Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi ya anga ya Israel yalazimisha kampeni ya chanjo kusitishwa Gaza Kaskazini: UN

Wanajeshi wa Israel walipiga mahema ya kuwahifadhi raia waliokimbia makazi yao karibu na hospitali ya Al-Aqsa katika eneo ambalo watu kutoka kaskazini mwa Gaza waliambiwa kuhamia.
UN Wanajeshi wa Israel walipiga mahema ya kuwahifadhi raia waliokimbia makazi yao karibu na hospitali ya Al-Aqsa katika eneo ambalo watu kutoka kaskazini mwa Gaza waliambiwa kuhamia.

Mashambulizi ya anga ya Israel yalazimisha kampeni ya chanjo kusitishwa Gaza Kaskazini: UN

Afya

Mashambulizi makali ya anga kutoka kwa jeshi la Israel, idadi kubwa ya watu kutawanywa na ukosefu wa fursa ya kufika Gaza Kaskakzini vimelazimisha kuahirishwa kwa kameni ya chanjo kwa mujibu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la Afya Duniani WHO, la kuhudumia watoto UNICEF na la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA.

Kampeni hiyo iliyoahirishwa ilitakiwa kuanza leo na ni duru ya mwisho ya chango ya kampeni iliyolenga kuwachanja watoto 119,279 kote Gaza Kaskazini kwa dozi ya pili ya chanjo ya polio aina ya nOPV2, lakini hali ya sasa imefanya iwe vigumu kwa familia kupeleka watoto wao kwenye vituo vya chanjo, na kwa wahudumu wa afya kuendesha huduma kwa usalama.

Mashambulizi ya makombora yanayoendelea dhidi ya miundombinu ya kiraia yamepunguza maeneo yanayokubaliwa kwa usitishaji wa uhasama kwa mnajili ya masuala ya kibinadamu kuwa kwenye Jiji la Gaza pekee, ikilinganishwa na wakati wa awamu ya kwanza ya chanjo iliyofanyika tarehe 1-12 Septemba 2024.

Vikosi vya Israel vililenga na mikombora mahema ya kuwahifadhi raia waliokimbia makazi yao karibu na Hospitali ya Al-Aqsa, katika eneo ambalo watu kutoka kaskazini mwa Gaza waliambiwa kuhama.
UN Vikosi vya Israel vililenga na mikombora mahema ya kuwahifadhi raia waliokimbia makazi yao karibu na Hospitali ya Al-Aqsa, katika eneo ambalo watu kutoka kaskazini mwa Gaza waliambiwa kuhama.

Hatari yakutofikia lengo la chanjo

Hali hii inahatarisha kufikiwa kwa lengo la angalau asilimia 90 ya watoto kuchanjwa, jambo ambalo ni muhimu ili kukomesha usambaaji wa virusi vya polio na kulinda afya za watoto.

WHO na UNICEF wamesema kuwa kucheleweshwa kwa chanjo ya polio kunaweza kuongeza hatari ya virusi kuenea zaidi Gaza na maeneo Jirani na kuchelewesha utoaji wa dozi ya pili ya chanjo ndani ya wiki sita kunapunguza uwezo wa chanjo hiyo kuimarisha kinga za watoto na kuzuia maambukizi.

Tangu duru ya pili ilipoanza tarehe 14 Oktoba 2024, jumla ya watoto 442,855 wenye umri wa chini ya miaka kumi wamefanikiwa kuchanjwa katika maeneo ya kati na kusini mwa Gaza.

Usitishaji uhasama ni muhimu

UNICEF na WHO wanatoa wito kwa pande zote zinazohusika katika mzozo kutekeleza usitishaji mapigano  wa kibinadamu na kuhakikisha kuwa raia, wahudumu wa afya, na miundombinu ya kiraia kama shule na hospitali inakingwa dhidi ya mashambulizi.

Mashirika hayo yamesisitiza umuhimu wa kuanza tena kampeni ya chanjo mara moja ili kuzuia kupooza kwa watoto na kuimarisha kinga dhidi ya polio.

Katika juhudi za kuhakikisha huduma bora, takribani watoto 357,802 pia walipatiwa virutubisho vya vitamini A kama sehemu ya juhudi za kuunganisha chanjo ya polio na huduma zingine muhimu za afya.

Mashirika ya WHO na UNICEF ymesisitiza kuwa kusitisha vita na kuwezesha chanjo ni hatua muhimu ili kuzuia mlipuko wa polio kuendelea na kulinda afya ya watoto wote Gaza.

Umoja wa Mataifa, kwa ushirikiano na mamlaka ya afya ya Palestina, ilianza kutoa chanjo kwa watoto 640,000 katika Ukanda wa Gaza mwezi Septemba. (Maktaba)
© UNRWA/Mohamed Hinnawi Umoja wa Mataifa, kwa ushirikiano na mamlaka ya afya ya Palestina, ilianza kutoa chanjo kwa watoto 640,000 katika Ukanda wa Gaza mwezi Septemba. (Maktaba)

Kurejea kwa polio Gaza

Baada ya kutokomeza ugonjwa huo wa polio robo karne iliyopita, Gaza iliripoti kisa chake cha kwanza cha polio mapema mwaka huu, moja ya matokeo ya vita ya mwaka mzima na kuzingirwa kwa Ukanda huo, ambao umeshuhudia kuwekewa vikwazo vya utoaji wa misaada, uharibifu na vikwazo vya upatikanaji, kwa huduma muhimu za maji na usafi wa mazingira na msongamano wa watu katika makazi ya muda unaoendeshwa na maagizo ya mara kwa mara ya Israel ya kuwataka watu kuhama.

Kurejea huko kwa polio kulisababisha hatua za haraka za WHO na washirika kuzindua kampeni katika Ukanda huo ulioharibiwa na vita.

Ili kukomesha maambukizi ya virusi vya polio na kuenea kwake, angalau asilimia 90 ya watoto wote katika kila jamii na ujirani lazima wapewe chanjo.

Polio husababisha kupooza na dalili nyingine mbaya na inaweza kusambaa kwa haraka.