Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 800,000 wanaokabiliwa na njaa wameshapokea msaada wa chakula Sudan: WFP

Wafanyakazi wakipakua magunia ya chakula cha msaada kutoka kwa lori la Mpango wa Chakula Duniani katika kambi moja nchini Sudan.
WFP/Mohamed Galal Msaada wa chakula unawasilishwa kwa watu waliokimbia makazi yao katika kambi ya Zamzam huko Darfur Kaskazini.

Watu 800,000 wanaokabiliwa na njaa wameshapokea msaada wa chakula Sudan: WFP

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP limesema limeshafikisha msaada wa chakula kwa watu 800,000 wanaokabiliwa na baa la njaa na walio katika hatari ya baa la njaa katika maeneo mbalimbali nchini Sudan tangu ilipozindua kampeni kubwa ya kusambaza msaada wa chakula katika taifa hilo lililoghubikwa na vita iliyozuka upya Aprili 2023.

Shirika hilo linasema operesheni hiyo bado inakabiliwa na changamoto sababu ya hjali tete ya usalama katika maeneo mengi na hatari kwa wahudumu wa misaada.

Hata hivyo WFP inasema licha ya changamoto zote hizo tangu kuzuka kwa vita imefanikiwa kusambaza msaada wa chakula, kutoa fedha taslim na lishe kwa watu milioni 2.8 nchini zniama na mwezi Oktoba ndio ilitoa msaada mkubwa zaidi tangu vita ilipoanza.

Maeneo yaliyoathirika zaidi na njaa na kupokea msaada ni pamoja na Zamzam, Abu Shouk, makambi ya wakimbizi wa ndani ya  Al Salam  Kaskazini mwa Darfur, Kereneik na Sirba Darfur Magharibi,  Sheikan Kaskazini mwa Kordofa, vituo vya  wakimbizi wa ndani Katikati na Kusini mwa Darfur na baadhi ya maeneo yam ji mkuu Khartoumikiwemo Jebel Awlia na kisiwa cha Tuti.

Kwa mujibu wa WFP “Hii inachangia karibu nusu ya watu wote milioni 1.7 wanaokabiliwa na njaa au hatari.”

WFP imesema inafanya kila linalowezekana kupanua wigo wa msaada katika maeneo yote yaliyo katika hatari ya kukumbwa na njaa.

Pia WFP inashinikiza kupata msaada muhimu wa chakula na lishe kwa maeneo 14 yenye njaa, mengi yakiwa ni yenye migogoro katika majimbo ya Darfur, Kordofan, Khartoum na Gezira, ambako licha ya mapigano ya miezi 20, migogoro inaendelea kuongezeka.

Usambazaji wa msaada

WFP imetuma msaada wa chakula mara nne zaidi mwezi Novemba ikilinganishwa na Septemba huku vibali zaidi vikipokelewa kwa misafara ya kibinadamu.

Tangu Septemba, karibu watu 135,000 katika kambi ya Zamzam mahali pekee duniani ambako baa la njaa limethibitishwa wamepokea msaada wa chakula, kupitia chakula cha WFP kilichoingizwa kambini na vocha za bidhaa kwa ajili ya chakula cha asili.

Malori ya kwanza ya WFP tangu Aprili yaliwasili katika kambi ya Zamzam nje ya El Fasher, mji mkuu wa Darfur Kaskazini, tarehe 22 Novemba. Usambazaji wa tani 150 za usaidizi kwa watu 12,500 ulihitimishwa ndani ya wiki moja.

Msafara mwingine wa WFP kwa mujibu wa shirika hilo uko njiani kuelekea kambi ya Zamzam kupitia kivuko cha mpaka cha Adre nchini Chad, ukibeba tani za nafafaka 860 kwa ajili ya kusambazwa kwa zaidi ya watu 70,000.

Njia zinazopatikana kuvuka mpaka kutoka Adre nchini Chad au njia ya kuvuka kutoka Bandari ya Sudan kupitia Dabbah kufikia Zamzam zimekuwa hatari zaidi katika wiki za hivi karibuni huku mapigano na makombora yakiongezeka.

Msafara wa WFP ulifika Kambi ya Kalma huko Beleil, Darfur Kusini hatari eneo jingine lenye hatari ya baa la njaa ikiwa imebeba tani 178 za chakula na lishe kwa ajili ya kusaidia karibu watu 15,000. Hapo awali msafara huu ulipelekwa katika Kambi ya Zamzam lakini ulielekezwa kwingine na WFP kutokana na ukosefu wa usalama njiani.

Misafara ya chakula inaendelea kufikisha msaada

WFP inasema msafara huu uliondoka Bandari ya Sudan tarehe 12 Novemba na kusafiri kupitia Dabbah hadi eneo la Darfur.

Mapigano huko Um Rawwaba, Kordofan Kaskazini, yamezuia msafara wa watu kufika maeneo hatarishi yenye njaa Kaskazini na Kusini mwa Kordofan, ikiwa ni pamoja na Kadugli na Dilling.

Malori hayo yalilazimika kurejea katika eneo salama na yanasubiri kuelekezwa katika maeneo mengine yanayofikiwa na watu wengi katika jimbo la Kordofan Kusini na Blue Nile kadri hali inavyoruhusu.

Msafara huu uliondoka Bandari ya Sudan tarehe 12 Novemba. WFP inaendelea kutoa msaada kuvuka mpaka kutoka Chad kupitia kivuko muhimu cha Adre.

Tangu Agosti, WFP imesema imesafirisha tani 9,800 za msaada kwa zaidi ya watu 850,000 katika eneo la Darfur kupitia ukanda huu muhimu.

WFP pia imesaidia zaidi ya watu milioni mbili kwa msaada wa fedha nchini Sudan mwaka huu hii ni mara kumi zaidi ya watu wanapokea msaada wa fedha kutoka WFP leo kuliko mwanzoni mwa mwaka limesema shirika hilo.

Kupanua wigo wa huduma ya uhamishaji wa pesa taslimu na vocha ni muhimu katika muktadha kwamba kuna ufikiaji mdogo wa kibinadamu.

Shirika hilo limesisitiza kwamba “Mgogoro wa ukwasi wa Sudan ni changamoto inayoendelea”.