Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yatoa tahadhari kuhusu kuendelea kwa viwango vya juu vya njaa DRC

Mwanamke aliyevaa gauni lenye muundo wa njano na bluu akitunza bustani ya mboga katika shamba huko Tshikapa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
© FAO/Junior D. Kannah Mkulima nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo., ambapo ukosefu wa uhakika wa chakula umeathiri watu wengi.

FAO yatoa tahadhari kuhusu kuendelea kwa viwango vya juu vya njaa DRC

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa ya chakula na kilimo (FAO) limeonya kuhusu hali ya uhakika wa chakula nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambapo takribani robo ya wananchi wanakabiliwa na ukosefu wa chakula uliokithiri. Kwa mujibu wa ripoti mpya ya tathmini jumuishi ya usalama wa chakula (IPC) iliyotolewa leo, kati ya Julai na Desemba 2024, watu milioni 25.6 wanakabiliwa na njaa kali (IPC Awamu ya 3 au zaidi), huku milioni 3.1 wakiwa katika hatari kubwa (IPC Awamu ya 4).

Mkurugenzi wa Ofisi ya dharura na ustahimilivu ya FAO, Rein Paulsen, amesema hali hiyo inatokana na ghasia za silaha na ushindani wa rasilimali, ambavyo vimesababisha madhara makubwa kwa maisha vijijini na kuzorotesha uzalishaji wa kilimo.

"Hali hii inahitaji hatua za haraka ili kumaliza mapigano, kurejesha uzalishaji wa chakula na kusaidia familia za vijijini kujijengea ustahimilivu na kuboresha uzalishaji," amesema Paulsen.

FAO inatoa msaada kwa familia zilizoathiriwa na mizozo mashariki mwa DRC kwa lengo la kuboresha usalama wa chakula na lishe. Shirika hilo linasaidia wakimbizi wa ndani, waliorejea na jamii zinazokaribisha kwa kuwapatia msaada wa haraka na kuwasaidia kujikimu. Hii ni pamoja na usambazaji wa pembejeo za kilimo kama mbegu za mboga na zana ili kuanzisha tena uzalishaji wa kilimo.

Katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri, FAO inaendelea kusaidia kaya 25,000 zilizo hatarini, sawa na watu 150,000, kupitia mpango wa Cash+, ambao unajumuisha fedha taslimu na pembejeo za bustani ndogo au mifugo. Mgao wa fedha katika Kivu Kaskazini unawasaidia wakimbizi wa ndani kukidhi mahitaji yao ya chakula na huduma za msingi.

Kuanzia Novemba, familia hizo zitanufaika na mbegu za mboga, zana, na mafunzo pamoja na vifaa vya ulinzi wa afya ya mifugo na kampeni za chanjo. Hatua hizi zinalenga kuboresha afya ya mifugo na uzalishaji wa chakula ili familia ziweze kujitegemea. FAO imeeleza kuwa msaada wa haraka unahitajika ili kuzuia athari zaidi na kupunguza kasi ya kuenea kwa njaa.