Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wafanyakazi wahamiaji duniani waongezeka, wengi wako kwenye sekta ya huduma - ILO

Wafanyakazi wanatekeleza jukumu lao katika kiwanda cha uzalishaji nchini Ethiopia.
ILO Photo/Marcel Crozet
Wafanyakazi wanatekeleza jukumu lao katika kiwanda cha uzalishaji nchini Ethiopia.

Wafanyakazi wahamiaji duniani waongezeka, wengi wako kwenye sekta ya huduma - ILO

Masuala ya UM

Wahamiaji wa kimataifa wameendelea kuongezeka na kuwa na majukumu muhimu kwenye soko la ajira duniani kwani wamechangia asilimia 4.7 ya nguvu kazi yote duniani kwa mwaka 2022, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la Kazi duniani katika ripoti mpya iliyotolewa leo Geneva, Uswisi iliyopatiwa jina Makadirio ya Wafanyakazi Wahamiaji duniani.

Ripotiinadokeza kuwa mwaka 2022 wafanyakazi wahamiaji milioni 167.7 walikuwa sehemu ya nguvu kazi ya nchi walizohamia na kati yao hao milioni 102.7 walikuwa wanaume na milioni 64.9 walikuwa wanawake. Kiwango hicho ni ongezeko kwa zaidi ya wafanyakazi zaidi ya milioni 30 tangu mwaka 2013.

ILO inasema idadi kubwa ya wafanyakazi hao wako kwenye nchi za kipato cha juu ikiwa ni asilimia 68, wengi wao wakiwa Ulaya Kaskazini, Kusini na Magharibi na kisha Amerika ya Kaskazini na nchi za kiarabu.

Ripoti hii imetolewa kuelekea siku ya kimataifa ya wahamiaji tarehe 18 mwezi huu wa Desemba.

Je wafanyakazi hao wanajishughulisha na kazi gani?

Ripoti imeweka bayana kuwa zaidi ya asilimia 68 ya wafanyakazi wote wahamiaji mwaka 2022 walikuwa kwenye sekta ya huduma, ikilinganishwa na asilimia 51.5 ambao si wahamiaji kwenye sekta hiyo.

Hii ina maana wahamiaji wengi ndio wanaofanya kazi kwenye sekta ya huduma katika mataifa hayo ya kipato cha juu.

“Mwelekeo huu ulichochewa kwa kiasi kikubwa na ongezeko duniani la kazi za malezi na za majumbani, hasa miongoni mwa wanawake. Asilimia 28.8 ya wanawake wahamiaji na asilimia 12.4 ya wahamiaji wanaume waliajiriwa kwenye kazi za kuhudumia watu,” imesema ripoti hiyo ikiainisha kuwa katika sekta hiyo wafanyakazi ambao hawakuwa wahamiaji ni asilimia 19.2 wanawake na asilimia 6.2 wanaume.

Changamoto kwenye ajira za wahamiaji wa kimataifa

Wahamiaji walikabiliwa na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira ikilinganishwa na raia wa nchi husika, ambapo wanawake ndio waliokumbwa zaidi ya changamoto hiyo ya kukosa ajira kuliko wanaume.

“Tofauti hii inachochewa na vigezo mbalimbali ikiwemo vikwazo vya lugha, sifa au ujuzi wao kutotambuliwa, ubaguzi, kukosa watu wa kulea watoto wao, matarajio ya kijinsia yanayokwamisha fursa za ajira hasa kwa wanawake,” imesema ripoti hiyo.

Kutatua changamoto za mahitaji ya wafanyakazi wahamiaji

Ripoti inaweka bayana umuhimu wa sera mahsusi kusaidia wafanyakazi wahamiaji wa kimataifa ikiwemo kuhakikisha ajira zinakuwa za kiutu, ulinzi wa kazi zao, ajira zao ziwe endelevu.

“Wafanyakazi wahamiaji ni wa muhimu sana katika kutatua uhaba wa nguvu kazi duniani na kuchangia katika ukuaji wa kiuchumi,” amenukuliwa Mkurugenzi Mkuu wa ILO Gilbert F. Houngbo.

Amesema kuhakikisha haki zao na kupata ajira zenye utu sio tu jambo la kimaadili bali pia ni kitu kinachohitajika kiuchumi.