Je wafahamu madini ya kimkakati?
Je wafahamu madini ya kimkakati?
- Ni madini ya aina gani?
- Yana faida gani katika kulinda tabianchi?
- Na kwa nini yanaitwa ya kimkakati?
Mkutano wa 29 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP29 ukiendelea huko Baku, Azerbaijan, Adam Anthony, Mkurugenzi Mtendaji wa HakiRasilimali kutoka Tanzania amedadavua madini ya kimkakati ambayo yamekuwa yakitajwa sana kuwa moja ya majawabu makuu katika kuhimili na kukabili madhara ya mabadiliko ya tabianchi.
Priscilla Lecomte kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Misaada ya kibinadamu, OCHA alizungumza na Adam kando ya vikao vya Baku ambaye alianza kwa kuelezea sababu ya kuweko Baku.
“Mimi Niko hapa Baku kwa ajili ya kufuatilia zaidi mazungumzo kuhusu madini ya kimkakati au critical minerals ambayo ni muhimu sana katika kipindi hiki cha mhamo wa nishati, yaani kutoka katika nishati kisukuku au nishati chafu na kuelekea katika nishati jadidifu au renewable energy.”
Amesema madini hayo ya mkakati kwa nchi nyingi za Afrika, hususan Tanzania ni fursa ya kuweza kuhama kutoka nishati chafu na vile vile ni fursa ya kupata kipato kwa wananchi na taifa. Madini haya pamoja na manufaa yake yanakuja na changamoto nyingi za kimazingira, kiafya, haki za binadamu.
“Kwa hiyo ni muhimu sana kwa mataifa yanapokutana kwenye COP kama hii kuangalia masuala ya madini ya kimkakati, fursa bila kusahau changamoto zake,” amesema Adam.
Kipi kimemvutia zaidi kwenye mazungumzo ya madini ya kimkakati
Kilichomvutia ni yaliyomo kwenye ripoti ya jopo lililoundwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kuhusu madini ya kimkakati, ripoti iliyozinduliwa Baku.
“Ripoti imeweka misingi ya namna gani madini ya kimkakati yanaweza kupatikana, jinsi ya kutatua changamoto kwenye sekta ya madini hayo. Mathalni kuongeza thamani ya madini hayo hususan barani Afrika, na vile vile mapendekezo ya kuboresha viwanda vya kushughulikia madini hayo kule yanakochimbwa,” amesema Adam akisema matumaini yake ni kwamba mapendekezo hayo yatatekelezwa.
Je Tanzania madini ya kimkakati yapo?
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji huyo wa HakiRasilimali, Tanzania ina madini mengi ya kimakati ikiwemo ya Grafaiti yanayopatikana kusini, na Nikeli yanayopatikana kaskazini.
“Madini haya ni sehemu tu kati ya orodha kubwa ya madini ya kimkakati ambayo ni sehemu muhimu sana katika kutengeneza nishati na pia katika mapinduzi ya kidijitali,” amesema Adam.
Madini mengi ya kimkakati yanatumika katika nishati. “Kwa mfano grafaiti na nikeli ni hutumika katika betri za kuhifadhi nishati kwenye magari ya umeme. Na kwenye mapinduzi ya kidijitali ni madini mengine kama kobalti ambayo hutumika kwenye teknolojia ya simu.
Alipoulizwa kuhusu Tanzania kutumia madini hayo ya kimkakati kutengeneza simu inawezekana, Adam amesema, “kwenye mkutano kama huu ndio utaweza kuangalia nchi za Afrika zenye amdini kama haya zinawezaje kuongeza thamani badala ya kusafirisha tu malighafi.”