Maharagwe ya Guajiro yenye mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ni lulu kwa jamii ya Wayúu
Maharagwe ya Guajiro yenye mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ni lulu kwa jamii ya Wayúu
Mabadiliko ya tabianchi yanapoendela kujadiliwa nchini Colombia, aina ya maharagwe yenye ladha nzuri na stahimilivu ambayo imekuwepo kwa karne nyingi inaweza kuwa jawabu kwa watu wa jamii ya asili ya Wayúu nchini Colombia.
Hakuna neno la mabadiliko ya tabianchi katika lugha ya Wayunaikki, lugha ya watu wa asili wa Wayúu wa Amerika Kusini, lakini tangu mgogoro huo uanze kuathiri jamii zao, huenda sasa wamepata ufunguo wa mnepo ambao ni maharagwe ya kawaida.
Wakati COP16 inakamilisha mkutano wake wa kimataifa wa bioanuwai nchini Colombia wiki hii, tunakuleta kwenye mstari wa mbele wa mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, ambapo kwa karne nyingi Wayúu wameweza kukabiliana na changamoto katika mojawapo ya mazingira magumu zaidi duniani.
Pale maarifa ya jadi yanapokutana na bioanuwai ya kilimo au kwa kimombo agrobiodiversity, neno linalomaanisha kufuata kanuni za kilimo zinazohifadhi na kurutubisha mazingira huku zikichangia mnepo wa muda mrefu na uhakika wa chakula, suluhu ya kipekee inajitokeza ni aina ya kipekee ya maharagwe ya kapeshuna, yanayojulikana zaidi kama maharagwe ya Guajiro.
“Maharagwe ya Guajiro yana mnepo kama walivyo watu wa Wayúu,” anasema Manuel Montiel, kutoka kijiji cha Ipasharrain katikati ya La Guajira, Colombia. “Kwa mfano yanakuwa imara zaidi unapoyakanyaga.”
Kiungo muhimu cha jadi
Nyumbani kwa zaidi ya watu 600,000, La Guajira ni ardhi ya asili ya Wayúu, ikiwa na eneo la karibu kilomita za mraba 21,000 kupitia misitu mikavu na michanga jangwani katika sehemu ya kaskazini kabisa ya bara hilo la Amerika Kusini inayopakana na Colombia na Venezuela. Pia ni mahali ambapo pana ugumu wa kukuza chakula katikati ya ukame, mafuriko, jua kali, upepo mkali, mvua chache, na joto linalosalia kati ya nyuzi joto 35°C na 40°C mwaka mzima.
Huku akitembea kwenye uwanja wenye majani ya kijani kibichi huko Ipasharrain, Bwana Montiel anakanyaga kwa ujasiri mimea yenye nyuzi za kijani, kahawia na zambarau, na kusimama kuchuma kwa uangalifu maharagwe ambayo aliwapa dada yake, mkewe na binti yake, ambao pamoja na wanawake wengine wanandaa mlo unaotumia mbegu hizi za hali ya juu kama kiungo muhimu zaidi.
Kama kitafunio, chakula kikuu au kichocheo, maharagwe ya Guajiro yanaridhisha. Wakati wakishiriki mapishi wakiwa katika jiko la pamoja la Ipasharrain, Ana Griselda Gonzalez anasema kwamba maharagwe haya yanaweza kuliwa kwa njia nyingi, ikiwa ni pamoja na kuliwa kama yalivyo au katika vyakula kama shapulana, supu yenye ladha nzuri iliyotengenezwa na mafuta ya mbuzi na mahindi ya njano, au, kama anavyopendelea zaidi, kupikwa ndani ya ganda na kuunganishwa na jibini ya mbuzi.
“Yalilisha mababu zangu, na hata wakati hali ilikuwa mbaya, maharagwe ya Guajiro yalikuwa chanzo chetu kikuu cha chakula,” anasema, akirejelea madhara makubwa ya mabadiliko ya tabianchi yaliyoathiri eneo hilo.
Uhakika wa chakula wa karne nyingi kuharibiwa.
"Miaka ishirini iliyopita, mabadiliko ya tabianchi yaliathiri uhakika wa chakula wa karne nyingi kwa Wayúu wakati mzunguko wa msimu wa mvua na kiangazi ulipoacha kuwa thabiti kufuatia kuibuka kwa El Niño na El Niña na mambo mengine ya tabianchi yanayoendeshwa na mabadiliko ya joto." - Bwana Montiel
Mvua haiji inapopaswa.
Ukame mkali uliikumba La Guajira kati ya mwaka 2012 na 2016, ukiharibu maisha ya zaidi ya wakazi 900,000, wakiwemo takriban Wayúu 450,000. Utapiamlo, magonjwa na vifo vya watoto vilienea, mazao yalikauka, na mbegu za asili zilitoweka. Asilimia 60 ya mifugo ilikufa, hali ambayo ilivunja uti wa mgongo wa uchumi wa Wayúu.
“Miaka ishirini iliyopita, tulipokuwa tukijua ni lini mvua ingekuja, tulihifadhi chakula kwa ajili ya wanyama wetu na kingetutosha hadi msimu wa baridi ujao,” anasema Bwana Montiel. “Lakini sasa, wanyama katika jamii nyingine wanakufa kwa sababu mimea inaanza kukauka mapema, na mvua haiji inapopaswa.”
Kutoka majangwa hadi kugeuka mabwawa
Sasa, jamii kama Ipaharrain zinageuza maeneo ya jangwa kuwa mabwawa, kwa msaada wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) na washirika wake. Zaidi ya hayo, mbinu na maarifa ya jadi yenye mnepo ya Wayúu pia yanarekodiwa ili kushirikiwa na mataifa yenye dhamira ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi, kupitia mradi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP), unaojulikana kwa kifupi kama SCALA.
Hadi sasa, matokeo ni ya kupendeza na mengi. Ipaharrain imetenga nusu ekari kwa ajili ya uzalishaji wa chakula pekee, mahali pa kijani kibichi kinachohifadhiwa kwa kutumia pampu zinazoendeshwa kwa nishati safi na umwagiliaji wa tone baada tone, ukichota maji kutoka kisima kilichohuishwa.
Mabwawa mengine kama hayo yanaibuka huku wahandisi wa FAO wakifanya kazi na zaidi ya jamii 50, ambapo wanafuata mbinu za kilimo zenye ufahamu wa mabadiliko ya tabianchi ili kuendana na tamaduni na muktadha wa kijamii, huku wakitambua na kuingiza maarifa ya jadi ya watu wa kiasili, mifumo ya matumizi na desturi za kihistoria za uzalishaji.
Maarifa ya jadi yanakutana na ubunifu.
Ili kuboresha mnepo wa Wayúu katika hali ya mabadilikoya tabianchi inaendelea kuwa kali zaidi, juhudi zinaelekezwa kwenye kutafuta suluhisho zenye ustahimilivu kwa changamoto zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi, kwa mujibu wa Jorge Gutiérrez, mratibu wa FAO kwa mradi wa SCALA nchini Kolombia.
Mbinu za jadi sasa zinakutana na ubunifu mpya kupitia mchakato wa majaribio na makosa ambao umepata matokeo mazuri, kuanzia usimamizi wa udongo hadi uzalishaji wa chakula endelevu.
Kutambua utegemezi wa Wayúu kwenye mvua kumesaidia kuboresha visima vilivyopo na kuunda mabwawa ili kuwezesha umwagiliaji wa aina ya matone kwa matone. Wachungaji wa mbuzi wa jadi sasa wanatumia kinyesi cha wanyama kilichochanganywa na madini, majivu, na vihifadhi maji ili kuimarisha udongo na kutoa virutubisho muhimu kwa mazao na mbegu za asili
Bioanuwai ya kilimo katika vitendo
Matokeo haya yanaonesha nguvu ya bioanuwai ya kilimo katika vitendo, anafafanua Gutiérrez.
“Wakati FAO haitakuwa hapa tena, tutakuwa na uhakika kwamba wamejenga mzunguko mzima, virutubisho, mbegu, majaruba ya mbegu, maeneo ya miche, na usimamizi wa maji ambao baada ya muda utakua hali ya kawaida katika maisha yao ya kila siku.” - Gutiérrez
Wakati huo huo, baadhi ya jamii za Wayúu zimeongeza mazao mapya kama vile mrehani, mabiringanya, na nyanya katika bustani zao za jadi za maharagwe, mahindi, maboga, na matikitimaji, aina ya utofauti zinayoboresha uhakika wa chakula, zikitoa kinga dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi na kuwawezesha Wayúu kuboresha lishe yao na ustawi wa kiuchumi.
“Tunarudisha maarifa ya jadi kuhusu ardhi kupitia mbegu za kienyeji ambazo pia zina ustahimilivu,” anasema Gutiérrez. “Mazungumzo ya mbegu za jamii yanahakikisha kwamba watoto katika eneo hili, ambao kwa bahati mbaya wamepitia changamoto kubwa katika miaka ya hivi karibuni, wataona maboresho katika hali zao za lishe na chakula.”
Mbinu mpya zimepelekea baadhi ya jamii kuwa na ziada ya maharagwe ya Guajiro ambayo wanaweza kuuza au kufanyia biashara ya kubadilishana bidhaa, anasema Gutiérrez, akiongeza kwamba juhudi za sasa zinazoungwa mkono na Umoja wa Mataifa zinalenga kupambana na njaa na kuacha urithi wa maeneo ya chakula katika La Guajira.
“Wakati FAO haitakuwa hapa tena, tutakuwa na uhakika kwamba wamejenga mzunguko mzima; virutubisho, mbegu, vitanda vya mbegu, maeneo ya miche, na usimamizi wa maji ambao baada ya muda utakua hali ya kawaida katika maisha yao ya kila siku.”
Maarifa ya jadi ni hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Kurudi katika kijiji cha Ipasharrain, Bi. Gonzalez anashiriki neno la kuaga kabla ya kuigeukia sahani yake ya maharagwe.
“Tuna shukrani kuwa na chakula hiki chote sasa,” anasema. “Hapo awali, ilibidi tungoje mvua ili tuweze kupanda au kupata maji ya kunywa. Sasa, tuna kisima na chakula mwaka mzima.”
Bi. Gonzalez na jamii yake pia wamechukua hatua muhimu katika kujenga ustahimilivu katika mapambano yanayoendelea dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.