Kimbunga Chido kikiacha uharibifu mkubwa Msumbiji, UN yashikamana na waathirika
Kimbunga Chido kikiacha uharibifu mkubwa Msumbiji, UN yashikamana na waathirika
Mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa leo yamesema kimbunga Chido ambacho kimeambatana na mvua kubwa na upepo mkali kimesababisha madhara makubwa, ikiwemo uharibifu wa miundombinu na kutawanya maelfu ya watu nchini Msumbiji ambako sasa watu zaidi ya 190,000 wanahitaji msaada wa haraka wa kuokoa maisha.
Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF takribani watoto 90,000 wameathirika na kimbunga hicho kilichosambaratisha nyumba zaidi ya 35,000 katika jimbo la Cabo Delgado Kaskazini mwa Msumbiji jimbo ambalo limeghubikwa na machafuko baada ya kimbunga hiccho kuwasili Jumapili.
Sasa UNICEF inahofia kusambaa kwa magonjwa yanayosababishwa na maji na pia kutawanywa kwa wimbi kubwa la watu.
Mbali ya kusambaratisha nyumba kimbunga hicho pia kimeharibu madarasa 186 na vituo vya afya 20.
Msumbiji ni muathirika mkubwa wa mabadiliko ya tabianchi
Mwakilishi wa UNICEF nchini Msumbiji Mary Louise Eagleton amesema “Msumbihi inachukuliwa kuwa ni moja ya nchi mwathirika mkubwa wa mabadiliko ya tabianchi duniani na watoto walikuwa tayari wanakabiliwa na dharura nyingi zinazotishia maisha yao hata kabla ya kimbunga Chido ikiwemo machafuko, ukame na magonjwa ya milipuko.”
Ameongeza kuwa “UNICEF pamoja na serikali, mashirika dada ya Umoja wa Mataifa, mashirika yasiyo ya kiserikali na washirika wqengine wanachukua hatua kukabiliana na athari za kimbunga hicho kwa kutoa kipaumbele katika masuala ya dharura ya kibinadamu licha ya changamoto lukuki zinazowakabili watoto nchini Msumbiji.”
Kimbunga Chido kilipiga karibu na mji wa Pemba jimboni Cabo Delgado, na kuezua mapa ya nyumba, kuharibu miundombinu ya kiraia na kuathiri mfumo wa umeme na mawasiliano.
Shirika hilo la watoto linasema jimbo la Cabo Delgado limeathirika na karibu miaka saba ya machafuko mabaya yaliyosababisha takriban watu miliobi 1.3 kuwa wakimbizi wa ndani, huku asilimia 80 miongoni mwao wakiwa ni wanawake na watoto.
Maelfu ya watu wametawanywa na kimbunga Chido: UNHCR
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema athari za kimbunga hicho kwa watu ni kubwa sana na maelfu wamelazimika kukimbia kwenda kusaka mahala salama, na kutokana na kubomoka kwa miundombinu kama barabara na mfumo wa mawasiliano kumeathiri juhudi za utoaji misaada ya kibinadamu inayohitajika sana katika maeneo kama Cabo Delgado na Nampula ambayo tayari yalikuwa yanahifadhi idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani.
Hivi sasa UNHCR inasema ina wasiwasi mkubwa kuhusu athari kwa jamii hizi zilizo katika mazingira magumu na shirika hilo linafanya kazi kwa karibu na Serikali ya Msumbiji na washirika wa kibinadamu kutoa msaada wa haraka.
Ndani ya saa 48 za kwanza, UNHCR ilitoa msaada katika kituo kikubwa zaidi cha malazi kisiwani Pemba, mji mkuu wa Cabo Delgado, ambapo zaidi ya watu 2,600 walipata msaada wa dharura na vifaa muhimu kama vile mablanketi, mikeka ya kulalia, vyandarua na vifaa vya dharura.
UNHCR pia inaratibu utoaji wa huduma muhimu za ulinzi kwa walio hatarini zaidi.
Idadi ya wanaohitaji msaada
Ingawa kiwango kamili cha uharibifu katika maeneo ya vijijini bado hakijafahamika, tathmini za awali za UNHCR zinaonyesha kuwa karibu watu 190,000 wanahitaji msaada wa kibinadamu haraka, shule 33 zimeathirika na karibu nyumba 10,000 zimeharibiwa.
Katika baadhi ya vijiji shirika hilo linasema, nyumba chache sana zimebaki zimesimama.
Miaka mingi ya mizozo, watu kulazimishwa kuhama makazi yao na matatizo ya kiuchumi yameacha jamii katika eneo hilo zikiathirika zaidi limesema shirika la UNHCR.
Kwa familia nyingi zilizofurushwa makwao shirika hilo linasema , Kimbunga Chido kimesababisha ugumu wa maisha, na kusomba kile kidogo walichoweza kukijenga tena.
UN inashikamana na waathirika wa kimbunga Chido
Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X limesema kimbunga Chido kimeaacha amala kubwa ya uharibifu nchini Msumbiji.
Linasema mvua kubwa na upepo mkali ulioambatana na kimbu nnga hicho vimesambaratisha nyumba, miundombinu , kukata umeme na kuvuruga kabisa mfumo wa mawasiliano.
Hata hivyo limesisitiza kuwa pamoja na changamoto hizo Umoja wa mataifa na washirika wake wako msitari wa mbele kusaidia katika tathimini ya athari na juhudi za kufikisha msaada wa kibinadamu unaohitajika sana.