Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuna ongezeko la asilimia 70 la kusajili watoto kwenye vikundi vyenye silaha Haiti: UNICEF

Watoto watatu wamesimama ndani ya kibanda cha muda kilichojengwa kwa kutumia turu katika jengo la shule lililojengwa kwa sehemu huko Port-au-Prince, Haiti, wakiwa wamezungukwa na mali zao.
© UNOCHA/Giles Clarke Familia iliyopoteza makazi kufuatia migogoro inaishi katika shule kidogo iliyojengwa huko Port-au-Prince, Haiti.

Kuna ongezeko la asilimia 70 la kusajili watoto kwenye vikundi vyenye silaha Haiti: UNICEF

Amani na Usalama

Idadi ya watoto wanaoandikishwa katika makundi yenye silaha nchini Haiti imeongezeka kwa asilimia 70 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita,  limeonya leo Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF.

Ongezeko hilo ambalo halijawahi kushuhudiwa kwa mujibu wa UNICEF pia linaonyesha kuzorota kwa kiwango cha kutisha kwa ulinzi wa watoto huku kukiwa na ongezeko la vurugu katika taifa hilo la Karibea.

Makadirio ya hivi karibuni ya shirika hilo yanasema watoto sasa wanajumuisha hadi nusu ya wanachama wote wa vikundi vyenye silaha, na kuajiriwa katika vikundi hivyo kunachochewa na umaskini uliokita miziz, ukosefu wa elimu na kuporomoka kwa huduma muhimu.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell, akibainisha kuwa "Watoto nchini Haiti wamenaswa katika mzunguko mbaya na wameandikishwa katika vikundi vyenye silaha ambavyo vinazidisha hali yao ya kukata tamaa, na idadi inaendelea inaongezeka. Machafuko na vitisho vimekuwa sehemu ya maisha ya kila siku".

Wanaishi katika tishio la mara kwa mara

Taarifa ya UNICEF inasema hali katika mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince, inatisha sana, huku watoto milioni 1.2 wakiishi chini ya tishio la mara kwa mara la unyanyasaji wa kutumia silaha.

Inakadiriwa kuwa asilimia 25 ya wakimbizi wote wa ndani 703,000 ni watoto, wanaoishi katika hali mbaya na kukabiliwa na vitisho vingi.

Kudorora kwa hali ya usalama kumesababisha kuongezeka kwa kasi kwa ghasia dhidi ya watu walio hatarini zaidi wa Haiti.

UNICEF pia imeonya kwamba ukatili wa kijinsia na ubakaji umekithiri, huku ripoti za Ofisi ya Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Watoto na Migogoro ya Kivita zikionyesha ongezeko la mara kumi  zaidi la  watoto wanaokabiliwa na ukatili wa kijinsia mwaka huu pekee.

Mwaka huu, UNICEF imetoa huduma za msaada, ikiwa ni pamoja na msaada wa kisaikolojia na uhamasishaji wa jamii kwa zaidi ya watu 25,000 walioathiriwa na unyanyasaji wa kingono na kijinsia mwaka 2024.

Watoto hushiriki katika shughuli ya kisaikolojia na kielimu na UNICEF huko Port-au-Prince, Haiti.
© UNICEF/Ralph Tedy Erol Msichana wa shule huko Port-au-Prince ameinua ishara kwa Kifaransa inayosomeka "Amani".

Juhudi za ulinzi na kujikwamua

Katika kukabiliana na changamoto ya ulinzi unaowakabili watoto wanaoandikishwa na makundi yenye silaha au walio katika hatari ya kuajiriwa, UNICEF imetekeleza mipango kadhaa ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa vikosi vya usalama na mashirika ya kiraia kuhusu hatua za ulinzi wa watoto.

Pia hutoa huduma kwa wanajeshi watoto wa zamani, pamoja na msaada wa kisaikolojia na huduma za kuunganishwa ten ana familia.

UNICEF inatoa wito kwa pande zote nchini Haiti kutanguliza ulinzi wa watoto, kuunga mkono kuachiliwa mara moja kwa watoto walioajiriwa na kuhakikisha haki zao ni muhimu kwa makubaliano yoyote.

“Watoto katika sehemu nyingi za Haiti wanatendewa ukatili ambao mtoto hapaswi kamwe kutendewa,” amesisitiza Bi. Russell, akiongeza kwamba “Ukatili huo huwaacha na makovu ya kiakili na kihisia ambayo huenda yakawasumbua maisha yao yote.”