Mradi wa umwagiliaji warejesha matumaini kwa wakulima wa Masvingo, Zimbabwe
Mradi wa umwagiliaji warejesha matumaini kwa wakulima wa Masvingo, Zimbabwe
Hivi karibuni mkutano wa Umoja wa Mataifa wa kuzuia kuzuia kuenea kwa jangwa, ulikunja jamvi huko Riyadh, Saudi Arabia ambapo Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Kilimo, IFAD ulitumia fursa hiyo kuelezea harakati zake za kusaidia wakulima barani Afrika walioathiriwa vibaya na kuenea kwa jangwa. Miongoni mwa mataifa hayo ni Zimbabwe ambako IFAD imeshaanza kuchukua hatua na kuleta nuru kwa wakulima.
Taswira ya matumaini kwenye shamba la mahindi yakiwa yamestawi, wakulima wakivuna wakiwa na tabasamu. Ni kupitia video ya Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Kilimo IFAD.
Hapa ni jimbo la Masvingo kusini -magharibi mwa Zimbabwe, taifa la kusini mwa Afrika ambalo mwaka huu limekumbwa na ukame hadi Rais Emmerson Mnangagwa kutangaza
Taswira ya awali kwenye video hii inaonesha ukame mkali, mabomba yasiyo na maji na ziwa lililokauka.
Ukame wa hivi karibuni Mashariki na kaskazini mwa Afrika ulikuwa mbaya zaidi kuwahi kukumba maeneo hayo kwa kipindi cha miaka 40.
Katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita, Ukanda wa Sahel ambao uko kaskazini mwa jangwa la Sahara, sasa umehamia kilometa 200 kuelekea kusini.
Monugwei Mateza, mkulima huyu anasema "kama uonavyo mvua ni kidogo. Imetangazwa kwamba itanyesha lakini bado hakuna. Hivyo tunatarajia mvua karibuni.
Mateza ni miongoni mwa asilimia 40 ya wakulima Zimbabwe waliokosa kabisa mavuno ya mazao mwaka huu kutokana na mkondo joto El Nino uliosababisha ukame mbaya zaidi kwenye historia yao.
IFAD kwa kubaini changamoto ya wakulima kama Mateza, kwa kushirikia na serikali walianzisha mradi wa umwagiliaji kwa wakulima wadogo, SIRP. Mradi unaotekelezwa katika majimbo ya Manicaland, Matabeleland Kusini, Midlands na Masvingo ukilenga kunufaisha kaya maskini 27,700.
Eka 6,100 zilizoko katika mifumo ya sasa 152 ya umwagiliaji inayosimamiwa na wakulima wadogo itafikiwa. Wakulima wataweza kumwagilia mazao yao wakati wa ukame na hivyo kuweza kulima mazao tofauti tofauti
Mradi wa SIRP umeleta mabadiliko makubwa. Mahindi yamemea vizuri hapa Masvingo, kwa sababu ya umwagiliaji.
Mkulima Dzanisai Makhozo akiwa nyumbani na mumewe Tobias Makhozo, anakumbuka hali kabla ya mradi huo.
"Kabla ya SIRP kulikuweko na mifereji ambayo tuliitumia kwenye mfumo wa umwagiliaji kutoka bwawani. Mifereji ilikuwa inavuja kwa hiyo bwawa lilikauka maji haraka. Lakini mradi wa SIRP ulipokuja mabomba yaliyowekwa yalibadili maisha yetu.”
Mahindi sasa yamekomaa na wakulima wanavuna na kuyajaza kwenye gari tayari kufikia walaji.
Rais wa IFAD Alvaro Lario akizungumzia umuhimu wa kusaidia wakulima wadogo kama wa huko Masvingo, Zimbabwe anasema.
"Wakulima wadogo milioni 500 duniani ni uti wa mgongo wa mifumo yetu ya chakula duniani kote. Wao ndio wanabeba mzigo wa madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Wao ndio wako hatarini zaidi nao ni wa mwisho kwa wawekezaji kufikiria kuwekeza kwao. Kuwekeza kwa wakulima hawa ni jambo la lazima iwapo tunataka kuhakikisha upatikanaji wa chakula.”