Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Karla Quintana wa Mexico kuongoza Tume ya kuchunguza waliotoweshwa Syria

Mwanamke Karla Quintana akizungumza kwenye jukwaa akiwa na bendera ya Mexico nyuma yake.
© Karla Quintana Karla Quintana mwanaharakati wa haki za binadamu na mbobezi wa sheria kutoka Mexico ameteuliwa kuongoza Tume Huru ya kuchunguza watu waliotoweshwa nchini Syria.

Karla Quintana wa Mexico kuongoza Tume ya kuchunguza waliotoweshwa Syria

Amani na Usalama

Karla Quintana mwanaharakati wa haki za binadamu na mbobezi wa sheria kutoka Mexico ameteuliwa na Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa António Guterres hii leo kuongoza Tume Huru ya kuchunguza watu waliotoweshwa nchini Syria, Tume ambayo imeundwa na Baraza la Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Juni mwaka jana 2023.

Guterres amewaambia waandishi wa habari hii leo kwamba yeye na timu yake lazima waruhusiwe kutekeleza kwa kina jukumu lao, na vile vile mifumo yote ya kimataifa ya kusongesha ulinzi wa haki za binadamu nchini Syria na uwajibikaji wa uhalifu uliotendwa lazima wawe na wanachohitaji ili kutekeleza majukumu yao muhimu.

Katibu Mkuu UN António Guterres akizungumza kwenye jukwaa wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
UN Photo/Eskinder Debebe Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia waandishi wa habari kuhusu hali nchini Syria.

Katibu Mkuu amesema  ingawa kinachomulikwa hivi sasa ni kusaka fedha kwa ajili ya usaidizi wa kibinadamu, kutambua mustakabali wa watu waliotoweshwa ni muhimu pia na hivyo ameahidi mshikamano na wale wote ambao wanaendelea kuishi kwenye machungu ya sintofahamu kuhusu wapendwa wao.

Kwa mujibu wa azimio namba 77/301 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, makao makuu ya Tume hiyo yatakuwa Geneva, Uswisi kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa.

Bado kuna changamoto ya usalama Syria

Guterres ametumia pia hotuba yake kuzungumzia hali ya usalama Syria akisema kuwa ingawa kuna utulivu nchini humo, bado vita haijaisha kwani raia bado wako hatarini, wanauawa, wanajeruhiwa na wanafurushwa makwao, hasa eneo la kaskazini.

“ISIL imeendelea kuwa tishio kubwa kwenye maeneo mengi. Na wakati huo huo, mashambulizi kutoka angani yanayofanywa na Israeli yanaendelea. Vitendo hivi ni ukiukaji wa uhuru na kujitawala kwa Syria. Hii lazima ikome,” amesema Katibu Mkuu.

Jeshi lolote lisiweko eneo tenganishi huko Golani zaidi ya walinda amani wa UN

Amegusia eneo la milima ya Golan upande wa Syria ambalo linakaliwa na Israeli akisema ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani kwenye eneo hilo, UNDOF, unaendelea kuangalia uwepo wa vikosi vya Israeli na wanajeshi wake kwenye maeneo kadhaa ya eneo linalotenga nchi hizo na eneo la ukomo.

Familia zilizopoteza makazi, wakiwemo wanawake na watoto, zimepumzika kwenye blanketi chini katika kituo cha mapokezi cha nje huko Ar-Raqqa, Syria.
© UNICEF/Muhannad Aldhaher Familia inakusanyika katika kituo cha mapokezi katika mji wa Ar-Raqqa, Syria.

“Hebu nieleze bayana: Hakupaswi kuweko kwa jeshi kwenye eneo tenganishi zaidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa. Israeli na Syria lazima wazingatie Makubaliano ya mwaka 1974 kuhusu kuondoa majeshi, makubaliano ambayo bado yanatambuliwa,” amesema Katibu Mkuu.

Mfahamu Karla Quintana

Bi. Quintana ni mtaalamu wa masuala ya haki za binadamu na mwanazuoni wa masuala ya sheria akiwa na uzoefu mkubwa kwenye sheria ya kimataifa ya haki za binadamu, utatuzi wa ukiukwaji wa haki za binadamu na sheria ya katiba.

Alikuwa Kamishna wa Kitaifa wa Tume ya kusaka watu waliotoweshwa nchini Mexico ambapo aliongoza juhudi za kutatua kesi 100,000 za watu waliopotea na zaidi ya miili 70,000 ya watu ambao hawakufahamika.

Wakati wa kipindi chake, alianzisha Masjarala ya Kitaifa ya Watu waliotoweka, na aliongoza hatua za msingi kama vile uchunguzi wa kimazingira.

Kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa wa sasa, Bi. Quintana alikuwa Mkuu wa  Jopo la Utetezi Mexico ambako aliongoza hatua za kuimarisha upataji wa haki, usaidizi wa kisaikolojia na fidia kwa waathiriwa wa uhalifu na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Ajira yake ya mwanzoni ni karani wa sheria kwenye  Mahakama Kuu ya Mexico.