Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano kati ya IDF na Hezbollah ‘yakipamba moto’ madhara ni pande zote - UNIFIL

Mlinda amani UN kutoka Serbia anaangalia kupitia darubini kutoka kwenye mnara wa ulinzi huko Naqoura, Lebanon.
© UNIFIL/Haidar Fahs Kikosi cha Muda cha walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon (UNIFIL) kinashikilia nyadhifa zake kusini, ambako ghasia zinaongezeka.

Mapigano kati ya IDF na Hezbollah ‘yakipamba moto’ madhara ni pande zote - UNIFIL

Amani na Usalama

Mapigano kati ya jeshi la Israeli, IDF na wapiganaji wa Hezbollah ndani ya Lebanon yanazidi kushamiri na kuleta madhara zaidi, umesema Ujumbe wa  Umoja wa Mataifa wa kikosi cha mpito nchini Lebanon, UNIFIL.

Mapigano kati ya pande mbili hizo yalianza Oktoba 8, mwaka 2023.

Andrea Tenenti, ambaye ni msemaji wa UNIFIL akizungumza kutoka mji mkuu wa Lebanon, Beirut hii leo amewaambia waandishi wa habari wa Geneva, Uswisi kwamba makabiliano yameendelea kati ya pande mbili hizo kwenye eneo linalodhibitiwa na UNIFIL ambalo halipaswi kuwa na mapigano.

“Mashambulizi  ya angani kila siku nchini Lebanon kutoka Israeli, na makombora pamoja na droni kutoka Hezbollah kwenda Israeli yamesababisha uharibifu wa vijiji na miji katika pande zote za eneo lisilopaswa kuwa na mapigano,” amesema Tenenti.

Wito wa sitisho la mapigano wapuuzwa

Amesema wakati idadi ya vifo kutokana na mzozo huo ikiwa isiyofikirika, wito wa kimataifa wa sitisho la mapigano kwa bahati mbaya umekuwa hausikilizwi.

Ijapokuwa majukumu ya UNIFIL kwa mujibu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, yamekumbwa na changamoto kubwa ikiwemo kushambuliwa kwa miundombinu yake, “majukumu ya msingi kama vile usalama, ulinzi na kusaka amani ya kudumu, bado yameendelea kuwa na umuhimu,” amesema Tenenti.

“Msimamo wa zaidi  ya walinda amani 10,000 kutoka takribani nchi 50 haujabadilika tangu Septemba 23,” amesema Tenenti, akiongeza kuwa “wote wamesalia kwenye maeneo 50 kwenye maeneo  yote ya operesheni, wakifuatilia na kutoa taarifa kuhusu kinachoendelea kwenye maeneo yao.”

Wakimbizi wamepumzika kwenye matandiko ya muda katika hema linaloangalia bahari nchini Lebanon.
© UNICEF/UNI658595/Dar al Mussawir/Ramzi Haidar Makumi ya maelfu ya familia za Lebanon zimekimbilia usalama na makazi salama kutokana na mashambulizi ya anga ya mara kwa mara ya Israel.

Mustakabali wa watoto mashakani – UNICEF

Kuzidi kushamiri kwa mapigano nchini Lebanon kati ya jeshi la Israeli na wanamgambo wa Hezbollah, ‘kumehalalisha ukimya wa kihoro’ kinachopata watoto nchini humo kama ilivyo Ukanda wa Gaza, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudimia watoto, UNICEF.

Kwa wastani, watoto watatu wamekuwa wanauawa kila siku katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, amesema James Elderl msemaji wa UNICEF akizungumza na waandishi wa habari hii leo huko Geneva, Uswisi.

Mamia ya maelfu ya watu wamelazimika kukimbia makazi yao huku makombora ya Israeli yakizidi kumiminika; idadi kubwa ya makombora imepiga miundombinu ambayo watoto wanategemea, kama vile vituo vya afya.

“Tunapaswa kutumainia kuwa utu katu hautoachia kiwango cha ukatili kwa watoto kama Gaza, ijapokuwa tunaona hali inafanana Lebanon,” amesema Elder.

Wanatusaidia kupata furaha hapa lakini twataka kurejea nyumbani- Joud
Tweet URL

Kutana na Joud, mtoto mwenye umri wa miaka 12 ambaye ni miongoni mwa watu 878,00 waliofurushwa makwao huko Lebanon kufuatia mapigano kati ya jeshi la Israeli na wanamgambo wa Hezbollah. Mapigano hayo yalianza Oktoba 8 mwaka 2023.

Kupitia video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA, iliyochapishwa kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X, Joud anasema, “jina langu ni Joud, nina umri wa miaka 12. Tulikuwa nyumbani na kisha tukakimbilia shuleni. Nimekuja hapa na nimekutana na watoto wa umri wangu. Tumefahamiana, tukaanza kucheza soka, tunacheza mpira, tunacheza michezo yote.”

Joud anasema walianza kuongea na kubadilishana simulizi mbalimbali na  hata kukumbushana mambo ya zamani walipokuwa watoto.

“Shuleni kuna watu wanakuja na kupanga mambo mbalimbali kwa ajili yetu. Wanatusaidia kukumbuka raha ya kucheza soka na mambo mazuri kabla ya vita. Tuna furaha hapa lakini tunatamani kurejea nyumbani,” amesema Joud.

UNRWA inatoa misaada kwa familia zilizoko katika vituo 11 vya dharura nchini kote Lebanon.