Watu wenye ulemavu washiriki kwenye uamuzi wa masuala yanayowahusu
Watu wenye ulemavu washiriki kwenye uamuzi wa masuala yanayowahusu
Kusongesha uongozi wa watu wenye ulemavu kwa ajili ya mustakabali jmuishi na endelevu, ndio maudhui ya siku ya leo ya kimataifa kwa ajili ya watu wenye ulemavu, wakati huu ambapo duniani kote takribani watu bilioni 1.3 wanaishi na aina mbali mbali za ulemavu.
Umoja wa Mataifa unadadavua takwimu hizo ikisema ina maana kwamba mtu 1 kati ya 6 duniani kote ana ulemavu, sawa na asilimia 16 ya wakazi wote wa dunia.
Na ni kwa kutambua takwimu na maudhui hayo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ujumbewake wa siku hii anasema vinatukumbusha “tunahitaji uongozi wa watu wenye ulemavu kuliko wakati wowote ule.”
Amesema watu wenye ulemavu tayari kwa kiwango kikubwa wanabeba mzigo wa majanga yanayotikisa dunia – kuanzia mizozo hadi majanga ya tabianchi, umaskini na ukosefu wa usawa – kwa sababu ya ubaguzi uliokomaa, unyanyapaa, vikwazo vya kupata haki za msingi na huduma.
Watu wenye ulemavu wananyimwa haki ya kutoa michango yao
Katibu Mkuu anasema pamoja na kukumbwa na changamoto hizo, bado pia wananyimwa haki ya kuwasilisha majawabu au kutoa michango yao ili kutatua majanga hayo.
Ingawa hivyo amesema suala hilo limepatiwa jawabu kupitia Mkataba wa Zama Zijazo uliopitishwa na wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa Septemba 2024 jijini New York, Marekani, mkataba ambao umeazimia kusahihisha ukosefu wa haki kwa watu wenye ulemavu wa kizazi cha sasa na vijavyo.
Mkataba uliazimia hivyo kwa kutambua dhima muhimu ya watu wenye ulemavu katika kuumba mustakabali wenye vifaa vya teknolojia vya usaidizi kama vile vinavyotumia Akili Mnemba au AI — na kisha kuchochea mabadiliko kwenye jamii na kuchechemua pia nafasi yao sahihi kwenye michakato ya kupitisha uamuzi wa masuala yanayoagusa maisha yao.
Na kwa siku zijazo, Guterres amegusia Mkutano wa Viongozi wa dunia kuhusu Maendeleo ya Kijamii ambao amesema utafanyika mwakani ukiwa ni fursa muhimu kwa kusongesha yaliyomo kwenye Mkataba wa Zama Zijazo na mengineyo.
“Katika kila jamii, watu wenye ulemavu ni waleta mabadiliko na wale amani. Wao pia ni viongozi,” amesema Katibu Mkuu akitamatisha ujumbe wake kwamba, “katika siku hii muhimu, na kila siku, hebu tufanye kazi na watu wenye ulemavu ili kufanikisha mustakabali jumuishi na endelevu kwa watu wote.”
Je wajua?
- Baadhi ya watu wenye ulemavu wanafariki dunia mapema zaidi kwa miaka 20 kuliko wale wasio na ulemavu?
- Watu wenye ulemavu wako hatarini mara mbili zaidi kupata msongo wa mawazo, pumu, kisukari, kiharusi, utipwatipwa au afya mbaya ya kinywa?
- Ukosefu wa uwiano kwenye afya kutokana na mazingira yasiyo sahihi kwa watu wenye ulemavu, ikiwemo unyanyapaa, umaskini, kutengwa kwenye elimu, ajira na vikwazo kwenye mfumo wa afya.