MONUSCO imetuondoa mtaani, asema mkuu wa RTNC Beni, DRC
MONUSCO imetuondoa mtaani, asema mkuu wa RTNC Beni, DRC
Ikumbukwe kuwa kituo cha Redio na Televisheni ya Taifa RTNC mjini Beni, jimboni Kivu Kaskazini, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, kilikuwepo tangu Mei 2014, lakini mnamo 2019 tulikuwa na shida ya kulipia pango na tukafukuzwa, anasema Alexis Jacques Maseseme, Kiongozi wa kituo hicho ambacho sasa kimerejea hewani kwa msaada wa Umoja wa Mataifa.
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO kilitumia dola 50,000 za kimarekani kurejesha hewani matangazo na pia ofisi za RTNC mjini Beni baada ya kutokuweko hewani kwa miaka mitano.
Msaada ni vifaa kama vinasa sauti na paneli za nishati ya jua
MONUSCO iliwezesha ujenzi wa majengo ya kisasa, samani na vifaa vya kiufundi ikiwa ni pamoja na paneli za nishati ya jua, kompyuta, mashine za kunasa sauti.
Hivi vilitolewa ili kufanikisha utendaji kazi mzuri wa redio na televisheni hiyo hasa kwenye suala la kukabiliana na habari potofu na za uongo, wakati huu ambapo kushamiri kwa mapigano mashariki mwa nchi kunaambatana pia na habari potofu na za uongo kutoka vikundi vilivyojihami.
Bwana Maseseme anaeleza kwamba baada ya kushindwa kulipa pango la nyumba, mwaka 2019 “tulifukuzwa na tukajikuta tuko mtaani. Mwezi Julai mwaka 2024 tulianza tena matangazo kutokana na msaada wa MONUSCO. Ilitufanyia jambo kubwa sana kwa sababu tulikuwa mtaani kama nilivyosema, na ndivyo ilivyo shukrani kwa MONUSCO kwamba tuko katika majengo haya mazuri, ambayo ni kontena MONUSCO ilitupatia, na yenyewe ikabadilisha kuwa ofisi.”
Amesema wamejipanga na wana safu nzuri ya wahariri. Wanasongesha harakati za serikali kukwamua wananchi na pia habari za wananchi zinapatiwa kipaumbele.
Mkuu huyo wa RTNC- Beni akatoa shukrani kwa Umoja wa Mataifa akisema “tunashukuru msaada huu, vinginevyo tungekuwa bado tuko mitaani lakini tumerejea, tunayo anwani yetu sasa. Kituo cha RTNC-Beni kimerekebishwa na tuko kwenye kiwanja chetu. tayari ni kubwa ndicho kilichofanywa na MONUSCO. "
Alipoulizwa iwapo wametosheka na msaada uliotolewa, Bwana Maseseme akasema, “mahitaji hayana ukomo. Bado tuna mahitaji kwa mfano waandishi wetu wa habari inabidi waende mashinani kutafuta habari za wananchi, Hatuna usafiri. Tukiweza kupata chombo cha usafiri itakuwa bora zaidi.”
RTNC itanipatia taarifa kuhusu amani hapa kwetu
Baada ya kuzungumza na mkuu huyo wa kituo, mwandishi wetu aliingia mtaani Beni kupata maoni ya wananchi ambapo mmoja wao Kavira Vakekya amesema, “"RTNC ilikuwa imetufungia na kutunyima taarifa za serikali, sasa tulipojua kwamba imefungua milango yake ni furaha kwetu kwa sababu tutakuwa na taarifa za serikali na tunaenda kusikia yanayoendelea nchini na hasa katika mji wetu ambao unasumbuliwa na mauaji.”
Amesema anaamini kwamba RTNC “inatupa habari za kweli na sio za uongo. Tunaamini kwamba tunapewa taarifa nzuri na ndiyo maana tunafurahi kusikiliza RTNC".
Mwingine ni Moïse Movambi, yeye ni mkimbizi na anasema ailifurahi sana alipopata habari za kurejea kwa RTNC kwa sababu “RTNC inatupa habari halisi na inatufahamisha kuhusu kile kinachotokea katika jiji letu la Beni. itatufahamisha ili kujua ni lini amani itarudishwa kwetu, kutokana na habari hii nitajua kwamba napaswa pia kurudi nyumbani kwetu".