UNIFIL inasalia Lebanon na kuendelea na majukumu yake licha ya changamoto: Lacroix
UNIFIL inasalia Lebanon na kuendelea na majukumu yake licha ya changamoto: Lacroix
Amani na Usalama
Mkuu wa operesheni za amani za Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix leo Novemba Mosi amesema “walinda amani katika Kikosi cha Muda cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon UNIFIL) wanasalian nchini humo, wanashikilia mstari wa blu na wameazimia kuendelea kufanya kile ambacho wameagizwa kufanya Lebanon."
Katika mahojiano maalum na Mkurugenzi wa Idara ya Habari na vyombo vya habari wa Umoja wa Mataifa, Ian Phillips, Bwana Lacroix amesema ni "wakati muafaka wa kusitisha mapigano nchini Lebanon” lakini amekiri kwamba "bado tunafuatilia taarifa za hivi karibuni kutoka kwa pande tofauti."
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kwamba kwamba UNIFIL ina uungwaji mkono mkubwa wa nchi wanachama.
UNIFIL haiondoki Lebanon
Licha ya ombi la hivi karibuni kabisa la mamlaka ya Israel kwa askari wa kulinda amani wa UNIFIL likiwataka kuondoka kilomita tano kutoka kwenye msitari tenganishi wa blu au Blue Line, Lacroix amesema, "tulifanya uamuzi uliotathiminiwa sana kwamba ilikuwa muhimu kusalia, kwanza kabisa, kwa sababu kuna agizo, na sisi ni lazima tuwajibike kwa mamlaka ya taifa hilo. Walinzi wa amani wanahitaji kubaki. Pili, kwa sababu tulifikiri kwamba ikiwa vituo hivyo kando ya Mstari wa Bluu vitaachwa, basi vingeweza kukaliwa na chama kimoja au kingine. Na hiyo itakuwa mbaya sana kwa sababu nyingi, ikiwa ni pamoja na mtazamo wa Umoja wa Mataifa wa kutopendelea na kutoegemea upande wowote.”
Mkuu huyo wa ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa UNIFIL ina wanajeshi kutoka zaidi ya nchi 40 wanaochangia vikosi vya ulinzi wa amani kutoka mabara yote na wote wamejitolea sana kwa mamlaka yao, kwa wajibu wao. Jukumu lao ni kweli kuunga mkono utekelezaji wa suluhu ya kisiasa."
Mashambulizi dhidi ya walinda amani hayakubaliki
Lacroix amesisitiza kuwa “mashambulizi dhidi ya walinda amani hayakubaliki, ni ukiukaji wa sheria za kimataifa. Na, unajua, tumekuwa tukizikumbusha pande zote wajibu wao wa kulinda walinda amani, ulinzi na usalama wa walinda amani sio chaguo ni wajibu.”
Wanajeshi wanane wa kulinda amani wa UNIFIL wamejeruhiwa tangu kuanza kwa operesheni za Israel nchini Lebanon.
Lacroix amesema, "Nadhani tumeona taarifa hii kuhusu jukumu la UNIFIL. Na nadhani baadhi yake, yaani baadhi ya taarifa hizo potofu zinaelekea kupendekeza kwamba, jukumu la UNIFIL lilikuwa kutekeleza suluhu ya kisiasa, lilikuwa hata kutekeleza azimio 1701 linalosisitizwa na Baraza la Usalama. Kwa hakika sivyo ilivyo. Kuna mengi ambayo UNIFIL inaweza kufanya, na imefanya, na itafanya ikiwa kutakuwa na usitishaji wa mapigano katika suala la kuunga mkono pande zote na ni kwa ajili yao. Ni kwa ajili ya pande hizo, lazima kuwe na utashi wa kisiasa kutoka kwa pande hizo ili kutekeleza suluhu ya kisiasa, kutekeleza kipengele cha Azimio 1701 lililopitishwa kwa kauli moja mwaka 2006, madhumuni ya azimio nambari 1701 yanaendelea kuwa ni juu ya kumaliza uhasama kati ya Hezbollah na Israel, huku Baraza likitoa wito wa usitishaji wa kudumu wa mapigano kwa msingi wa kuundwa kwa eneo la usalama.
Ameendelea kusema kwamba kwa azimio hilo, Baraza liliamua kuchukua hatua za kuhakikisha amani, miongoni mwao kwa kuidhinisha ongezeko la uwezo wa kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon UNIFIL hadi kufikia wanajeshi 15,000 ambao, pamoja na mambo mengine, watafuatilia kusitishwa kwa mapigano, kuunga mkono majeshi ya Lebanon wakati Israel inajiondoa kutoka kusini mwa Lebanon na kuhakikisha kuwa watu waliokimbia makazi yao wanarejea salama.