Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF Rwanda kwa kushirikiana na UNICEF Switzerland na Liechtenstein wafanikisha ‘kinesitherapy’ kwa watoto

Mtoto mchanga mweusi aliyevaa sare ya shule ya bluu anaosha mikono yake kwenye bomba la maji la kijani katika Kituo cha Maendeleo ya Watoto Wadogo cha Gikomero nchini Rwanda.
© UNICEF/Olivier Minega Mtoto akinawa mkono nchini Rwanda.

UNICEF Rwanda kwa kushirikiana na UNICEF Switzerland na Liechtenstein wafanikisha ‘kinesitherapy’ kwa watoto

Afya

Nchini Rwanda Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF kwa msaada wa UNICEF Switzerland na Liechtenstein wamesaidia tiba kwa njia ya mazoezi kuponya watoto wenye ulemavu wa viungo. 

Katika Wilaya ya Bugesera kwenye Jimbo la Mashariki nchini Rwanda, programu inayofadhiliwa na UNICEF inafanya kile ambacho kwa lugha kitabibu kinaitwa Kinesiotherapy. Tiba ya kutembeza viungo vya mwili ili kuvipa nguvu. Kwa watoto tiba hii inafanya kazi kwa ufanisi inapofanywa mapema wakiwa bado wadogo.

Francoise Uwuzuyinema, mama wa Joshua anaeleza kwamba Joshua aliyezaliwa mwaka 2019 ni mtoto wa nne kwa kuzaliwa na ndiye mdogo katika ndugu zake. Alizaliwa kabla ya wakati…miezi 7, na kadri muda ulivyosogea alianza kugundua mtoto wake anachelewa kuimarika kimwili.

Anasema alikuwa na bahati kukutana na programu hii ya UNICEF, mtoto wake akaanzishiwa mazoezi na wazazi wakaoneshwa cha kufanya. Hivi sasa Joshua ambaye alikuwa hawezi kutembea, anaenda shuleni kama watoto wengine.

“Alipoanza kinesitherapy nilianza kuona mabadiliko. Akaimarika kiasi cha kukaa mwenyewe, kushika chombo na kula mwenyewe bila usaidizi wowote. Hii ilinipa nguvu zaidi ya kuendelea na juhudi zangu. Anapoamka anapenda kupiga mswaki na kunisaidia kufagia sakafu. Anafurahia sana hiyo. Na anapenda sana mpira wa miguu hasa mtu anapopiga mpira kwa nguvu. Joshua anapenda hiyo.”