Nini kifanyike nchi zenye maendeleo duni zinufaike na biashara ya hewa ya ukaa?
Nini kifanyike nchi zenye maendeleo duni zinufaike na biashara ya hewa ya ukaa?
Nchi zenye maendeleo duni, LDCs, zinaweza kutumia miradi ya soko la biashara ya hewa ya ukaa ili kuchochea harakati zao za maendeleo. Hata hivyo miradi hiyo inaweza kuwa na manufaa iwapo itasimamiwa vizuri, imesema Ripoti mpya ya LDCs kwa mwaka 2024, iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo, UNCTAD.
Ripoti hiyo imetolewa Geneva, USwisi hii leo ikisema kuwa biashara ya hewa ya ukaa inaweza pia kuchangia katika harakati za dunia za kutozalisha kabisa hewa ya ukaa na hivyo kuwa ni hatua dhidi ya tabianchi.
Soko la hewa ya ukaa ni nini?
UNCTAD inasema soko la hewa ya ukaa ni majukwaa ambamo kwamo kiwango cha utoaji wa chafuzi kinauzwa na wengine wananunua. Nchi zinazouza zinakuwa zimetenga maeneo ya misitu ambako hakuna uchafuzi unafanyika na kisha wale wanaotoa hewa chafuzi wanazipatia nchi hizo fedha na hivyo kupunguza kiwango cha utoaji hewa chafuzi,
“Kwa kushiriki kwenye masoko hayo, nchi zinazouza zinaweza kujipatia mapato na kuchangia katika hatua kwa tabianchi na hivyo kuondoa uchafuzi kutoka kwa wanunuzi.”
Washiriki wa mapema, lakini bila faida
LDCs zilikuwa miongoni mwa nchi za kwanza kujiunga na soko la hewa ya ukaa, lakini kwa sasa zimekuwa na ushawishi mdogo kutokana na kiwango kidogo cha uchumi wao wa changamoto za miundombinu, teknolojia na uwezo wa kitaasisi.
Kuwekeza katika maeneo kama vile kufuatilia na kutoa ripoti kunahitaji uwekezaji wa mapema, lakini kunaweza kuongeza ushiriki na faida.
Hadi sasa ni nchi sita tu za LDCs - Bangladesh, Cambodia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Malawi, Uganda, na Zambia – ndio zinachangia zaidi ya asilimia 75 ya biashara yote ya ukaa kupitia masoko ya hiari, na asilimia 80 ya biashara ya ukaa chini ya Ifitaki ya Kyoto ya Mfumo wa Maendeleo Safi, CDM.
Ijapokuwa LDCs ni asilimia 1.5 ya miradi ya CDM, hii inaonesha fursa kubwa ya kuongeza ushiriki wao na kuanzisha masoko jumuishi zaidi ya yanayoweza kunufaisha LDCs.
Mwaka 2023, thamani ya soko la biashara ya hewa ya ukaa kutoka LDCs ilifikia dola milioni 403, ambayo ni asilimia 1 tu ya misaada ya maendeleo kutoka nchi moja kwenye nchi nyingine.
UNCTAD inasema soko la biashara ya hewa ya ukaa haliwezi kufanikisha LDCs kutimiza Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs, lakini si haba linaweza kuchochea kusongesha mbele.
Mapendekezo ya UNCTAD
- Kuimarisha mifumo y anchi kwa kujenga uwezo na kutekeleza mifumo ya ufuatiliaji na kuripoti, na kuhakikisha jamii zinanufaika na miradi ya uuzaji wa hewa ya ukaa
- Kupanua ubia wa kimataifa kwa kuunda taasisi za kikanda ili kupunguza gharama na kuboresha masoko, mathalani baina ya nchi za kusini.
- Kupatia kipaumbele kujengea uwezo, kupitia ufadhili kutoka wadau wa maendeleo. Nchi ziweze kujumuisha soko la hewa ya ukaa kwenye sera ikiwa na malengo ya kuboresha na kufanyia marekebisho uchumi.