Mpango wa kurekebisha katiba DRC waleta mvutano - Keita
Mpango wa kurekebisha katiba DRC waleta mvutano - Keita
Mvutano wa kisiasa unaendelea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kufuatia wito wa wito wa kukata kuangaliwa upya kwa hatua ya marekebisho ya katiba, na kuzidi kuporomoka kwa hali ya usalama kwenye majimbo ya Ituri na Kivu Kaskazini.
Taarifa hiyo imetolewa na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, Bintou Keita wakati akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani leo lililokutana pamoja na mamo mengine kupokea ripoti ya Katibu Mkuu wa UN kuhusu hali ya usalama mashariki mwa DRC kuanzia Septemba 20 mwaka huu.
Mwezi Oktoba mwaka huu, Rais wa DRC Félix Tshisekedi alidokeza marekebisho hayo akisema katiba ya sasa imepitwa na wakati na inahitaji kuendana na mazingira ya sasa, na kuelezea nia yake ya kuunda kamisheni ya kuandaa rasimu ya katiba mpya.
Hata hivyo vyama vya upinzani na mashirika ya kiraia wanapinga hatua hiyo wakidai kuwa rais anataka kuongeza muda wake wa uongozi na kutaja vifungu kwenye katiba ya sasa vinavyozuia marekebisho ya idadi na muda wa uongozi wa rais.
Makundi yaliyojihami yazidi kutesa raia
Kuhusu hali ya usalama bi, Keita ambaye pia ni Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa kwa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO, ametaja makundi ya ADF, M23, CODECO na Zaïre kuwa yanatikisa usalama huko Ituri na Kivu Kaskazini na kwamba “M23 ambalo halikutia saini makubaliano ya sitisho la mapigano limejiimarisha udhibiti wake wa kijeshi na kiraia kwenye maeneo ya Masisi, RUtshuru, Walikale Nyiragongo na Lubero jimboni Kivu Kaskazini,” eneo ambalo ni mara mbili ya lile walidhibiti mwaka 2012.
Ingawa hivyo kundi la ADF limesalia kuwa kundi katili zaidi likiwa limeua mamia ya raia katika miezi ya karibuni.
Usalie nyumbani uende kambini kote ni sawa hakuna usalama
Hali tete ya usalama imethibitishwa pian a Passy Mubalama ambaye alihutubia wajumbe kwa njia ya video kutoka DRC akisema, kambi za wakimbizi zimegeuka pahala pa ghasia, hakuna usalama.
"Kwa wakimbizi, kukimbilia kambini au kusalia nyumbani ni sawa na kuchagua wapi ukauawe,” amesema Bi. Mubalama akimnukuu Noella mama mwenye umri wa miaka 26, mmoja wa watu wanaowasaidia
Noella anatoka Masisi na aliwaeleza kuwa mumewe aliuawa na waasi wa M23 wakati waasi hao walipotwaa mji wa Mushaki.
Hali tete ya usalama pamoja na mabadiliko ya tabianchi vimezidi kutwamisha hali ya kibinadamu kwani kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kiutu, OCHA, takribani watu milioni 6.4 sasa ni wakimbizi huku milipuko lukuki ya magonjwa yanafanya hali kuwa mbaya zaidi.
Baraza na mamlaka na majukumu mapya ya MONUSCO
Bi.Keita akaeleza kwamba wakati huu Baraza linajiandaa kubaini jukumu jipya la MONUSCO ambalo kwa sasa linapatia kipaumbele ulinzi wa raia sambamba na kupokonya silaha, kuvunja makundi yaliyojihami na kujumuisha wapiganaji uraiani, DDR, na marekebisho ya sekta ya ulinzi, SSR.
“Napenda kusisitiza kuwa MONUSCO imejizatiti na mpango wake wa kuondoka DRC kwa mpango wajibifu. Na kwa kuzingatia mafundisho ya Kivu Kusini, MONUSCO na serikali ya DRC wanashirikiana kwenye mpango wa kuondoka unaozingatia hali ya usalama na mahitaji ya ulinziwa raia.
Muda wa MONUSCO unatarajiwa kumalizika tarehe 20 mwezi huu wa Desemba.
Kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC
Akihutubia Baraza, Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC, Thérèse Kayikwamba Wagner, amezungumzia kuongeza muda wa MONUSCO na kusema “lazima uzingatie mtazamo wa sasa wa kikanda kwenye mzozo unaoendelea huku ikizingatia mpango wa kuondoka taratibu na wenye uwajibikaji.
“Hii ni muhimu kutatua vitisho vya mipakani na kuhakikisha hakuna ombwe la usalama,” amesema Bi. Kayikwamba Wagner.
Huu si mzozo wa DRC na Rwanda
Mwakilishi wa Kudumu wa Rwanda kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Ernest Rwamucyo, alitumia hotuba yake kueleza kuwa “kutazama mzozo unaoendelea kama chuki kati ya nchi za Afrika kunaondoka mazingira ya mzozo huo na nafasi ya pande mbalimbali zinazohusika kwenye mzozo huo.”
Amesema, “hili si suala la Rwanda na DRC bali ni mzozo wenye sura mbalimbali ambao unahitaji uelewa wa kina na hatua zinazoratibiwa na jamii ya kimataifa.”
Mkutano wa utatu kufanyika Luanda Desemba 15
Angola inaratibu Mchakato wa amani wa Luanda ambao uliwezesha kutiwa saini wa sitisho la mapigano hivi karibuni kati ya Rwanda na DRC.
Naibu Mwakilishi wa Angola kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Mateus Luemba, amewajulisha wajumbe kuwa mkutano wa utatu kati ya Angola, Rwanda na DRC utafanyika tarehe 15 mwezi huu wa Desemba huko Luanda chini ya Rais Lourenço wa Angola.
Mkutano huo utasongesha hatua za kuleta utulivu kwa ajili ya amani mashariki mwa DRC .
“Hata hivyo tunapenda kuwa wazi kwa mara nyingine tena kwamba juhudi za msuluhishi zitakuwa na mafanikio iwapo pande zote husika na wadau, likiwemo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wataendelea kuunga mkono mchakato huu ili uchangie katika mazingira bora ya usalama na utulivu kwenye ukanda huu,” amesema Balozi Luemba.