Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ajabu hata katiba za Afrika ziko kwa lugha za Ulaya – Profesa Ngũgĩ wa Thiong’o

Ngũgĩ wa Thiong'o, profesa kutoka Chuo Kikuu cha California, Irvine, ameketi katika mazingira ya ndani huku piano ikiwa nyuma.
UNOOSA Ngũgĩ wa Thion’go, Profesa wa lugha ya Kiingereza na fasihi kutoka Chuo Kikuu cha California, Irvine.

Ajabu hata katiba za Afrika ziko kwa lugha za Ulaya – Profesa Ngũgĩ wa Thiong’o

Haki za binadamu

Haki si haki iwapo inatolewa kwa lugha ambayo haileweki kwa wahusika, wamejulishwa washiriki wa mkutano wa pili wa wanazuoni unaofanyika hapa makao makuu ya Umoja wa Mataifa New York, Marekani na pia mtandaoni ukimulika Madaraka, Haki na Binadamu: Utawala wa Sheria na mabadiliko Afrika. 

Mmoja wa washiriki wa mkutano huo, akianza hotuba yake kwa kujitambulisha kwa lugha ya kabila la kikuyu nchini Kenya akisema.. jina langu ni Ngũgĩ wa Thion’go Profesa wa lugha ya Kiingereza na fasihi kutoka Chuo Kikuu cha California, Irvine.

Ametumia hotuba yake kwa njia ya video iliyochezwa wakati wa ufunguzi wa mkutano huo jijini New York, Marekani ikiwa na tafsiri ya maandishi ya lugha ya Kiingereza kuzungumzia umuhimu wa lugha za kiafrika katika kusongesha haki, na jinsi wenyewe waafrika wanazikana na kung’ang’ania lugha za kigeni kama vile kiingereza, kireno na kifaransa.

Anasema mimi ni mwandishi wa vitabu na nilikuwa naandika kwa lugha ya kiingereza lakini baadaye nikaona hapana nikaanza kuandika kwa lugha ya Kikuyu ambayo ni lugha mama yangu.

Ametolea mfano wa kesi iliyoendeshwa kwa lugha ambayo si mama kwa yule mtuhumiwa, na maelezo yake kutafsiriwa na mkalimani ambaye hakutoa tafsiri sahihi na kisha kuhumiwa adhabu ya kifo.

Anasema hali hii inaelezea bara la Afrika ambako watu wengi wananyimwa haki. Sheria zote ziko kwa lugha za Ulaya, hata Katiba, msingi wa sheria wa nchi uko kwa kiingereza, kifaransa au kireno.

Amestaajabishwa na viongozi wa nchi ambao hata kwenye sherehe za kitaifa huzungumza na wananchi wao kwa lugha za Ulaya.

Amehoji je umewahi kuona kwenye Umoja wa Mataifa kiongozi hata mmoja wa kiafrika akihutubia mikutano kwa lugha ya kiafrika?

Viongozi wa Ufaransa watahutubia kwa lugha ya kifaransa, Uingereza kwa kiingereza, China kwa kimandarini, Urusi kwa kirusi.

Ametamatisha hotuba yake kwa kusema kuwa haki si haki iwapo lugha inayotumika kutoa haki hiyo si lugha ya mhusika.