Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 15 ya Mkataba wa Kampala kuhusu wakimbizi wa ndani, wito watolewa kwa nchi kuidhinisha na kutekeleza

Wanawake wakipakia mali zao kwenye lori la UNHCR huko Malakal, Sudan Kusini.
© UNHCR/Charlotte Hallqvist Raia wa Sudan Kusini waliokimbia makazi yao huko Malakal wakipakia mali zao zilizosalia kwenye lori la kubeba mizigo la UNHCR ili kusafirishwa hadi eneo la wakimbizi wa ndani.

Miaka 15 ya Mkataba wa Kampala kuhusu wakimbizi wa ndani, wito watolewa kwa nchi kuidhinisha na kutekeleza

Wahamiaji na Wakimbizi

Katika kuadhimisha miaka 15 tangu kupitishwa kwa Mkataba wa Kampala wa Ulinzi na Usaidizi wa Wakimbizi wa Ndani barani Afrika chini Muungano wa Afrika, Kamishna Mkuu Msaidizi wa Ulinzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, Ruven Menikdiwela NA Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu za Wakimbizi wa ndani Paula Gaviria Betancur wametoa kauli ya pamoja ya kupongeza Muungano wa Afrika kwa maono haya ya mbali na pia kuzisihi nchi zote barani Afrika kuutekeleza mkataba huo muhimu.

“Mkataba huu wa kihistoria unasalia kuwa mfumo wa kwanza duniani na wa pekee unaobana kisheria, unaofanya kazi kote katika bara, unaolenga kulinda haki na ustawi wa watu waliofurushwa ndani ya nchi zao. Mkataba unaonesha uongozi wa Afrika na kujitolea kwa pamoja katika kushughulikia changamoto zinazokabili mamilioni ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na migogoro, vurugu, ukiukwaji wa haki za binadamu, majanga na athari za mabadiliko ya tabianchi,” ndivyo ilivyoanza taarifa ya pamoja ya wawili hao waliyoitoa leo jijini Geniva, Uswisi hii leo Desemba sita.

Watu waliokimbia makazi yao katika makazi ya UNHCR huko Plain Savo, DRC, wanarudi kutoka kuchota maji.
© UNHCR/Hélène Caux Wanawake wakichota maji katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. (Maktaba)

Hali si nzuri bado

Wameeleza takwimu kwamba Wakimbizi wa ndani (IDPs) katika bara zima la Afrika wanaendelea kukabiliwa na changamoto kubwa, huku suluhu za kudumu za uhamishaji wao zikisalia kuwa ngumu. Hadi kufikia mwisho wa mwaka jana 2023, karibu nusu ya Wakimbizi wa ndani milioni 75.9 duniani walikuwa barani Afrika. Kuanzia Januari hadi Juni 2024, mzozo nchini Sudan ulisababisha watu milioni 1.5 kuyahama makazi yao, na kusababisha watu milioni 10.5 kuwa wakimbizi wa ndani nchini humo.

Vile vile, ghasia zinazoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zilisababisha wakimbizi wapya 852,000 katika nusu ya kwanza ya mwaka, na kusababisha zaidi ya Wakimbizi wa ndani milioni 7. Mashambulizi ya makundi yasiyo ya kiserikali yenye silaha nchini Msumbiji yaliwafanya watu 201,000 kukimbia makazi yao, na hivyo kuongeza idadi ya Wakimbizi wa ndani hadi karibu 600,000. Wakati huo huo, Nigeria ilikumbwa na mafuriko makubwa mnamo Septemba 2024, na kusababisha zaidi ya watu 600,000 kuyahama makazi yao katika siku chache, nyongeza katika watu milioni 3.3 waliokimbia makazi hapo awali.

Takwimu hizi zinasisitiza haja ya dharura ya kuendelea kuchukua hatua na jukumu kuu la Mkataba wa Kampala katika kuelezea majukumu ya Mataifa na wadau wengine wasio serikali, ikiwa ni pamoja na makundi yenye silaha na wadau wengine. Pia inazipa Nchi Wanachama mwongozo wa kuratibu hatua zao katika ngazi za kitaifa na za ngazi za chini, huku ikisisitiza kujumuishwa kwa watu waliofurushwa na jamii zinazowakaribisha katika kutafuta suluhu za kudumu.

Mvulana mdogo aliyevaa vipokea sauti vya masikioni vya bluu anatumia kompyuta kibao wakati wa kikao cha kujifunza mtandaoni katika eneo linalowafaa watoto UNICEF nchini Sudan.
© UNICEF/Ahmed Mohamdeen Elfati Watoto wanahudhuria kikao cha mafunzo ya kielektroniki katika kambi ya muda ya wakimbizi wa ndani Abdullah Naj huko Port Sudan.

Pongezi

Wamepongeza maono ya mbele ya Muungano wa Afrika na kujitolea kwa Nchi Wanachama 34 ambazo zimeridhia Mkataba huo katika kipindi cha miaka 15 iliyopita.

“Tunatambua na kupongeza hatua madhubuti zilizochukuliwa kutekeleza Mkataba, hasa kwa kujumuisha vifungu vyake katika sheria za kitaifa, na tunasalia kujitolea kuunga mkono juhudi hizi zinazoendelea. Hadi sasa, nchi 21 za Afrika zimepitisha sheria na sera 43 zinazoshughulikia wakimbizi wa ndani. Simulizi za mafanikio zinatoka Niger, Chad, na Jamhuri ya Congo, ambapo mkataba huo umegeuzwa kuwa sheria ya kitaifa. Nchi hizi zinatoa mifano muhimu kwa nchi zingine kufuata.” Wamesema.

Wito

Katika maadhimisho haya, UNHCR na Mtaalamu Maalum wanathibitisha tena kujitolea kwao kusaidia Nchi Wanachama wa Muungano wa Afrika katika kuendeleza ulinzi, usaidizi na suluhu kwa Wakimbizi wa ndani. “Tunatoa wito kwa Nchi Wanachama wa Muungano wa Afrika ambazo bado hazijaidhinisha au kujumuisha Mkataba wa Kampala katika sheria ya kitaifa kuchukua hatua bila kuchelewa na kuhakikisha kwamba masharti yake yanatekelezwa kikamilifu ili kutoa ulinzi wa maana kwa wale walioathiriwa na kuhama.”