Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana wachochee hatua kwa tabianchi na uendelevu wa miji – Guterres

Bustani ya kijani kibichi katika miji inachagiza matokeo chanya kwa bioanuwai, hali ya hewa, ustawi na ubora wa hewa.
© Unsplash/Nerea Martí Sesarin
Bustani ya kijani kibichi katika miji inachagiza matokeo chanya kwa bioanuwai, hali ya hewa, ustawi na ubora wa hewa.

Vijana wachochee hatua kwa tabianchi na uendelevu wa miji – Guterres

Tabianchi na mazingira

Ikiwa leo tarehe 31 Oktoba ni siku ya miji duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametumia ujumbe wake wa siku hii kusisitiza nafasi muhimu ya vijana katika kuchochea hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kuunda mustakabali endelevu kwa miji kote duniani.

Guterres amesema mchango wa vijana ni wa kipekee katika kukabiliana na changamoto za tabianchi zinazoukumba ulimwengu, hasa mijini ambako ni makazi ya zaidi ya nusu ya wakazi wote duniani na pia chanzo cha asilimia 70 ya gesi chafuzi kwa mazingira.

“Hii inadhihirisha jinsi miji ilivyo katika mstari wa mbele wa janga la tabianchi, ikihitaji nguvu na maono ya vijana katika kuleta mabadiliko yanayohitajika,” amesema Guterres.

Amesema  vijana wamekuwa wakiongoza njia kupitia harakati za kijamii na uvumbuzi wa kiteknolojia, wakishinikiza matumizi ya nishati mbadala, ajira rafiki kwa mazingira, usafiri wa umma usio na uchafuzi, na hatua za kuhimili mabadiliko ya tabianchi.

Sauti za vijana zisikilizwe

“Juhudi hizi zimekuwa muhimu katika kufanikisha miji endelevu ambayo inaweza kuwahudumia watu wote, hasa katika mazingira yanayokumbwa na athari za tabianchi,” amesema Guterres.

Katibu Mkuu amesema ni muhimu kuwekeza katika mawazo ya vijana na kutoa nafasi kwa mawazo yao katika maamuzi yanayohusu mustakabali wa miji.

“Kwa kuwawezesha vijana, tunaweza kuharakisha hatua za tabianchi na kuimarisha maendeleo endelevu,” ameeleza.

Wito wa Katibu Mkuu

Kwa mantiki hiyo ametaka kushirikiana na vijana, kuwasaidia na kuwapa fursa za kubuni majawabu rafiki kwa mazingira ili kutatua changamoto za miji.  

Kwa kufanya hivyo, amesema, ulimwengu unaweza kuhakikisha miji inakuwa na ustahimilivu wa kukabiliana na changamoto za tabianchi na kuyafikia Malengo ya Maendeleo Endelevu.

“Tunapoadhimisha siku ya miji duniani, hebu na tusherehehee uthabiti wa vijana katika kujenga miji inayojali mazingira, yenye mnepo na jumuishi inayokidhi mahitaji na matamanio ya vizazi vijavyo,” ametamatisha Katibu Mkuu.