Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusipomakinika, Akili Mnemba (AI) itaiacha dunia na ‘upofu’ - Guterres

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana kujadili athari za Akili Mnemba kwa amani na usalama wa kimataifa.
© Unsplash/Igor Omilaev
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana kujadili athari za Akili Mnemba kwa amani na usalama wa kimataifa.

Tusipomakinika, Akili Mnemba (AI) itaiacha dunia na ‘upofu’ - Guterres

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mapinduzi makubwa yanayoletwa na Akili Mnemba (AI) duniani hivi sasa yamesababisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kusema kuwa bila usimamizi wa binadamu, Akili Mnemba inaweza kuiacha dunia na upofu.

Amesema hayo akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililokutana kumulika athari za Akili Mnemba kwenye amani na usalama duniani wakati huu ambapo teknolojia hiyo inatumia kwenye tasnia mbalimbali ikiwemo kijeshi, kiuchumi, kiulinzi, kiafya na kijamii.

Mkutano huo umeitishwa na Marekani na Guterres amesema Akili Mnemba sio tu inaumba upya dunia bali inaleta mapinduzi ya dunia.

Kilichohitaji miaka kadhaa kukamilika sasa ni sekunde tu

Kazi ambazo zamani zilihitaji miaka kadhaa ya utaalamu wa binadamu, sasa zinafanyika kwa pigo moja tu la moyo. Hata hivyo madhara yake nayo ni makubwa mno.

Katibu Mkuu amesema kasi kubwa ya ukuaji wa AI inazidi uwezo wa kuisimamia na hivyo kuibua maswali lukuki kuhusu uwajibikaji, usawa, usalama na ulinzi.

Ingawa tayari AI imeleta mabadiliko chanya kama kwenye kubaini kulikotegwa mabomu ya ardhini, maeneo yenye uhaba wa chakula na punde inaweza kubaini vurugu kabla ya kuibuka, teknolojia hiyo inaweza kuleta vurugu kwenye diplomasia.

Maudhui bandia yatengenezwayo na Akili Mnemba ni tishio

“AI inatengeneza maudhui ya uhalisia ambayo yanasambaa kwa kasi kubwa kwenye mitandao ya kijamii na kubadili maoni au mtazamo wa jamii kuhusu suala fulani, inatishia maadili ya taarifa na kufanya ukweli kushindwa kutofautishwa na uongo,” amesema Guterres.

Tweet URL

Amesema taarifa za uongo zinaweza kuchochea majanga ya kidiplomasia, vurugu na kuvuruga misingi ya jamii.

Amekumbusha kuwa maazimio yamepitishwa na nchi wanachama, makundi ya kikanda, mashirika ya kimataifa na  hata Umoja wa Mataifa ili AI iweze kuwa ya manufaa kwa nchi zote.

Mathalani Mkataba wa Kimataifa wa Kidijitali uliopitishwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa mwezi Septemba mwaka huu wa 2024 jijini New York, Marekani.

Mkataba huo unataka pamoja na mambo mengine ufadhili bunifu wa kupeleka AI kule inakohitajika zaidi – kuhakikisha nchi zinazoendelea zinapata usaidizi kamilifu.

Mapendekezo ya Guterres

Na ndipo akapendekeza kuundwa mwa mfumo wa kimataifa wa kuendeleza Akili Mnemba kwa uwiano na usawa, ukijikita kusaidia nchi zinazoendelea kuzuia kuibuka kwa pengo la teknolojia hiyo kati ya walio nayo na wasio nayo.

“Ninasihi nchi wanachama ziongeze kasi kuanzisha Jopo la Kimataifa la Kisayansi kuhusu Akili Mnemba na wazinduie Mashauriano ya Kimataifa kuhusu usimamizi wa AI ndani ya Umoja wa Mataifa,” amesema Guterres.

Halikadhalika kupiga marufuku silaha za sumu zinazojifyatua zenyewe na kwamba  hakuna nchi yoyote itakayobuni, kutengenenza au kupeleka silaha za kijeshi za mfumo wa AI iliyo kinyume na sheria za kimataifa za haki za binadamu na ubinadamu.

Mifumo ya sasa ya AI haina uwezo wa kutafakari kama binadamu 

Baada ya hotuba  ya Katibu Mkuu, wajumbe wa baraza walitoa maoni yao,  halikadhalika wageni maalum wakiwemo wabobezi wa masuala ya Akili Mnemba.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony J. Blinken, ambaye ndiye aliongoza kikao hicho kwa kuwa nchi  yake inashikilia Urais kwa mwezi huu wa Desemba, amesema kwa maendeleo yote yaliyopatikana kwenye AI, bado kuna kazi kubwa ya kufanya. Mataifa yaliyoko mbele kiteknolojia lazima yachukue hatua zaidi kuzingatia viwango vya usalama ili kuepusha matumizi mabaya ya AI au Akili Mnemba.

Yann LeCun, Mwanasayansi Mkuu wa Akili Mnemba kutoka Meta na pia Chuo Kikuu cha New York nchini Marekani amefafanua kuhusu uelewa wa mifumo ya Akili Mnemba akisema “mifumo ya sasa ya Akili Mnemba haina uelewa wa dunia halisia, haina kumbukumbu ya moja kwa moja, na haiwezi kutafakari mambo au kupanga. Haiwezi kusoma stadi mpya kwa kasi na ufanisi wa binadamu au Wanyama.”

Muongo mmoja au miwili ijayo, AI itakuwa na uwezo wa kutafakari

Yann LeCun, Mwanasayansi Mkuu Meta na Jacob T. Schwartz na Professa wa Sayansi ya Kompyuta na Data, na Uhandisi wa Umeme na Kompyuta katika Chuo Kikuu cha New York, Marekani akihutubia Baraza la Usalama lililokutana kuhusu uendelezaji wa amani na usalama…
UN Photo/Loey Felipe
Yann LeCun, Mwanasayansi Mkuu Meta na Jacob T. Schwartz na Professa wa Sayansi ya Kompyuta na Data, na Uhandisi wa Umeme na Kompyuta katika Chuo Kikuu cha New York, Marekani akihutubia Baraza la Usalama lililokutana kuhusu uendelezaji wa amani na usalama hususan Akili Mnemba

Hata hivyo amesema hakuna mjadala kwamba katika siku zijazo, mifumo ya AI itaweza kuwa na uwezo na hata kuzidi uwezo wa kiakili wa binadamu.

“Lakini itakuwa ni mifumo tofauti na mifumo ya sasa ya Akili Mnemba (AI). Watakuwa na uwezo wa kuelewa muonekano wa dunia, kukumbuka, kutafakari na kupanga. Wanawezakuwa na kiasi fulani cha utambuzi wa mambo. Hii haitafanyika kesho, pengine muongo mmoja au miwili ijayo,” amefafanua LeCun.

AI isinufaishe mataifa tajiri peke yake - Profesa Li

Kwa upande wake Fei-Fei Li, kutoka Kampuni ya Sequoia, na pia mjumbe wa Bodi ya Ushauri wa Kisayansi iliyoundwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema manufaa ya AI hayapaswi kuwa kwa ajili ya mataifa tajiri peke yake.

Badala yake, Profesa huyo wa Chuo Kikuu cha Stanford amesema “ni wajibu wetu wa pamoja  kuhakikisha kila mtu ana uwiano sawa wa kufikia mbinu za AI, mafunzo na miundombinu. Hili si suala la usawa – ni suala la utulivu wa dunia.”