Gharama ya ulacho ni zaidi ya bei ulipayo – FAO
Gharama ya ulacho ni zaidi ya bei ulipayo – FAO
Taarifa hizo zinatokana na ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO ikipatiwa jina Hali ya Chakula na Kilimo au SOFA, ripoti ikitaja gharama hizo kuwa ni za kiuchumi, kijamii na kimazingira na zinafikia dola trilioni 12 kwa mwaka.
Utajiuliza pengine mbona ni kawaida? La hasha! FAO imefanya uchambuzi wa kina na kubaini kuwa ingawa mifumo ya uzalishaji wa chakula, yaani kilimo cha mazao, husaidia kufikishia watu chakula na vile vile wengine kujipatia kipato kwa kushiriki kwenye uzalishaji chakula, baadhi imekuwa na gharama hizo zisizoonekana.
Mathalani, uharibifu wa mazingira kutokana na kilimo cha mazao ya chakula; mtu kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi kutokana na lishe duni; madhara ya kijamii yanayohusishwa na umaskini au kutokula chakula cha kutosha.
Aina 6 za mifumo ya uzalishaji chakula
Ili kudadavua vema gharama hizo, FAO imegawanya mifumo ya uzalishaji wa chakula katika makundi sita: mizozo; kijadi; ukuao;tofauti; rasimishwa na viwanda.
FAO inasema kadri nchi zinavyosonga mbele kutimiza ahadi zao za kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs, mifumo yao ya uzalishaji wa chakula ina uwezo mkubwa wa kubadilika na kuwa ya viwanda, badala ya kutumia jembe la mkono.
Mathalani, kwenye mifumo takribani yote ya uzalishaji chakula, mlo wenye kiwango kidogo cha nafaka nzima ni kichocheo cha lishe duni.
Hata hivyo katika maeneo ya mizozo ya muda mrefu, inayogubikwa na ukosefu wa uhakika wa chakula, na kwenye mfumo wa kijadi unaogubikwa na uzalishaji na teknolojia kidogo na mnyororo mdogo wa thamani wa vyakula, hofu kubwa hapo ni ulaji wa kiwango kidogo cha matunda na mboga za majani.
Nyama nyekundu, nyama zilizosindikwa na kutokula matunda ni tatizo
Gharama za kimazingira, kiuchumi, kijamii na kiafya hazionekani kwenye bei inayolipwa na mtu kununua chakula, na hutofautiana kulingana na eneo ambalo mtu anaishi.
Kwa mfano mifumo ya kuzalisha chakula kwenye maeneo ya mizozo iliyodumu muda mrefu inakuwa na gharama kubwa ukilinganisha na uwezo wao kiuchumi, ikigubikwa na gharama kubwa za kimazingira kama vile uharibifu wa mazingira na gharama za kijamii zilizofichika.
Hata hivyo katika mifumo mingi ya kuzalisha chakula, gharama kubwa iliyofichika ni ile itokanayo na mienendo ya ulaji isiyo ya kiafya Kutokula nafaka zisizosindikwa, matunda, mboga za majani; ulaji wa kupitiliza wa chumvi, nyama nyekundu na nyama iliyosindikwa.
Nini kifanyike?
FAO inasema mifumo inapaswa iboreshwe majawabu yakizingatia mazingira ya kila jamii husika.
Kigezo kikubwa duniani cha gharama zilizofichika kwenye ulaji ni ulaji mdogo wa nafaka na matunda, na ulaji wa chumvi kwa kiwango cha juu.
FAO inasema kila mtu ana jukumu katika kuboresha mifumo ya uzalishaji chakula ambapo Mkurugenzi wake Mkuu QU Dongyu anasema, “chaguo tunalofanya sasa, vipaumbele tunavyoweka na majawabu tunayotekeleza yataamua mustakabali wetu wa pamoja.”
Kwa kutumia mbinu bora za kilimo, kipato cha kutosha kwa wafanyakazi kwenye sekta hiyo na kuchagua chakula chenye lishe kulinga na eneo la kila jamii, kunaweza kufanya sayari kuwa bora halikadhalika watu wanaoishi ndani yake.