Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viwango vya joto duniani vyazidi kuongezeka na kuelekea kuvunja rekodi - WMO

Wenzi wa ndoa wanatembea kwenye bandari ya mbao wakati wa machweo ya jua katika Visiwa vya Maldives.
© Unsplash/Ishan @seefromthesk 2024 imeshuhudia mawimbi ya joto yaliyovunja rekodi.

Viwango vya joto duniani vyazidi kuongezeka na kuelekea kuvunja rekodi - WMO

Tabianchi na mazingira

Mwaka 2024  unaelekea kuvunja rekodi na kuwa mwaka wenye kiwango cha juu zaidi cha joto, ambapo wastani wa kiwango cha joto la ardhi ni kikubwa kuliko mwaka 2023, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa, WMO.

WMO imesema hayo katika uchambuzi wake wa viwango vya joto kuanzia mwezi Januari hadi Septemba mwaka huu, uchambuzi ambao shirika hilo limempatia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, kabla ya mkutano wa 29 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabainchi, COP29 huko Baku, Azerbaijan.

Taarifa hizo zinatokana na takwimu kutoka vituo sita vya kimataifa vya kufuatilia tabianchi na viwango vya joto ambapo Guterres amesema “WMO na wadau wametoa taarifa ya kwamba 2024 unaelekea kuwa mwaka wenye joto zaidi, ikiwa imesalia miezi miwili kumalizika.

“Ubinadamu  unateketeza sayari na  unalipia gharama,” amesema Katibu Mkuu baada ya kupokea taarifa hiyo, ambayo kwa kina itatolewa na WMO katika Ripoti ya Tabianchi Duniani mwaka 2024 huko COP29.

Ripoti itamulika viashiria muhimu ikiwemo wastani wa joto la ardhini, joto baharini, ongezeko la kina cha bahari, theluji baharini na barafu za ncha za dunia.

Itatoa pia taarifa kuhusu hali mbaya za hewa za kupitiliza na matukio ya tabianchi yenye madhara kwa maendeleo endelevu.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka taasisi ya kufuatilia tabianchi Ulaya, au Copernicus Climate Change Service, Oktoba 2024 ulikuwa ni mwezi wa pili wa Oktoba kwa kuwa na joto kali zaidi, baada ya Oktoba 2023. Taarifa kutoka fungu lingine la takwimu zitatolewa kadri muda unavyosonga.