Mashambulizi Kaskazini mwa Gaza yanakwamisha ufikishaji wa huduma muhimu za afya zinazohitajika: WHO
Mashambulizi Kaskazini mwa Gaza yanakwamisha ufikishaji wa huduma muhimu za afya zinazohitajika: WHO
Afya
Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO leo limeonya kwamba mashambulizi ya Israel yanayoendelea Kaskazini mwa Gaza yanaendelea kuzuia upatikanaji wa huduma muhimu za afya zinazohitajika sana.
Akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini Geneva Uswisi Dkt. Richard Peeperkorn ambaye ni mwakilishi wa WHO katika eneo linalokaliwa la Palestina amesema “Ufikiaji wa hospitali za Kamal Adwan, Al Awda na Indonesia bado umewekewa vikwazo vikali, huku kukiripotiwa uhaba mkubwa wa vifaa vya matibabu, mafuta na vitengo vya damu na operesheni za WHO zinaendelea kutatizwa kwa kiasi kikubwa.”
Amesema “tangu Oktoba 2023 na kufikia tarehe 4 Desemba mwaka huu asilimia , 58 ya operesheni 273 zilizopangwa kuongozwa na WHO ndani ya Gaza aidha zilikataliwa, kufutwa au kuzuiwa, hukukukiwa na operesheni chache zaidi zinazokamilika Kaskazini mwa Gaza.”
Mashambulizi katika hospitali ya Kamal Adwan yanaendelea
Dkt. Peeperkon ameeleza kuwa Jana tarehe 5 Disemba, vifaa vya kijeshi vya quadcopter vilifanya shambulizi katika hospitali ya Kamal Adwan huko Beit Lahia. Kulingana na wizara ya afya yaGaza mgonjwa mwenye umri wa miaka 16 aliuawa akiwa kwenye kitimwendo akipelekwa kwenye vipimo vya x-ray.
Ameongeza kuwa “Watu wengine 12 walijeruhiwa wakiwemo wahudumu 2 wa afya, 1 kati yao alipata jeraha mbaya. Hospitali ilipigwa risasi na quadcopter mara 8 kuanzia asubuhi hadi jioni. Mitambo ya hewa ya oksijeni na mfumo wa maji katika hospitali hiyo pis vilipata uharibifu.”
Katika wiki iliyopita amesema mashambulizi yalisababisha wahudumu watatu wa afya kujeruhiwa, kifo cha muuguzi mkuu wa kitengo cha wagonjwa mahututi au ICU na uharibifu wa jenereta za hospitali.
Misaada ya WHO Gaza Kaskazini
Kwa mujibu wa WHO tarehe 30 Novemba hadi 2 Desemba, WHO na washirika walifanya operesheni Kaskazini mwa Gaza, kupeleka mafuta, vifaa, ikiwa ni pamoja na vifurushi vya chakula, na kusaidia kupelekwa kwa timu za Matibabu ya dharura kwenye sehemu hiyo.
Katika hospitali ya Kamal Adwan iliwasilisha lita 10 000 za mafuta, vifurushi 200 vya chakula, mahitajiya vitengo vya damu na vifaa vya matibabu.
Baada ya wiki 7 za majaribio bila mafanikio na kukataliwa operesheni za msaada, timu ya kimataifa ya matibabu ya dharura EMT hatimaye ilitumwa katika Hospitali ya Kamal Adwan ili kuisidia hospitali hiyo ifanye kazi na timu ziilijumuisha madaktari wawili wa upasuaji, wauguzi wawili wa dharura, daktari na mtaalamu wa magonjwa ya wanawake.
Pia usambazaji wa EMT ulikuwa umekataliwa angalau mara tano katika wiki chache zilizopita.
Mji wa Gaza ulipokea lita 24,000 za mafuta na vifaa vya matibabu kwenye Hospitali ya Al-Shifa ili kusambazwa katika hospitali zingine, na kwenye ghala la WHO katika Jiji la Gaza.
Na huduma za uhamisho wa matibabu ziilifanikiwa kuhamisha wagonjwa watatu muhimu kutoka Kamal Adwan hadi hospitali ya Al-Shifa na wagonjwa wengine 7 na wenzao 18 kutoka mjiwa Gaza hadi katika hospitali ya European Gaza na na kituo cha matibabu cha Nasser Medical Complex kwa ajili ya uhamisho wa kimataifa wa matibabu hadi nchini Jordan ambao ulifanyika tarehe 3 Desemba.
Mashambulizi katika vituo vya afya
WHO inasema tangu tarehe 7 Oktoba 2023 hadi 6 Desemba 2024, zaidi ya mashambulizi 1249 dhidi ya huduma za afya yamethibitishwa, na mashambulizi 591 huko Gaza wakati mashambulizi 658 yamefanyika katika Ukingo wa Magharibi.
Na kuhusu operesheni za misaada tangu Oktoba 2023 na kufikia tarehe 4 Desemba, asilimia 58 ya operesheni 273 zilizopangwa kuongozwa na WHO ndani ya Gaza zilikataliwa , operesheni misioni 66 sawa na asilimia 24 zilifutwa, operesheni misheni 26, saw ana asilimia 10 zilizuiwa , operesheni misioni 65 au asilimia 24, na chini ya nusu au asilimia 42 ya operesheni misheni 116 ndio zimekamilika.