Kuna muafaka kwa nachi wanachama Afrika inastahili viti 2 Baraza la Usalama: Guterres
Kuna muafaka kwa nachi wanachama Afrika inastahili viti 2 Baraza la Usalama: Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres yuko Addis Ababa Ethiopia ambako leo, ameshiriki katika mkutano wa 8 wa kila mwaka wa Muungano wa Afrika AU na Umoja wa Mataifa.
Majadiliano hayo ya ngazi ya juu, yaliyoongozwa na Mwenyekiti Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Muungano wa Afrika na Katibu Mkuu, “yamelenga maendeleo katika utekelezaji wa mifumo ya ushirikiano kati ya mashirika hayo mawili, pamoja na uendeshaji wa Baraza la Usalama. azimio namba 2719, ambalo linaweka mfumo wa kufadhili shughuli za usaidizi wa amani zinazoongozwa na Muungano wa Afrika kupitia michango iliyotathminiwa na Umoja wa Mataifa.”
Washiriki pia wamejadili hatua za pamoja, pamoja na changamoto zinazohusiana na amani, usalama, maendeleo, haki za binadamu na athari za mabadiliko ya tabianchi katika bara la Afrika.
Majadiliano pia yamejumuisha utekelezaji wa Mkataba wa Zama Zijazo.
Mkutano na waandishi wa habari
Katika ziara hiyo Katibu Mkuu na Moussa Faki Mahamat, wamekuwa na mkutano wa pamoja na waandishi wa habari ambapo Guterres amesisitiza umuhimu wa kuendelea kwa ushirikiano kati ya mashirika hayo mawili tunapoanza utekelezaji wa Mkataba wa Zama Zijazo.
Pia ametoa pongezi kwa Mwenyekiti, ambaye anatazamiwa kumaliza majukumu yake baada ya miezi michache ijayo.
Katibu Mkuu pia amepata fursa ya kutoa hotuba kwenye Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Afrika UNECA, wakati wa hafla ya uzinduzi wa ukumbi uliokarabatiwa wa Afrika. Ukumbi huu ndio ambapo Afrika iliungana kuupa uhai Umoja wa Afrika, ambao sasa ni Muungano wa Afrika, amesema Katibu Mkuu alisema.
Guterres ameongeza kuwa "Jumba hili ni daraja kati ya wakati uliopita na ujao wa Afrika, ni sanaa ya aina yake, kituo cha karne ya 21 ambacho kinahifadhi uzuri na historia ya bara hili kubwa".
Kuhusu Baraza la Usalama
Kuhusu Mabadiliko katika Baraza la Usalama Guterres amesema ni suala lililo bayana kwamba ni muhimu na lazima yafanyike kwa manufaa ya nchi wanachama.
"Sasa kuna maafikiano kutoka kwa Nchi Wanachama kwamba Baraza la Usalama lazima lifanyiwe mageuzi, na kuna makubaliano ya Nchi Wanachama wote kwamba kipengele muhimu cha mageuzi hayo ni kuwa na wajumbe wawili wa Afrika kama wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama."
Pia akiwa mjini Addis Ababa, Katibu Mkuu amefanya mikutano na Rais Sahle-Work Zewde na Waziri Mkuu Abiy Ahmed wa Ethiopia.