Elimu ndio ufunguo wa kutokomeza FGM Kenya: UNFPA
Elimu ndio ufunguo wa kutokomeza FGM Kenya: UNFPA
Wakati ulimwengu ukihitimisha leo siku 16 za uhamasishaji wa kupinga ukatili wa kijinsia, ukeketaji wa wanawake ambao ni ukatili dhidi ya wanawake na ukiukwaji Mkubwa wa haki za binadamu bado ni tatizo katika baadhi ya jamii duniani.
Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi UNFPA, ukeketaji huchangia matatizo ya afya ya uzazi na kusababisha hali kama fistula na madhara mengine.
Jamii za wafugaji nchini Kenya aghalabu bado zinaendekeza mila hiyo potofu ya ukeketaji na tamaduni huo umekita mizizi ijapokuwa juhudi za kuupiga vita zinaendelea.
Takwimu rasmi za Kenya zinaashiria matumaini kwamba ukeketaji umepungua kwa nusu katika kipindi cha miongo miwili iliyopita.
Wanawake wakielimishwa ukeketaji unapungua
Hata hivyo, tathmini ya serikali ya idadi ya watu na afya ya mwaka 2022, KDHS, ilibaini kuwa ukeketaji ni tatizo hasa katika jamii ambazo wanawake hawajapata elimu rasmi shuleni.
Elly Modestar ni mkaazi wa Koija katika kaunti ya Laikipia na anakiri kuwa kina mama wa jamii yake wanahitaji msukumo wa elimu ili kutupilia mbali mila zilizopitwa na wakati kwani ”Kwasababu ya mila na desturi ya ndoa za utotoni na ukeketaji, sasa hivi tumeona umuhimu wa kwenda kwenye shule kuzungumza na wasichana wetu ili watimize ndoto zao ndipo wawe watu muhimu kwa jamii.”
Ameongeza kuwa “Ukeketaji ni kitu kinachoendelea kupungua maana hata wasichana wenyewe wana sauti na wanakataa kukeketwa. Na sisi kina mama tuliokuwa tunawakeketa wasichana tumesema mila na desturi ambazo hazifai tunazipiga vita hadi zitokomee,”anasimulia.
Mwanamke 1 kati ya 4 amekeketwa Afrika
Kwa mujibu wa shirika la UNFPA, mwanamke mmoja kati ya wanne amekeketwa katika eneo la Afrika lililo kusini mwa jangwa la Sahara.
Hata hivyo idadi na viwango vinatofauatiana kutokea nchi hadi nchi. Kigen Korir ni mshauri wa masuala ya afya ya uzazi katika shirika la UNFPA na anasisitiza kuwa silaha kubwa ni elimu katika jamii kuhusu madhara ya ukeketaji kwavile,
” Ni swala ambalo limekithiri katika sehemu mbalimbali nchini Kenya na vilevile katika eneo la Afrika lililo kusini mwa jangwa la Sahara. Imefika wakati ambapo suala hili linapaswa kuzungumziwa kwa kina.Tumekuwa na lengo kuwa ifikapo mwaka 2030 ,masuala yanayoibuka katika jamii yawe yametokomea.”.
Mpango wa Beijing wa haki za wanawake kutimiza miaka 30
Mpango wa kuhakikisha usawa wa kijinsia kupitia tamko la Beijing, BfPA unatimiza miaka 30 mwakani tangu kuanza kufanya kazi.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa dhamira ni kushinikiza usawa wa kijinsia na haki za wanawake na wasichana kwa jumla.
Elimu ni silaha muhimu katika vita dhidi ya ukeketaji anasimulia Josephine Ndirias, muasisi wa shirika la kupambana na ukeketaji huko Il Ngwesi katika kaunti ya Laikipia na anahisi kuwa,” Idadi ya watoto wa kike wanaojiunga na shule na kusoma ni kubwa na imeongezeka. Kinachoturejesha nyuma kwa sasa ni mimba za utotoni. Wazazi wasiopungua asilimia 90 wamewapeleka watoto wao shuleni na hayo ni mabadiliko makubwa sana.”
Ameongeza kuwa “Pili, mila potofu kama ukeketaji kitambo zilikuwa zinafanyiwa sherehe kubwa lakini kwa sasa huwezi kuona wala kujua zilifanyika kwani hakuna sherehe au mavazi maalum waliokuwa wanapewa wasichana kwahiyo mabadiliko ni mengi.Pia wanawake walikuwa hawasikiki lakini sasa wana sauti katika jamii kwahiyo yote hayo ni mabadiliko makubwa.”
Shirika la UNFPA la umoja wa mataifa limekuwa mstari wa mbele kufanya kazi na serikali na wadau wengine kuutokomeza ukeketaji. Takwimu rasmi zinaashiria kuwaasilimia 21 ya wanawake wa Kenya walio na umri kati ya miaka 15-49 wamefanyiwa aina fulani ya ukeketaji. Korir Kigen afisa wa shirika la UNFPA anaelezea hatua zilizopigwa hadi sasa, na ”UNFPA imekuwa ikishirikiana na wadau wengine kama wizara za afya na mashirika ya kijamii kama Amref, wakfu wa MPESA, Wakfu wa Fistula na Amref Flying Doctors kuweza kuhakikisha kuwa mbali na mifumo ya afya inawahudumia wagonjwa wanavyohitaji,kuna madaktari wa kutosha waliopata mafunzo mujarab kushughulikia masuala hayo, wakunga waliopata elimu ili kuweza kuwajibika,”anasimulia.
Takwimu za UNFPA zinakisia kuwa wasichana milioni 68 wamekuwa katika hatari ya kukeketwa kwenye kipindi cha kati ya mwaka 2015 hadi 2030.
Utamaduni huu wa kikatili una madhara ya afya ya uzazi na kisaikolojia na hufanyika kwenye mazingira magumu.
Siku 16 za uhamasishaji wa kupinga ukatili wa kijinsia ni fursa ya kuzipa nguvu mpya ahadi za Umoja wa Mataifa za kutokomeza jinamizi hili na kadhalika kuimarisha mapambano.