Jukwaa la miji duniani (WUF12) linang’oa nanga leo Cairo
Kadri kasi ya watu kuhamia miji mikubwa inavyoongezeka, tunaweza vipi kuhakikisha kuwa mazingira katika miji hiyo ni endelevu na salama kwa raia? Maswali hayo na mengine mengi yatapatiwa majibu katika mkutano wa 12 wa Jukwaa la Miji Duniani linaloanza leo huko Cairo, nchini Misri.
Jukwaa la Miji Duniani ni nini?
Jukwaa la Miji Duniani, au World Urban Forum (WUF) kwa lugha ya kiingereza, ni mkutano mkubwa wa Umoja wa Mataifa kuhusu maendeleo endelevu ya miji, na lilianzishwa mwaka 2001 kutatua changamoto ukuaji wa miji duniani, moja ya masuala makubwa yanayosababisha changamoto duniani hivi sasa. Tangu wakati huo, jukwaa hilo limekuwa likifanyika kila baada ya miaka miwili, na mwaka huu linafanyika mji mkuu wa Misri, Cairo kuanzia tarehe 4 hadi 8 Novemba.
Tangu mwanzo, jukwaa hilo limesaidia shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi, UN-Habitat, kukusanya taarifa kuhusu masuala na mienendo na kujenga ubia ili kusaidia kazi yake na kupata majawabu juu ya janga la makazi na majanga mengine yanayohusiana kama vile mabadiliko ya tabianchi, vita na umaskini.
Kwa nini ni muhimu?
Leo hii, takribani asilimia 50 ya wakazi wa dunia wanaishi mijini, na idadi hii inatarajiwa kuongezeka hadi asilimia 70 ifikapo mwaka 2050. Kitendo cha watu kuhamia katika vitovu vya miji kina madhara makubwa kwa jamii, majiji, uchumi, mabadiliko ya tabianchi na sera.
Ukuaji huo kwa kiasi kikubwa utafanyika Afrika, ambako idadi ya watu inatarajiwa kuongezeka maradufu katika miaka 30 ijayo.
Cairo, sambamba na miji mingine mingi ya Afrika, unaweza kuw amoja ya vitovu vikubwa zaidi duniani , ukiwa na zaidi ya watu milioni 10 ifikapo mwaka 2035.
“Naona WUF kama ubia mkubwa wa kusaidia mabadiliko yenye marekebisho,” amesema Anacláudia Rossbach, Mkurugenzi Mtendaji wa UN-Habitat akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa.
“Lengo lake ni kusongesha ushirikiano na ubia kati ya wale wanaohusika na kusongesha na kutekeleza maendeleo endelevu ya miji.”
Maudhui ya WUF12 ni nini?
Maudhui ya WUF12 ni Inaanzia nyumbani:Hatua za kijamii kwa miji na jamii endelevu. Maudhui haya yanasisitiza kuwa majawabu ya changamoto lazima yaanzie pale ambako watu wanaishi, wanafanya kazi na wanajenga maishayao.
Kutakuweko na msisitizo katika majawabu ya kijamii kutatua janga la makazi duniani, janga ambalo linachochewa zaidi na mabadiliko ya tabianchi na kuongezeka kwa ukosefu wa usawa.
“Kwa kusogeza mjadala karibu na nyumbani na kujikita katika hatua za kijamii, tunalenga kutafsiri kivitendo malengo ya dunia ili yaweze kuwa na mabadiliko au mchango kwa jamii,” amesema Bi. Rossbach.
Amesema WUF12 itakuwa jukwaa la kujadili na kujifunza kutokana na mipango ya mafanikio ya jamii, na kuhakikisha maendeleo katika mji mmoja yanaweza kujenga hamasa kwa juhudi kama hizo katika miji mingine.
Washiriki pia watajifunza kuhusu mbinu mbali mbali za wapanga miji na mamlaka, mathalani kuendeleza maeneo ya kijani au yenye miti na bustani na misitu ya mijini, ambayo inasaidia kupunguza madhara ya joto mijini yatokanayo na ujenzi wa majengo marefu yanayotumia viyoyozi. Hii itasaidia kupunguza joto na kuimarisha bayonuai.
Nini kitafuatia?
Matokeo makubwa yanayotarajiwa kutokana na mkutano huo kwa Cairo, ni kupatia nguvu mpya Al Asmarat, kitongoji cha watu wa kipato cha chini mjini humo. Mpango huo, kwa kushirikiana na Gavana wa Cairo, ni sehemu ya mpango wa kubadili mji huo kuwa kielelezo cha ukuaji endelevu wa miji.
“Mpango huu ni kielelezo cha iman iyetu kwamba kila mji, kila jamii, na kila mkazi ana wajibu wa kutekeleza katika kujenga mustakabali bora,” amesema Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UN-Habitat.
Shirika hilo litaendelea kushirikiana na mamlaka za mitaa na kuchochea wanaharakati wa miradi ya mijini ambayo inabadili maisha ya watu.
Mathalani, Kibera, makazi duni kwenye mji mkuu wa Kenya, Nairobi, ambako UN-Habitat inashirikiana na mashirika ya mashinani kuimarisha mto Ngong na kuboresha mazingira ya jamii za eneo hilo.
Naweza kupata wapi taarifa zaidi?
Programu nzima ya mkutano iinapatikana hapa.
Unaweza kufuatilia pia matangazo na habari zetu kutoka WUF Cairo ambao mwandishi wetu wa habari amepiga kambi kukuletea kila kinachoendelea.