Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wenye ushawishi Syria chukueni hatua kumaliza machungu yanayoendelea - Guterres

Katibu Mkuu António Guterres akihutubia waandishi wa habari kuhusu matukio ya hivi karibuni nchini Syria.
UN Photo/Loey Felipe
Katibu Mkuu António Guterres akihutubia waandishi wa habari kuhusu matukio ya hivi karibuni nchini Syria.

Wenye ushawishi Syria chukueni hatua kumaliza machungu yanayoendelea - Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kumaliza mapigano nchini Syria, ambako mashambulizi yaliyoshamiri hivi karibuni yameibua hofu ya kusambaa zaidi na mgawanyiko kwenye vita hiyo ya wenyewe kwa wenyewe.

António Guterres ametoa wito huo akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Baraza la Usalama kuzungumzia ‘kihoro’ kinachoendelea kila uchao.

“Punde nimezungumza na Rais Erdoğan wa Uturuki kujadili kinachoendelea hivi sasa,” amesema  Katibu Mkuu.

Amesisitiza udharura wa kufikishia raia wote misaada ya kibinadamu – na kurejea kwa mchakato wa kisiasa unaoongozwa na Umoja wa Mataifa ili kumaliza umwagaji damu. “Pande zote zina wajibu wa kuzingatia sheria ya kimataifa na kulinda raia.”

Matokeo ya mashambulizi ya makombora huko Aleppo, Syria (Oktoba 2023)
© UNOCHA/Bilal Alhammoud
Matokeo ya mashambulizi ya makombora huko Aleppo, Syria (Oktoba 2023)

Tumeshindwa kunusuru Syria

Bwana Guterres anasema mapigano haya mapya yalianzishwa na wanamgambo wa Hayat Tahrir al-Sham dhidi ya maeneo yanayodhibitiwa na serikali, kundi ambalo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalitambua kuwa magaidi sambamba na makundi mengine ya upinzani yaliyojihami.

Mapigano hayo yameleta maeneo mapya ya mapigano na makumi ya maelfu ya raia wako hatarini kwenye ukanda huo ambao tayari mapigano yameshamiri.

“Tunashuhudia matunda machungu ya kushindwa kwa pamoja kusongesha juhudi zetu za awali za kukomesha mapigano.” Amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa “juhudi hizo za awali zimeshndwa kuzalisha sitisho dhahiri la mapigano nchini kote Syria au mchakato makini wa kisiasa ili kutekeleza maazimio ya Baraza la Usalama. Hii lazima ibadilike.”

Katibu Mkuu António Guterres akihutubia waandishi wa habari kuhusu matukio ya hivi karibuni nchini Syria.
UN Photo/Loey Felipe
Katibu Mkuu António Guterres akihutubia waandishi wa habari kuhusu matukio ya hivi karibuni nchini Syria.

Katibu Mkuu amesema baada ya miaka 14 ya mzozo Syria, ni wakati sasa kwa pande kinzani kushirikiana na Mjumbe Maalum wa UN kwa Syria, Geir Pedersen, ili hatimaye kuanza mwelekeo mpya, jumuishi na wa kina wa kutatua mzozo kwa mujibu wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 2254 (2015).

“Ni wakati wa mashaurino ya kina,” amesema Guterres. “Kwa maneno mengine, kurejesha kujitawala kwa Syria, umoja, uhuru na kujisimamia eneo lake – na kutimiza matamanio halali ya wananchi wa Syria.”

Kumaliza machungu

Ametambua kuwa Syria iko kwenye njia panda ya ustaarabu, na kwamba inaumiza kuona mparaganyiko wa taifa hilo.

Amekumbuka enzi zake akiwa Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR akisema “tulishuhudia ukarimu mkubwa wa wasyria, ambao walifungua nyoyo zao na milango ya nyumba zao kuwahifadhi wakimbizi kutoka Iraq.”

Siku tano mfululizo za makombora na mashambulizi ya anga yalisababisha uharibifu katika eneo la Idleb kaskazini-magharibi mwa Syria na maeneo ya mashambani ya Aleppo magharibi.
© UNOCHA

“Inanivunja moyo kuona machungu yao sasa yanaongezeka – sambamba na tishio la usalama wa kikanda na kimataifa,” amesema Katibu Mkuu.

“Kwa mara nyingine tena, nasihi wale wenye ushawishi watekeleze wajibu wao ili kumaliza machungu ya muda mrefu yanayokabili wananchi wa Syria,” ametamatisha Guterres.