Majaribio ya kufikisha misaada Gaza Kaskazini ‘yagonga mwamba’
Majaribio ya kufikisha misaada Gaza Kaskazini ‘yagonga mwamba’
Operesheni nzito ya jeshi la Israeli imeendelea huko Ukanda wa Gaza huku wahudumu wa Umoja wa Mataifa wa kibinadamu wakiripoti kuwa majaribio kadhaa ya kufikisha misaada ya kuokoa maisha kwenye eneo hilo la kaskazini lililozingirwa ‘yamegonga mwamba.’
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA, imesema wahudumu wa kibinadamu wamekataliwa au wamezuiwa kuingia.
“Katika siku mbili zilizopita, majaribio sita ya kufikisha misaada ya kuokoa maisha Gaza Kaskazini hayakufanikiwa,” imesema OCHA.
Majaribio hayo yalifanyika Jumanne na Jumatano wiki hii kwa lengo la kufikisha chakula na maji huko Jabalia, Beit Hanoun na Beit Lahiya, sambamba na misaada ya usaidizi wa kisaikolojia na kijami kwa watoto waliokumbwa na kiwewe kutokana na vita hiyo iliyodumu miezi 13 sasa.
“Watu wamenasa kwenye majengo ya makazi ya watu, wanajificha kutokana na operesheni ya kijeshi inayoendelea, “tunaishiwa chakula,” amesema Louise Wateridge, Afisa Mwandamizi wa UNRWA, ambalo ni shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina.
Akizungumza na waandish wa habari, Bi. Wateridge amenukuu shuhuda za wafanyakazi wa OCHA na watu wanaoishi eneo la kaskazini wakielezea “kuona maiti wengi wametapakaa mitaani na eneo karibu na hospitali ya kutoa huduma za afya.”
Takribani watu wote walilazimishwa kuhama
Kwa mujibu wa OCHA, takribani asilimia 79 ya Ukanda wa Gaza, uko kwenye eneo la kupatiwa amri mara kwa mara.
“Wapalestina wanaendelea kuelekezwa kwenda maeneo yaliyo ndani mwa Al Mawasi kusini mwa Gaza na viunga vyake, maeneo ambayo hayana miundombinu ya msingi na huduma muhimu,” imesema OCHA.