Baada ya kuangushwa utawala wa Bashar Al-Assad kuna matumaini kwa mamilioni ya waliofurushwa Syria: UNHCR
Baada ya kuangushwa utawala wa Bashar Al-Assad kuna matumaini kwa mamilioni ya waliofurushwa Syria: UNHCR
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR leo limesema Baada ya miaka 14 ya mzozo, matukio ya hivi karibuni ya kuangushwa kwa utawala wa Rais Bashar Al- Assad nchini Syria yameibua matumaini kwamba janga kubwa zaidi duniani la watu kulazimika kuyahama makazi yao linaweza kutatuliwa, lakini mustakabali bado haujulikani ukiwa njiapanda.
Shirika hilo linasema “Katika kipindi cha miaka 14 ya vita na mgogoro, mamia ya maelfu ya Wasyria wameuawa au kujeruhiwa na zaidi ya watu milioni 13 wamelazimika kukimbia makwao ikiwa nis awa na nusu ya idadi ya watu wote wan chi hiyo wa kabla ya vita kuzuka.”
Taarifa ya shirika hilo imeongeza kuwa “zaidi ya Wasyria milioni 7 ni wakimbizi wa ndani ya nchi yao huku wengine zaidi ya milioni 5 wakiishi kama wakimbizi, nje hasa katika nchi jirani za Uturuki, Lebanon na Jordan, lakini pia Ulaya na nchi zingine duniani.”
Kwa mujibu wa shirika hilo la wakimbizi la Umoja wa Mataifa wakimbizi wengi sasa wanajiuliza matukio ya siku za hivi karibuni yatamaanisha nini kwao.
Nina imani na uwezo wa wasyria katika kupanga mustakabali wao - Guterres
Akiwa Afrika Kusini kwenye ziara yake ya kuonesha mshikamano na kusaka haki kwa bara la Afrika, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amezungumzia pia Mashariki ya Kati ambako amesema kinachoendelea eneo hilo ni mabadiliko muhimu, yakiashiria kubadilika kwa ushirika na kushamiri kwa majanga ya kibinadamu, lakini kukiwa na nuru ya matumaini ya mustakabali tulivu.
Amegusia kuibuka kwa matumaini mapya hususan Syria, ambako amesisitiza azma isiyotetereka ya Umoja wa Mataifa ya kusaidia mpito wa uongozi na kujenga mchakato jumuishi wa kisiasa, baada ya serikali ya Rais Bashar Al-Assad kuondolewa madarakani na kundi la HTS.
“Nasisitiza umuhimu wa majawabu yanayoheshimu haki za makundi madogo na kuhakikisha uhuru na mipaka ya Syria inaheshimiwa,” amesema Guterres.
Amekumbusha kuwa, Mjumbe wake Maalum kwa Syria, Geir Pedersen, anashirikiana na pande zote kufanikisha malengo hayo. “Nina imani kubwa na wananchi wa Syria juu ya uwezo wao wa kuamua mustakabali wao,” amesema Katibu Mkuu.
Je nini hatma ya wakimbizi?
Wakati hali bado inabadilika kwa kasi na maswali mengi yanabaki, UNHCR inasema hii ndio tunayojua kwamba “Tangu kuanza kwa mashambulio hayo mapya tarehe 27 Novemba, takriban watu milioni 1 wamehama makazi yao kutoka maeneo ya Aleppo, Hama, Homs na Idlib. Na kwa zaidi ya mtu 1 kati ya 5, hii ni angalau mara ya pili kwao kufurishwa.”
Aidha, kati ya mwishoni mwa Septemba na mwishoni mwa Novemba, UNHCR inasema Syria ilipokea zaidi ya watu nusu milioni waliokimbia mashambulizi ya anga ya Israel katika nchi jirani ya Lebanon.
“Takriban asilimia 60 walikuwa ni Wasyria wanaorejea nyumbani, huku wengine wakiwa ni Walebanon” limesema.
Tangu kusitishwa kwa mapigano kati ya Israel na Lebanon kuanza kutekelezwa tarehe 27 Novemba, takriban wakimbizi 40,000 wa Lebanon wamerejea nchini mwao limesema shirika hilo la UNHCR.
Limeongeza kuwa “ingawa takwimu bado hazijapatikana, lakini maelfu ya wakimbizi wa Syria wameripotiwa kuanza kurejea nchini kwao kutoka Lebanon kupitia kituo rasmi cha mpaka cha Masnaa na vivuko vingine visivyo rasmi.”
Wakati huo huo, baadhi ya Wasyria wamekimbilia upande mwingine na kuingia Lebanon. Wakimbizi pia wanarejea kutoka Uturuki kupitia vivuko vya mpaka vya Bab al-Hawa na Bab al-Salam kuelekea kaskazini-magharibi mwa Syria.
Kauli za maafisa wa UN kuhusu wakimbizi
Mwakilishi wa UNHCR nchini Syria Gonzalo Vergas Llosa amesema kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X kwamba “Nilikuwa kwenye mpaka kati ya Syria na Lebanon leo. Nilikutana na baadhi ya Washami wakirudi nyumbani. Familia hii ilikuwa inarudi Idlib. Wameniambia kwamba walikuwa wameingojea kwa miaka 12 siku hii. Kwao kurudi ilikuwa sherehe.”
Ikiwa wimbi kubwa la watu kurejea nyumbani litafanyika uhamishaji wa amani wa mamlaka, uvumilivu katika jumuiya za wanaorejea na kuongeza misaada ya kibinadamu na ya kifedha kutoka kwa jumuiya ya kimataifa vitahitajika. Huu ni wakati wa fursa kubwa” amesema Gonzalo.
Kwa upande wake Kamisha mkuu wa wakimbizi Filippo Grandi amesema Maswali mengi yanaulizwa juu ya mustakabali wa wakimbizi wa Syria hali bado ni tete uvumilivu unahitajika.
Ameongeza kuwa wote lazima waunge mkono mageuzi ya amani, ni muhimu ili kuleta faida za hiari na zenye heshima na utu.
Amesema UNHCR na washirika wamesalia nchini Syria, wakitoa misaada ya kibinadamu inayohitajika sana.
Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP kupitia ukurasa wake wa X limesema linafuatilia mienendo ya watu baada ya kusitishwa kwa mapigano Syria na kurekebisha msaada wake kwa watu waliokimbia makazi yao na wanaorejea nyumbani.
Shirika hilo limesema wikii hii imefanya misafara 3 ya ushirikino na mashirika mengine kuelekea Kaskazini na Kusini, kupeleka msaada wa chakula na usio wa chakula katika maeneo yaliyoathiriwa sana.