Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Marekani yatumia turufu kupinga rasimu ya azimio la Gaza la usitishaji uhasama

Naibu Mwakilishi wa Kudumu Robert A. Wood wa Marekani akiinua mkono wake kupiga kura kupinga azimio kuhusu Gaza katika chumba cha Baraza la Usalama UN .
UN Photo/Loey Felipe Naibu mwakilishiwa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Robert A. Wood akipiga kura kwenye Baraza la Usalama

Marekani yatumia turufu kupinga rasimu ya azimio la Gaza la usitishaji uhasama

Amani na Usalama

Wakati mzozo ukiendelea Mashariki ya Kati huko Gaza na Lebanon, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekukutana mjini New York hii leo kupigia kura rasimu ya azimio linalotaka usitishwaji wa mapigano wa kudumu mara moja, bila masharti na kuachiliwa huru kwa mateka wote.

Matokeo ya kura ya rasimu hiyo ya azimio ni kwamba wajumbe wote 15 wamepiga kura na 14 wameunga mkono kwa kura ya ndio, mjumbe  mmoja ambaye ni Marekani ametumia turufu kupinga kwa kupiga kura ya hapana na hakuna mjumbe aliyejizuia kupiga kura

Hamas ndio kiwazo cha muafaka wa kusitisha mapgano: Marekani

Balozi wa Mrekani kwenye Umoja wa Mataifa Robert Wood akieleza msimamo wa wajumbe wake katika kupinga rasimu ya azimio hilo amesema Hamas  ndio kiswazo inasimama katika njia ya makubaliano ya kusitisha mapigano na kwamba Marekani imekuwa ikifanya kazi kwa wiki kadhaa ili kuepuka matokeo haya.
"Tumeweka wazi wakati wote wa mazungumzo kwamba hatungeweza kuunga mkono usitishaji vita bila masharti ambalo limeshindwa kuwaachilia mateka. Azimio hili limeacha ulazima huo. Kwa sababu hiyo, Marekani haikuweza kuunga mkono."
Ameongeza kuwa azimio hilo lingetuma ujumbe wa hatari kwa Hamas kwamba hakuna haja ya kurejea kwenye meza ya mazungumzo.
Ni wakati wa vita hivi kuisha na mateka waachiliwe amesema na kuongeza kuwa na haraka zaidi Marekani imekuwa wazi kwa Israeli kwamba lazima iongeze uwasilishaji wa misaada ya kibinadamu kwa Gaza, diplomasia ya Marekani itaendelea kuhakikisha kuboreshwa kwa hali ya huko.
Balozi Wood amesisitiza kuwa “Licha ya mapendekezo ya Marekani katika mchakato mzima, baadhi ya wajumbe wa Baraza waliendelea kupanda mbegu ya  mifarakano,”
Balozi Vassily Nebenzia wa Shirikisho la Urusi akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama UN kuhusu hali katika Mashariki ya Kati.
UN Photo/Evan Schneider Balozi Vassily Nebenzia wa Urusi akizungumza kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baada ya upigaji kura kuhusu rasimu ya azimio la Gaza

Hatupaswi kushangaa : Urusi

Balozi wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa Vassily Nebenzia baada ya kura hiyo ameliambia Baraza la Usalama kwamba "inashangaza kwamba Marekani ilipiga kura ya turufu kuokoa maisha ya Wapalestina na Waisraeli, ingawa hatupaswi kushangaa."
Ameongeza kuwa "Kwa miezi kadhaa, Merika imezuia na kusimama katika njia ya hatua ya Baraza kushughulikia hali mbaya ya Gaza na kuchezea upande mmoja wa mzozo ili kuendeleza malengo yake ya kisiasa kwa kugharimu maisha ya Wapalestina".
Ameongeza kuwa, Baraza la Usalama lingekutana pamoja ili kutoa wito wa kusitishwa kwa mapigano kwa kina, ulinzi wa raia na suluhisho la matatizo ya kibinadamu yanayowakabili Wapalestina.
Lakini amesema "Marekani inadai kuwa ni kwa manufaa ya eneo hilo lakini inapiga kura dhidi ya azimio linaloungwa mkono na nchi nyingi za eneo hilo," Ameendelea kusema kwamba Baraza lingeweza kudai usitishaji vita wa mara moja, usio na masharti na endelevu huko Gaza na vile vile usitishaji wa kudumu wa mapigano na kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa mateka wote.
"Ni jambo lisiloeleweka kwamba Marekani inakuwa kikwazo katika njia ya kudai vitendo kama hivyo ili kuokoa maisha katika mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu duniani".
Balozi wa China Fu Cong akihutubia Baraza la Usalama UN wakati wa mkutano kuhusu hali ya Mashariki ya Kati.
UN Photo/Eskinder Debebe Balozi Fu Cong wa China kwenye Umoja wa Mataifa akizungumza kwenye Baraza la Usalama

Marekani inapaswa kuchukua uanachama wake wa Baraza kwa uzito: China

Balozi wa China kwenye Umoja wa Mataifa  Fu Cong kwa upande wake amesema Israel imekiuka kwa udhalili kila mstari mwekundu wa sheria za kimataifa za kibinadamu, na hata kama ni janga la njaa linaodhihirika huko Gaza, Marekani daima inaonekana kupata uhalali wa kuilinda nchi hiyo.

"Sio ajabu watu wanahisi hasira," ameliambia Baraza la Usalama.

Ameongeza kuwa Utumiaji wa kura ya turufu unaorudiwa na Marekani umepunguza mamlaka ya Baraza la Usalama na na kuzifanya sheria za kimataifa kuwa chini kabisa".

Ametoa wito kwa Marekani kuchukua uanachama wake kwenye Baraza la Usalama kwa uzito na kuunga mkono Baraza hilo kuchukua hatua zote zinazohitajika, kufikia usitishaji vita, kuokoa maisha na kurejesha amani Mashariki ya Kati.

Majed Bamya, Naibu Mwangalizi wa Kudumu wa Jimbo la Palestina, akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu hali katika Mashariki ya Kati, ikiwa ni pamoja na suala la Palestina.
UN Photo/Loey Felipe Naibu mwangalizi wa kudumu wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa Majed Bamya akizungumza wakati wa kikao cha Baraza la Usalama kuhusu rasimu ya azimio la Gaza

Usitishwaji mapigano ungeokoa maisha ya kila mtu: Palestina

Naye Naibu mwangalizi wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa Majed Bamya,  baada ya kura hiyo amesema "hakuna haki ya mauaji ya halaiki ya raia, kusababisha njaa kwa raia wote, watu kufurushwa kwa nguvu na kuwatenganisha.”

Ameongeza kuwa "Hivi ndivyo Israeli inavyofanya huko Gaza. Haya ndiyo malengo yake ya vita. Hivi ndivyo kukosekana kwa usitishaji mapigano kunairuhusu kuendelea kufanya.”

Amebainisha kuwa shambulio "kamili la Israeli dhidi ya watu wa Palestina na ardhi ya Palestina ni kuhusu kila kitu isipokuwa mateka".

Ameendelea kuhoji kuwa"Ikiwa familia ya mateka inaweza kuona hilo, mtu yeyote katika chumba hiki anawezaje kudai vinginevyo?" akibainisha kuwa kusitisha mapigano kungeruhusu kuokoa maisha na maisha yote.

Ingawa haisuluhishi kila kitu, ni hatua ya kwanza ya kusuluhisha chochote, amesema akiuliza ni jibu gani wale ambao hawataki kuitisha usitishaji vita bila masharti baada ya vifo na uharibifu wote uliofanyika hadi sasa.

Je, azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linapitishwa vipi?

Kwanza linaanza na rasimu ya awali, kisha mashauriano baadaye mjadala zaidi. Na baada ya hapo kunakuwa na rasimu zilizorekebishwa ambazo zinawekwa kwenye  ukurasa maalum ujulikanao kama "katika ukurasa wa bluu" au Whats in blue?

Kuna miongo kadhaa ya michakato ambayo mabalozi hufuata kabla ya rasimu ya azimio kuingia katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Jinsi azimio la Baraza la Usalama lilivyozaliwa

Jukumu la Baraza la Usalama lenye wanachama 15 ni kuchukua hatua kupitia maazimio na maamuzi kuhusu vitisho vyovyote dhidi ya amani na usalama wa kimataifa.

Lakini kuna vikwazo vingi vinavyoweza kuzuia kupitishwa kwa rasimu za maazimio katika hati inayofunga kisheria kwa Nchi Wanachama 193 wa Umoja wa Mataifa.