Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yaisaidia serikali ya DRC kuchunguza mlipuko wa ugonjwa usiojulikana Panzi jimboni Kwango

Maafisa wa afya kutoka Shirika la Afya Duniani, UNICEF, na Tume ya Ulaya wakikagua shehena kubwa ya shehena ya chanjo ya mpox katika uwanja wa ndege katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
© WHO Dozi 99,000 za chanjo ya mpox iliyotolewa na Tume ya Ulaya yawasili Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

WHO yaisaidia serikali ya DRC kuchunguza mlipuko wa ugonjwa usiojulikana Panzi jimboni Kwango

Afya

Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO linatuma wataalam kusaidia mamlaka ya afya nchini  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC kufanya uchunguzi zaidi ili kubaini chanzo cha ugonjwa ambao bado haujatambuliwa ambao umeripotiwa katika eneo la Panzi, katika jimbo la Kwango kusini magharibi mwa nchi hiyo.

Uchunguzi wa kimaabara unafanywa ili kujua chanzo cha kuzuka kwa ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa  shirika hilo wataalamu hao wa WHO wanajiunga na Timu ya Kitaifa ya Hatua za Haraka na wako njiani kuelekea Panzi.

Timu hiyo inajumuisha wataalamu wa magonjwa, watatabibu, wataalamu wa maabara, wataalamu wa kuzuia na kudhibiti maambukizi, na wataalam wa mawasiliano ya hatari.

Timu ya awali ya WHO ya ndani imekuwa ikisaidia mamlaka ya afya huko Kwango tangu mwisho wa mwezi Novemba ili kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa na kutambua waathirika.

Timu pia zinafikisha dawa na vifaa vinavyohitajika

Kwa mujibu  wa WHO Wataalam hao wanaotumwa Panzi pia wanawasilisha dawa muhimu, vifaa vya uchunguzi na ukusanyaji wa sampuli ili kusaidia kuchambua haraka na kubaini sababu ya ugonjwa huo.

Timu zitazingatia kuimarisha hatua za kukabiliana na hali kama vile uchunguzi wa magonjwa na ukusanyaji wa sampuli kwa ajili ya kupima, kutafuta waathirika, matibabu na shughuli za uhamasishaji wa umma.

Dkt. Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika amesema “Timu pia zitafanya kazi na viongozi wa jamii kusaidia ufuatiliaji wa magonjwa na kuongeza hatua za kuzuia maambukizi, kubaini wagonjwa na kuripoti kesi zaidi.”

Ameongeza kuwa "Kipaumbele chetu ni kutoa msaada muhimu kwa familia na jamii zilizoathiriwa. Juhudi zote zinaendelea ili kubaini chanzo cha ugonjwa huo, kuelewa njia zake za maambukizi na kuhakikisha zinachukuliwahatua zinaofaa kwa haraka iwezekanavyo.”

Kulingana na takwimu Wizara ya Afya ya Umma ya DRC, kesi 394 na vifo 30 vimeripotiwa hadi sasa katika eneo la afya la Panzi.

“Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na maumivu ya kichwa, kikohozi, homa, matatizo ya kupumua na upungufu wa damu. Hadi matokeo ya uchunguzi wa maabara yatakapokelewa, chanzo cha ugonjwa huo bado haijulikani”.

Kuhusu eneo la Panzi liliko

Panzi ni jamii ya mashambani inayopatikana zaidi ya kilomita 700 kutoka mji mkuu wa DRC Kinshasa.

Upatikanaji wa barabara ni mgumu na mtandao wa mawasiliano ni mdogo. Kufikia sasa, ugonjwa huo umeripotiwa katika kanda saba kati ya 30 za afya katika jimbo la Kwango.

WHO inasema  kesi nyingi zinaripotiwa katika maeneo matatu kati ya saba yaliyoathiriwa.

WHO inasema Pathojeni ya upumuaji kama vile mafua au coronavirus">COVID-19 vinachunguzwa kama chanzo kinachowezekana, pamoja na malaria, surua na maradhi mengine.