Vifo vitokanavyo na kuzama majini vyapungua, ingawa bado kuna changamoto - WHO
Vifo vitokanavyo na kuzama majini vyapungua, ingawa bado kuna changamoto - WHO
Hatua za kuepusha watu kuzama na kisha kupoteza maisha zimeanza kuzaa matunda hadi kusababisha kupungua kwa vifo vya watu duniani vitokanavyo na watu kuzama kwenye maji, iwe baharini, ziwani, mtoni au kwenye vijito.
Limesema hii leo shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, WHO, kupitia taarifailiyotolewa leo Geneva, Uswisi.
Jinsi ya kuzuia watu kuzama majini
Mikakati hiyo ni pamoja na kuweka vizuizi ili kuzuia watoto kufikia maeneo yenye maji, kutenga maeneo salama mbali na maji mengi ambako watoto wa chekechea, wanafunzi wanaweza kujifunza stadi za kuogelea, kufundisha watu jinsi ya kuokoa na kupatia pumzi walio hatarini kuzama majini na kusimamia kanuni na sheria za usafirishaji kwenye boti na meli. Halikadhalika mbinu za kudhibiti mafuriko.
Ripoti ya WHO ya kwanza kabisa kuchapishwa kuhusu kuzuia watu kuzama inaonesha vifo vimepungua kwa asilimia 38 tangu mwaka 2000 hadi sasa, ikisema “ni mafanikio makubwa kiafya.”
“Kupungua kwa kiwango hicho ni habari njema na uthibitisho kwamba mikakati rahisi na inayotekelezeka ambayo imependekezwa na WHO inafanya kazi,” amesema Dkt. Tedros Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO kupitia taarifa hiyo.
Kuzama majini kunasalia tishio, mabwawa ya kuogelea hayana uzio
Hata hivyo ripoti inasema kuzama majini kunasalia tishio kubwa la afya ya umma kwani zaidi ya watu 30 hukadiriwa kuzama katika kila saa moja, na watu 300,000 walikufa kwa kuzama maji mwaka 2021.
Idadi kubwa ya vifo hivyo ni watu wenye umri wa chini ya miaka 29, imesema WHO na asilimia 25 ni watoto wenye umri wa chini ya miaka 5.
“Watoto wasio na usimamizi wa mtu mzima wako hatarini kuzama majini,” inasema WHO.
Halikadhalika ripoti inasema mafanikio ya kudhibiti vifo kwa kuzama majini yanatofautiana kikanda kwani vifo 9 kati ya 10 vinatokea katika nchi za kipato cha chini na kati. Eneo la Afrika linalosimamiwa na WHO lilishuhudia kupungua kwa vifo hivyo kwa asilimia 3 tu ilihali Ulaya asilimia 68.
Ni asilimia 15 tu ya nchi za Afrika zina mikakati ya kitaifa ya kuzuia watu kuzama majini.
Mfuko wa Bloomberg
Ni kwa mantiki hiyo, Michael R. Bloomberg ambaye ni Balozi mwema wa WHO wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza na majeraha anasema ripoti inaonesha nini nchi zinapaswa kufanya ili kudhibiti watu kufa kwa kuzama majini.
Mwezi Mei mwaka huu wa 2024, Mfuko wa Usaidizi wa Bloomberg ulitangaza nyongeza ya dola milioni 60 kwa ajili ya kuzuia vifo vitokanavyo na kuzama majini kwenye 6 ikiwemo Uganda, Ghana, Marekani na Viet Nam, na hivyo kufanya uwekezaji wa mfuko huo duniani kote kufikia dola milioni 104.
Iwapo mapendekezo ya WHO hayatazingatiwa, mathalani watu kutoweka uzio kwenye mabwawa ya kuogelea, zaidi ya watu milioni 7.2 wengi wao wakiwa watoto, wanaweza kufa maji ifikapo mwaka 2050.
Ripoti iliandaliwa kufuatia ombi la nchi wanachama wa WHO kupitia Baraza Kuu la Who azimio namba 76 (18) la mwaka 2023.
Soma ripoti nzima hapa.