoishi Wharf Jérémie.

MAtukio haya ya uhalifu yanatokea katika kasi ya kutisha yakihusisha magenge ya uhalifu, vikundi vinavyojihami na wananchi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, vyanzo vya uhakika vinadokeza pia kuhusika kwa vitengo maalum vya Polisi wa kitaifa Haiti.